NINI HATMA YA MGOGORO WA WAPALESTINA NA WAYAHUDI?
- NANI ANAPASWA KUWA MMILIKI HALALI WA NCHI HIYO?
- JUHUDI ZA USULUHISHI ZITAFANIKIWA?
NA JOSEPH MWAMBIJE
Mgogoro
uliopo kati ya Wayahudi(Waisraeli) na Wapalestina umeigawanya dunia
ambapo wapo wanaoamini kuwa Wayahudi ndio wanaopaswa kuwa wamiliki
halali wa Nchi ya Israeli na wapo wanaoamini kwamba Wapalestina ndio
wanaopaswa kuikalia Nchi hiyo kama Nchi yao .
Kwa watu wengine Wayahudi wanaonekana ni watu wakatili wanaoikalia Nchi hiyo kimabavu huku wakiwanyanyasa Wapalestina.
Wakati baadhi ya watu wanadai Wayahudi ndio wenye Nchi hiyo na
Wapalestina wanaonekana ni Magaidi na watu wakorofi wanaowanyanayasa
Wapalestina.Baadhi ya Wasomi na wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanaona
kwamba Wapalestina wanatendewa visivyo.
Baadhi
ya Waislamu wao wanalichukulia suala la kunyanyaswa Wapalestina kuwa
ni la mgogoro wa kidini na kwamba Wapalestina wananyanyaswa kwasababu ya
Uislamu wao.
Kimsingi mgogoro wa Wayahudi na Wapalestina umegawanyika kidini na
kisiasa. Waisraeli ndio wenye Nchi kidini lakini kisiasa Wayahudi au
Waisraeli ni wakoloni wanaoikalia Nchi ya Wapalestina kimabavu.
Imeshindwa kueleweka kwamba mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina
utatatuliwa kwa njia gani kwani Mataifa haya mawili yote yanaonekana
kufanya harakati kwa njia zinazotafsiriwa kuwa za kigaidi.
Wengine wamekuwa wakiilaumu Marekani kwamba inawapendelea Waisraeli
kitu ambacho mimi naona si kweli kulingana na mgogoro wenyewe, ila
ninachokiamini hapa ni ugumu wa mgogoro wenyewe.
Yameandikwa mengi kuhusiana na mgogoro huo na kila mmoja ametoa maoni
yake namna ya kutatua mgogoro huo. Imeundwa mikataba mingi ili kuleta
amani katika Nchi hiyo na eneo la Mashariki ya Kati.
Wapalestina wamekuwa wakidai kunyanyaswa na Waisraeli kwa kupigwa na
kutemewa mate usoni mbele ya watoto wao kitu kinachowafanya wakate tama
na kujitoa muhanga kwa kujiua wenyewe ili mradi wameuwa Wayahudi kadhaa.
Mbinu hiyo ya Wapalestina sijui walifundishwa na nani kwani inaonekana
ni ya kujidhalilisha zaidi kuliko kutetea maslahi yao .
Pengine tuyaangalie madai ya Wapalestina yanayowafanya wapambane na
Waisraeli kufa na kupona. Kimsingi Wapalestina wanapigania haki ya
kuwepo Taifa kamili la Kipalestina, Mji wa Jerusalemu ambao ndio
wanadai Mji Mkuu wa Nchi yao na kurudi kwa Wapalestina zaidi ya Milioni 5
ambao ni wakimbizi katika Nchi mbalimbali Duniani ambapo kwa sheria za
Israeli hawaruhusiwi kurudi Palestina bila kibali maalumu.
Watu wengi wamekuwa wakijiuliza nini hatma ya mgogoro wa Waisraeli na
Wapalestina. Kila mmoja anatoa majibu yake jinsi anavyoufahamu mgogoro
huo. Hata hivyo majibu ya msingi ya namna ya kutatua mgogoro huo
yanakosekana.
Kufuatia mgogoro huo maswali ya msingi yamekuwa yakijitokeza na watu
wengi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi bila majibu,baadhi ya maswali
hayo ni kwa nini Waisraeli na Wapalestina wanashindwa kuelewana, nani
atamaliza mgogoro wa Mataifa hayo na Je mgogoro baina ya Mataifa hayo
utakwisha na je Wapalestina wataweza kujikwamua kwenye makucha ya
Waisraeli?.
Mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina una mlolongo mrefu sana
uliochanganyika na udini ndani yake na ambao unawachanganya watu wengi
na kuwaachia maswali mengi.
Kama nilivyosema awali kwamba kuna Mikataba mingi iliundwa ili kujaribu
kuleta amani katika Nchi hiyo ya Palestina huko Mashariki ya Kati. Moja
ya mikataba iliyoundwa na inayokumbukwa ni Mkataba wa Oslo ambao
ulisainiwa katika Hoteli ya Plaza Mjini Oslo Norway Septemba 13, 1993.
Mkataba huo ulipingwa na baadhi ya wasomi wa kiarabu wakidai una kasoro
nyingi na baadhi ya wasomi hao walidai kuwa mkataba huo uliokuwa na
vifungu 17 na kurasa 14 za ufafanuzi ulikuwa na mapungufu mengi.
Wasomi hao walisema upungufu wa kwanza katika mkataba huo ni
kuwaondolea Wapalestina hadhi ya kuwa Taifa kamili na kuishia kuwapa
uwezo wa kuwa na mamlaka ya ndani (Internal Palestinian Authority ).
Upungufu wa pili wasomi hao walisema mazungumzo ya mkataba huo
hayakugusia lolote kuhusu hatma ya Mji wa Jerualem ambapo Wapalestina
wamekuwa wakiupigania sambamba na Taifa lao.
Wapalestina wanadai Jerusalem ndio makao yao makuu na kwamba utakuwa
Mji Mkuu pindi watakapounda Taifa lao. Wasomi hao walisema mkataba
utakaokwepa kuzungumzia hatma ya Jerusalem watakwepa kuuzungumzia.
Kimsingi mkataba huo wa Oslo haukuweza kutatua matatizo baina ya
Waisraeli na Wapalestina zaidi ya kuongezea matatizo na lawama nyingi
kumwangukia aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina wa wakati huo Marehemu
Yasser Arafat kwa kuukubali mkataba huo.
Manyanyaso ya Waisraeli dhidi ya Wapalestina yalipelekea kuundwa kwa
chama cha Ukombozi wa wapalestina PLO, kilichoongozwa na Marehemu Ysser
Arafat. Karibu Nchi zote zilizokuwa zikitawaliwa hapa duniani
zimejikomboa kutoka kwenye makucha ya wakoloni na kujitawala, swali ni
kwamba ni lini Wapalestina watapata Uhuru wao?.
Je watumie njia gani kuwatimua Waisraeli kwenye Nchi wanayodai ni ya
kwao, je watumie mtutu wa Bunduki ambao ulishindwa kwenye vita ya Mwaka
1967 iliyojulikana kama vita ya siku saba, pale Waarabu walipoungana ili
kuwaondoa Waisraeli katika Nchi hiyo ya Mashariki ya Kati. Je watumie
mdomo kuwabembeleza Waisraeli kuondoka Nchini humo na kama wakiondoka
watakwenda kuishi wapi? Hayo ni maswali magumu kujibiwa.
Kisiasa Waisraeli wanaonekana ni walowezi na wakoloni ambao wanaikalia Nchi isiyo yao kimabavu na wanaonekana
ni watu wakatili na wasio na huruma kwa wenyeji wao Wapalestina.
Wanaonekana kama wakaburu wa Afrika ya Kusini katika miaka ya nyuma au
Wareno katika Nchi ya Msumbiji katika enzi za ukoloni. Lakini la
kujiuliza ni kwamba hawa ni wakoloni wa aina gani wanaotaka kukaa kwenye
Nchi ya wenzao milele licha ya kelele zinazoambatana na machozi ya
mamba za baadhi ya Mataifa makubwa ya Ulaya.
Baadhi ya wasomi na wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema Wapalestina
ndio wanaopaswa kuikalia kihalali Nchi hiyo ya Palestina na kwamba
Wayahudi walifika tu hapo na kuikalia Nchi hiyo.
Hebu tuangalie kidini Taifa hili la Israeli kwa kuangalia Kitabu
Kitakatifu cha Biblia na baadhi ya vitabu vya dini. Kimsingi Taifa hili
lenye nguvu za kijeshi linaanzia kwa mtu mmoja anayeitwa Abramu ambaye
baadaye alibarikiwa na Mungu na kuitwa Ibrahimu.
Baadhi ya maandiko toka kwenye Biblia yanasema mimi agano langu
nimelifanya nawe, nawe utakuwa Baba wa Mataifa mengi wala jina lako
hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu kwani
nimekuweka uwe Baba wa Mataifa mengi.
Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana , nami nitakufanya kuwa Mataifa, na
wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na
wewe na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa Agano la milele,
kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baba yako. Nami nitakupa
wewe uzao wako baada yako Nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kaanani
kuwa milki yako ya milele. (Mwanzo 17:4-7).
Mungu alimtokea Ibrahimu wakati akiwa na miaka 100 na mkewe Sarai akiwa
na miaka 90 na kusema, Sarai mkeo hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa
jina lake ataitwa Sara. Nami nitambariki na tena nitakupa mwana kwake,
naam nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa na wafalme wa kabila
watatoka kwake. (Mwanzo 17:15-16).
Baada ya kuambiwa maneno hayo na Mungu Ibrahimu na Sara hawakuamini
kwani walikuwa wazee na miaka yote waliishi bila kupata mtoto ambapo
Sara alikuwa tasa. Licha ya mashaka hayo waliyokuwa nayo Ibrahimu na
Sara lakini Mungu aliwasisitiza kwamba watapata mtoto ambaye watamwita
Isaka.
Kwa Mungu hakuna linaloshindikana baada ya muda ule uliotamkwa na Mungu
kwamba Sara angepata mimba akapata mimba na kumzalia Ibrahimu mtoto wa
kiume katika uzee wake. Ibrahimu akamwita mtoto huyo Isaka kama Mungu
alivyosema (Mwanzo 21:1-3).
Kimsingi Ibrahimu ambaye Baba yake aliitwa Tera ndio Msingi mkubwa wa
Taifa hili. Isaka alizaa watoto wawili mapacha, akawaita Esau ambaye
alikuwa mkubwa yaani Kulwa na mdogo aliitwa Yakobo, yaani Doto. Kama
ilivyo kwa mama yake pia mke wa Isaka aliyeitwa Rebeka alikuwa Tasa,
watoto hao aliwapata baada ya kumwomba Mungu (Mwanzo 25:21,24:26).Esau
alikuwa mwindaji hodari wakati Yakobo alitulia nyumbani. Isaka alimpenda
Esau lakini Rebeka mkewe alimpenda Yakobo.
Wakati Isaka alipokuwa Mzee akikaribia kufa akataka kumbariki mwanaye
mkubwa Esau kutokana na uzee Isaka alikuwa amepofuka macho. Ilikuwa
desturi za wakati ule Baba kumbariki mwanaye wa kwanza kabla ya kufa.
Isaka akamwita mwanaye wa kwanza, Esau na kumweleza kwamba yeye ameshakuwa mzee hivyo anataka
kumbariki kabla hajafa, akamwambia amfanyie chakula kitamu kabla
hajambariki kama ilivyokuwa desturi ya wakati huo. Esau alipoambiwa hayo
akaenda nyikani kuwinda ili amtengenezee Baba yake nyama kama
alivyomuagiza.
Wakati Isaka akizungumza na Esau ndani Rebeka alisikia na akamwita
Yakobo na kumwambia nimemsikia baba yako akimwambia Esau akatafute
mawindo amfanyie chakula ili apate kumbariki.
Rebeka akamwambia Yakobo akamletee mbuzi wawili ili akamtengenezee na
akampe baba yake ili apate kumbariki. Kulikuwa na mabishano kati ya
Yakobo na Mama yake ambapo Yakobo akamwambia Mama yake kwamba Esau ni
mtu mwenye malaika (Vinyoleo) kifuani na mikononi hivyo baba yake
atakapompapasa na kugundua yeye si Esau atamlaani hivyo laana haiwezi
kuwa mbaraka, lakini mama yake akamwambia laana hiyo iwe juu yake.
Yakobo akafanya kama mama yake alivyomuagiza akamletea mbuzi wawili.
Mama yake akawatengeneza Mbuzi hao na kuchukua mavazi ya Esau mwanawe
mkubwa na kumpa Yakobo ayavae, wakati hayo yote yakifanyika Esau alienda
porini kuwinda.
Mama yake Yakobo akachukua ngozi ya Mbuzi na kumvika Yakobo mikononi na
kumpa nyama ya Mbuzi iliyotengenezwa vizuri na mikate akampe Baba yake.
Yakobo alipofika mbele ya Baba yake akasema nimefika Baba na nimefanya
kama ulivyoniagiza.
Yakobo akamwambia baba yake inuka ule ili unibariki. Baba yake
alipomuuliza wewe ni nani Yakobo akasema mimi ni Esau mzaliwa wako wa
kwanza. Isaka Baba yake akamuuliza imekuwaje umefanya haraka namna hii,
Yakobo akajibu Bwana Mungu wako amenifanikisha.
Yakobo akamwambia Baba yake inuka unipapase, naye alipompapasa mikononi
akasema mikono ni ya Esau lakini Sauti ni ya Yakobo maana hakumtambua.
Baada ya kula Isaka akambariki mwanaye.
Yakobo
alipotoka tu Esau naye akawa anaingia kutoka katika mawindo yake. Esau
akamwambia Baba yake ondoka ule mawindo yangu ili unibariki. Isaya
akamuuliza U’ nani wewe, akamjibu mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza.
Isaka akatetemeka na kushangaa na kuhoji ni nani aliyekuja na mawindo
akaniletea, nami nimeshakula kabla hujaja wewe, nikambariki, naam naye
atabarikiwa.
Baada ya kuambiwa maneno hayo Esau akalia kilio kikuu akisema nibariki
na mimi, Isaka akamjibu ndugu yako amekuja kwa hila na kuchukua mbaraka
wako. Baada ya hayo Esau akamchukia sana Yakobo na akapanga kumuua.
Rebeka Mama yao Esau na Yakobo aliposikia kwamba Esau anapanga kumuua
Yakobo alimwambia Yakobo mwanae akimbilie Harani kwa Lutu ndugu yake.
Akamwambia akae huko hadi hasira ya ndugu yake itakapopungua na
atakaposahau aliyotendewa. (Mwanzo 27:1-46) Kimsingi alikokimbilia
Yakobo ni sehemu za Mashariki ya Kati ya leo.
Yakobo akiwa huko katika Nchi ya ugeni malaika wa Mungu alimtokea na
kuongea naye na kumuuliza jina lake anaitwa nani. Akamjibu kuwa anaitwa
Yakobo. Malaika akamwambia hutaitwa tena Yakobo bali utaitwa Israeli
(Mwanzo 32:27-28).
Kimsingi Taifa la Israeli ambalo linasuguana na Wapalestina huko
Mashariki ya Kati linaanzia hapo. Ni habari za uhakika kwamba Mungu
alilibariki Taifa hilo katika msingi wa kidini na si wa kisiasa na asili
ya dini ya kikristo ni kutoka Taifa hilo ambalo Biblia imelitaja kama
Taifa teule la Mungu.
Mungu aliliteua Taifa hilo kama chanzo cha kufikisha Injili yake kwa
mataifa mengine, ndio maana Wayahudi walikuwa hawachangamani na Mataifa
mengine hadi alipokuja Yesu kuondoa utengano huo na kuwaambia Wayahudi
wasiwaite Najisi wale walioumbwa na Mungu.
Uteule wa Wayahudi kidini kama Taifa teule la Mungu ulikoma baada ya
kumkataa Yesu na kumsulubisha msalabani na kumuua Mtume wake aliyeitwa
Stephano. Kuanzia hapo sasa Injili iliwageukia Mataifa, yaani watu
wengine wasio Wakristo na katika Dunia yote na ndio maana Wakristo
wengine wanajiita Waisraeli wa Kiroho.
Lakini licha ya Wayahudi kumkataa Yesu hawakunyang`anywa mibaraka
waliyopewa pamoja na nguvu za kijeshi walizopewa. Istoria ya awali
inaonyesha kwamba mapigano kati ya waisraeli na Waarabu ni ya muda
mrefu, pengine tunaweza kuyaita mapigano yao kuwa ya Jadi. Kwa mujibu wa
Kitabu Kitakatifu cha Biblia, mapambano hayo yamekuwa yakitegemeana
ambapo mara nyingine Waisraeli walikuwa wakipigwa na mara nyingine
Wapalestina walikuwa wakipigwa.
Taifa hilo Teule limepitia katika mlolongo mrefu sana wa kutekwa na
Mataifa mengine kama adhabu iliyotolewa na Mungu kuliadhibu Taifa hilo .
Waisraeli walikuwa watu wa kuhama hama wakitafuta mahali panapowafaa
kwa kuishi.
Katika kulielezea Taifa la Israeli hatuwezi kuacha kuelezea habari za
mtu mmoja aitwae Yusufu. Huyu alikuwa mtoto wa mwisho wa Yakobo. Alikuwa
kijana mwenye miaka 17 kwa wakati huo, pia alikuwa mzuri wa sura
(Handsome). Katika hatua za awali alionekana kwamba angekuwa mtu mkubwa
kwa nyadhifa baadaye kwani alikuwa akiota ndoto za ajabu ajabu ambazo
ziliashiria hilo .
Baba yake alimpenda kuliko watoto wake wote. Alimshonea vazi zuri.
Baada ya kushonewa vazi hilo wivu uliibuka toka kwa ndugu zake. Siku
moja Baba yake alimtuma Yusufu kuwapelekea chakula ndugu zake machungani
walikokuwa wakichunga. Walipomwona kwa mbali akija wakasemezana tazama
mwota ndoto yule anakuja, tumuue.
Kaka yake aliyeitwa Reuben akasema tusimuue bali tumtupe humu kwenye
shimo. Wakachukua chakula wakamvua kanzu yake na kumtupa kwenye shimo.
Wakati wakila chakula waarabu wakapita wakielekea Misri ndipo ndugu zake
wakashauriana na kumuuza kwa Waarabu.
Ndugu za Yusufu wakamuuza Yusufu kwa vipande 20 vya fedha. Waarabu
wakamchukua Yusufu hadi Misri. Ndugu hao wa Yusufu wakachinja Kondoo na
kuirarua kanzu ya Yusufu na kumwagia damu ya Kondoo. Waliporudi
wakamwambia Baba yao kwamba mnyama mkali amemla Yusufu. (Mwanzo
37:5-36).
Yusufu alipopelekwa Misri alipandishwa cheo na kuwa Waziri Mkuu
kutokana na kipaji alichokuwanacho cha kutafsiri ndoto ambapo alitafsiri
ndoto aliyoota Farao juu ya miaka 7 ya mavuno na miaka 7 ya njaa.
(Mwanzo 40:1-57).
Kwa mujibu wa Kitabu Kitakatifu cha Biblia ni kwamba baada ya miaka 7
ya mavuno kupita kulikuwa na njaa katika Dunia yote isipokuwa Nchi ya
Misri ambako walihifadhi chakula wakati ule wa miaka 7 ya Neema(mavuno).
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Taifa la Israeli kwenda utumwani Misri kwani
kulipokuwa na njaa katika Nchi ya Israeli Yakobo na wanawe walihamia
Misri ambako waliishi kwa raha mustarehe hadi alipokuja Farao
asiyemtambua Yusufu (Mwanzo 46:8-27).
Waisraeli wakaanza kuzaana kwa kasi kuwashinda Wamisri wakati wana wa
Israeli wakiendelea kuzaana akainuka Farao mpya asiyemfahamu Yusufu na
kuwaambia Wamisri angalieni Waisraeli wengi tena wana nguvu kuliko sisi.
Farao akasema tunapaswa kutumia akili kwani ikitokea vita wanaweza
kuungana na maadui zetu na kutupiga, Basi Wamisri wakakubaliana
kuwawekea Waisraeli wasimamizi ili wawatese. Kadri walivyowatesa ndivyo
Waisraeli walizidi kuongezeka. Waisraeli wakafanyishwa kazi kama watumwa
ambapo walifanya kazi za mashambani, walijenga mapiramidi ambamo
wafalme wa Misri walizikwa.
Alipoona Waisraeli wanazidi kuongezeka Mfalme alipitisha Amri kwamba
akizaliwa mtoto Muizraeli wa kiume auawe na kama wa kike asiuawe. Amri
hii walipewa wakunga.
Wakati Waisraeli wakiteseka mikononi mwa Wamisri Mungu akamuandaa
mkombozi wa kuwakomboa Waisraeli katika makucha ya Farao. Mkombozi huyo
si mwingine bali ni Musa aliyezaliwa katika Nchi ya Misri.Musa
alipozaliwa alifichwa kando ya mto ili
asiuawe na binti wa Farao wakati kienda kuoga alimuokota na akatatafuta
msichana wa kiyahudi kwa ajili ya kumlea. (Kutoka 1:1-22, 2:1-25).
Mungu alimwandaa Musa kwa ajili ya kuwakomboa Waisraeli utumwani Misri,
Musa aliandaliwa kukabiliana na Farao Mfalme wa Misri ili aweze
kuwaachia Waisraeli.
Musa alienda kuzungumza na Farao ili awaruhusu Waisraeli waweze
kuondoka Misri kuelekea kwenye Nchi ya ahadi ambayo Mungu aliwaahidi.
Farao alikuwa mgumu kuwaruhusu Waisraeli waondoke Misri hadi pale Musa
alipofanya miujiza mingi ili Farao aweze kuamini kwamba Musa ametumwa
na Mungu. Muujiza wa mwisho uliomfanya Farao aamini kwamba Musa ametumwa
na Mungu ni ule wa kuuawa kwa mzaliwa wa kwanza wa Misri ambapo
waliuawa wanyama hadi wanadamu. (Kutoka 12:29-31).
Baada ya kuruhusiwa na Farao kutoka Misri Musa akaanza kuwaongoza
Waisraeli kuelekea Nchi ya Kaanani ambayo aliwaahidi Waisraeli.
Waisraeli waliishi Misri miaka 430.
Waisraeli walisafiri miaka 40 Jangwani wakielekea Nchi ya Kaanani.
Mungu aliwaongoza Waisraeli kupitia Musa. Awali Waisraeli waliambiwa
watakapofika katika Nchi ya Kaanani na Miji yake waue watu wote
wasimuache hata mmoja, bali wabakize wanyama tu.
Musa hakuendelea kuliongoza Taifa la Israeli kwa kuwa alikuwa mzee na hivyo
hakufika katika Nchi ya ahadi. Alikufa akiwa miaka 120 na kuzikwa katika Nchi ya
Moabu na Yoshua mwana wa Nuni akashika usukani wa kuliongoza taifa la Israeli
kuelekea Nchi ya hadi.
Walipofika katika Nchi hiyo kwanza wakatuma wapelelezi waende kupeleleza Nchi
hiyo ambapo walifikia kwa mwanamke mmoja aliyeitwa Rahabu.Upelelezi ulipokamilika
kazi ya kuupiga mji huo ikaanza.
Waisraeli wakiongozwa na Yoshua wakiipiga miji ya Nchi hiyo kwa makali ya upanga.
Waliteka miji ya Hai, Yeriko na Yordani. Awali kabla ya mapambano Yoshua
aliwaambia Waisraeli kama watayasikiliza maneno ya Mungu basi Mungu atawatia
Wakaanani mikononi mwao (Yoshua 3:9-10).
Yoshua akaipiga Nchi yote na kuiteka sawasawa na neno la Mungu, baada
ya kuitwaa akawagawia Waisraeli urithi wao kama walivyoambiwa na Mungu
(Yoshua 12:6-23).
Lakini kitu kikubwa walichokosea Waisraeli ni kuwabakiza Wakaanani, yaani Wapalestina wa leo ambao wanasuguana nao leo.
Katika vita hiyo mji mgumu kuuteka ulikuwa Yerusalemu ambao leo ndio
unaopiganiwa sana na Wapalestina na Waisraeli kila mmoja akidai ni wa
kwake. Ukiondoa Misaafu ya dini, hata vitabu vya kihistoria
vinalizungumzia suala la vita hii jinsi ilivyokuwa ngumu katika
kuishinda Mji wa Yerusalemu kwani kwa uwezo wa Mungu Yoshua aliamuru
Jua lisimame na likasimama bila kuzama hadi Waisraeli waliposhinda.
Mfalme wa Yerusalemu aliyeitwa Adoni-Sedeki aliposikia Yoshua
ameishinda Miji mingine akaungana na Wafalme watano wa Wapalestina
kupambana na waisraeli ili wasije wakauteka Mji wa Yerusalemu. Kufuatia
kuungana huku vita ikawa kali sana kati ya Waisraeli na Wakaanani
(Wapalestina).
Wakati vita ikiendelea kupiganwa jua lilikuwa likikaribia kuzama na
desturi ya enzi zile ni kwamba vita inapopiganwa linapozama jua, basi
vita hutulia kwa kitambo hadi kesho yake hivyo Yoshua akachukua jukumu
la kumuomba Mungu asimamishe jua hadi wao washinde. Jua lilizama baada
ya Waisraeli kuushinda mji wa Yerusalemu. (Yoshua 11:1-23).
Katika miji mingine Waisraeli waliwauwa Wapalesttina wote isipokuwa
katika miji ya Gath , Ashdodi na Gaza ambako kuna makazi ya Wapalestina
hata hivi leo. (Yoshua 11;22). Licha ya kuwaacha Wapalestina lakini
Waisraeli walifanya mapatano na Wapalestina suala ambalo lilikatazwa na
Mungu.
Mungu aliwaambia Waisraeli kwa sababu wamefanya mapatano na Wapalestina
basi Wapalestina watakuwa miiba mbavuni mwao na hatawafukuza watoke
mbele zao (Waamuzi 2:1-3).
Lakini hata hivyo Misaafu ya dini inajichanganya yenyewe kwa mfano
katika Biblia Kitabu cha Waamuzi 3:1, kinasema “Basi hayo ndiyo Mataifa
ambao Bwana aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao yaani awajaribu hao
wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kaanani, ili kwamba vizazi vya
Israeli wapate kujua, ili kuwafundisha vita, hasa wao ambao hawakuvijua
vita kabla ya wakati ule, aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti
(Wapalestina) Wakaanani wote na Wasidoni na Wahivi waliokaa katika
kilima cha Lebanoni toka mlima wa Baal-Hermoni mpaka kuingia Hamathi.
Awali kabisa Waisraeli waliishi Kaanani (Palestina) na kisha walienda
Misri baada ya Kaanani kukumbwa na njaa. Baada ya kuibuka Farao mpya
Nchini Misri, asiyemtambua Yusufu Waisraeli walianza kuteswa na kisha
kurejea katika Nchi waliyodai ya kwao yaani Nchi ya Kaanani ambayo ndiyo
Izraeli ya leo.
Mgogoro wa Wapalestina na Waisraeli unakuwa mgumu kwa sababu Waisraeli
wanaamini Palestina ni Nchi yao waliyoahidiwa na Mungu na Wapalestina
kwa upande wao wanaona wamevamiwa katika Nchi yao kama Biblia inavyosema
kwamba Wapalestina watakuwa miiba kwa Waisraeli na ndivyo ilivyo hivi
sasa.
Kitabu
cha GLOBAL INSIGHTS, People and Cultures kilichoandikwa na Waandishi
wanane baadhi yao wakiwa Maprofesa waliobobea katika masuala ya
historia, kinasema kuwa Wayahudi wanaami kuwa wao ni Taifa teule na
kwamba Masiha atatoka katika Taifa lao na kwamba katika Taifa hilo
wakati Yesu akizaliwa lilikuwa likitawaliwa na Warumi(ukurasa wa 33 na
34).
Katika
ukurasa wake wa 48 kitabu hicho kinaeleza kuwa Waaraabu waligawanyika
katika Makundi ya Wakaanani,Wafilisti na Wamisri na wote wakaja kuwa
Waarabu kwa kijifunza kiarabu.Kumbuka msomaji kwamba Wakanani ndio
Wapalestina wa leo.Pia kitabu hicho kinaelea kuwa asilimia 90 ya Waarabu
ni Waislamu.
Wapalestina wanaishi kama wakimbizi katika Nchi ya Israeli kwa mujibu
wa kitabu cha Global Insights, people and cultures ni kwamba zaidi ya
Wapalestina Milioni mbili wanaishi nje ya Israeli katika makambi yao
huko Yordani na wengine wanaishi katika ukanda wa Gaza chini ya
Waisraeli na wengine milioni moja wanaishi Israeli.
Kwa mujibu wa kitabu hicho ni kwambaWapalestina watajisikia furaha na
matumaini ikiwa watarejeshewa Nchi yao toka kwa Waisraeli na kutambuliwa
kama Taifa huru la Kipalestina. Wapalestina wamekata tamaa kufuatia
kunyanyaswa na Waisraeli na sasa wanaamua kuwafundisha watoto wao
kushika bunduki na kujilipua wenyewe ili mradi wameua Waisraeli kadhaa.
Kitabu
hicho cha Global Insight, people and Cultures kinawaonyesha watoto wa
kipalestina wenye umri kati ya miaka 5 hadi 7, wakiwa wamevalia nguo za
kijeshi, wakifundishwa kupambana na maadui zao Waisraeli.
Kwa mujibu wa kitabu hicho ni kwamba licha ya matatizo wanayokumbana
nayo Wapalestina. Wanaamini wao ni Wapalestina. Wanafunzi wa kipalestina
wanafundishwa kuamini suala hilo . Wanafunzi wanafundishwa kuamini
kwamba wao sio Wamisri au Waarabu wa sehemu nyingine bali wao ni
Wapalestina.
Kwa mujibu wa kitabu hicho ni kwamba mgogoro baina ya Wapalestina na
Waisraeli ulianza mara baada ya kuundwa Taifa la Israeli, Mei 14, 1948.
Kitabu hicho kinasema Waarabu hawakupendezewa na kuundwa kwa Taifa hilo
hivyo wakaamua kukungana ili kuliangamiza Taifa hilo ambapo Waarabu
walishindwa vibaya katika mapambano hayo.
Kitabu hicho kinasema zaidi ya wapalestina Milioni 2 wanaishi nje ya
Israeli, wengi wao wanaishi kwenye makambi ambayo yako katika hali ya
kimaskini. Kitabu hicho kinasema makambi hayo yana vibanda ambavyo
Wapalestina wanaishi watu tisa tisa katika vibanda hivyo. Wapalestina
wengine Milioni 1 wanaishi katika ukanda wa Gaza chini ya utawala wa
Waisraeli na nusu milioni wanaishi Israeli.
Kitabu hicho kinabainisha kwamba kuna waisraeli Milioni tatu na nusu
katika Nchi ya Israeli ambao wengine walitokea Uingereza, Mashariki ya
Kati, Afrika Kaskazini, Asia na Amerika Kusini na Kaskazini na
wanaunganishwa na dini ya Uyuda.Wanaamini kwamba Israeli ni Nchi yao
ambayo Mungu aliahidi kuwapa. Lugha wanayotumia ni kiebrania(Global
Insights, People and Cultures page 50-53)
Waisraeli na Wapalestina wanashindwa kuelewana kwa sababu ni watani wa
jadi ambapo wamekuwa wakipambana mara kwa mara katika Historia yao yote
ambapo kama ukisoma Biblia katika kitabu cha samweli 17:1-58, utaona
mapambano baina ya Daudi Muisraeli na Goliathi shujaa wa vita wa
wapalestina. Inakuwa vigumu Wapalestina kujikwamua kwenye makucha ya
waisraeli kwa sababu Mungu alisema Nchi hiyo amewapa Waisraeli
kama alivyowaahidi na Waisraeli kwa upande wao wanavuna walichokipanda
kwani Mungu aliwaagiza kuwaangamiza wapalestina wao wakawaacha.
Baadhi ya Wachambuzi wa masuala ya kidini wanasema kuwa Biblia inasema
Nchi ya Israeli ni Nchi halali ya Waisraeli kwa kuwa waliishi mwanzo na
kisha kwenda Misri baada ya njaa kuingia katika hiyo na wakarejea tena
kama Mungu alivyowaahidi na kwamba mgogoro huo hautakwisha hadi Yesu
atapokuja mara ya pili.
Hivyo basi katika kutatua mgogoro wa Wapalestina na Wayahudi hekima na
busara zaidi inatakiwa ikibidi kurejea kwenye vitabu vya dini vya Korani
na Biblia na kisha kuchanganya na Siasa. Hata hivyo viongozi wa
kimataifa wanaposuluhisha mgogoro huo wajaribu kutafakari kifungu kwamba
Mungu aliwabakiza Wapalestina ili kuwafundisha Vita Waisraeli
vinginevyo watakuwa wanaponda maji kwenye ikunu kaika kutatua nmgogoro
huo wa Mashariki ya kati
Kwa
mtizamo wangu katika mgogoro huu unaoendelea busara zaidi zinapaswa
zitumike katika wakati huu ambapo baadhi ya Wasomi wamekuwa wakiibuka na
kuitaka Israeli iache kuikalia Palestina na kwamba iwaachie Wapalestina
Nchi yao .
Wasipotumia akili wanaweza wakawa wanatumia pesa nyingi kutatua mgogoro
ambao hauishi na ambao ulitabiriwa kwamba Wapalestina waliwekwa kwa
ajili ya kuwafundisha vita Wayahudi na kwamba vita hivyo vitamalizwa na
Mungu mwenyewe.
MWISHO.
Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa,kijamii na kimataifa
Anapatikana kwa simu namba – 0755/0655 761195Barua pepe – josephmwambije@yahoo.co.uk
AHSANTE mwandishi kwa maelezo mazuri.
ReplyDeleteHaipingiki nchi ya Kanaani ni mali ya Israel kwa sababu kihistoria;
1.Waliahidiwa na kupewa waikalie milele
2.Kwa sababu zisizoepukika
(mf. njaa,kutekwa n.k) Waisrael waliondoka kwao kwenda ugenini
=>Muda huu ndipo waarabu wakajiimarisha hapo
SASA WENYE NCHI WAMERUDI
Nao ni waIsrael
3.