Na Joseph Mwambije
RUVUMA
WALIMU katika Shule mbalimbali Mkoani Ruvuma wameendelea  na mgomo wao  usiokuwa na kikomo  kuishinikiza Serikali kushughulikia madai yao huku Kaimu Mkuu wa Mkoa huo  Joseph Mkilikiti akitishia kuwafukuza kazi walimu waliogoma ambapo katika Shule nyingine walimu hawakufika kabisa Shuleni hali iliyofanya wanafunzi kurejea nyumbani.

Mwandishi wa habari hizi alitembelea Shule mbalimbali za Manispaa ya Songea na kushuhudia walimu wakiwa  kwenye mgomo huku baadhi ya Shule walimu wakifika kuripoti na kurejea nyumbani.Huku katika Shule nyingine walimu walionekana wakiota moto na kusema hawafundishi wanaota moto.

Baadhi ya Shule ambazo walimu  wake wamegoma  ni  Shule za Msingi Sabasaba,Mwembechai,Makambi,Mahilo,Majimaji,Sokoine,Bombambili,Sabasaba,Matarawe,Makambi na baadhi ya Shule za Sekondari huku katika Shule mbili  za Manispaa ya Songea walimu wakiendelea na kazi hali iliyofanya Viongozi wa Chama cha walimu kuwazuia kufanya kazi.

Katika Shule ya Msingi Matarawe Mwandishi alishuhudia ikiwa na walimu watatu akiwemo Mwalimu Mkuu ambapo walisema wao wamebaki kutokana na mradi wa Shule wa kuuza uji kwa wanafunzi vinginevyo  wangekuwa wamerejea nyumbani.

Katika Shule ya Msingi Matarawe yenye walimu 16 ni walimu watatu pekee ndio walikuwepo Shuleni  hapo akiwemo Mawalimu Mkuu wa Shule hiyo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini ambaye alisema Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Mkilikiti amekuwa akizunguka kuwatishia kuwafukuza kazi walimu waliogoma.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu  huyo wa Mkoa amewaagiza Watendaji wa Kata kuorodhesha majina ya walimu waligoma ambapo Mwandishi wa habari hizi alishudia baadhi ya Watendaji wa Kata wakiorodhesha majina ya walimu waliofika kuripoti Shuleni na kuendelea na mgomo na waliogoma kabisa hata kuja Shuleni.

Gazeti hli lilipotembelea kwenye Ofisi za Chama cha walimu Mkoa wa Ruvuma lilishuhudia viongozi wa Matawi ya vyama vya walimu toka kwenye Shule 72 za Manispaa ya Songea wakiwa kwenye majadiliano ya kupeana misimamo zaidi ya kuendelea na mgomo huo usiokuwa na kikomo hadi Serikali itakaposhughulikia madai ya walimu.

Baadhi ya Viongozi wa Chama cha walimu  Mkoani humo ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini wakizungumzia hatua ya Kaimu Mkuu wa Mkoa ya kuwatisha walimu waliogoma walisema hakupaswa kufanya hivyo kwa kuwa mgomo huo uko kihalali.

Hata hivyo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusiana na mgomo huo alisema  wana vikao viwili kujadili suala la hilo na  bado wanalifuatilia na atakapomaliza vikao hivyo atakuwa na maelezo kamili.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwatisha kuwafukuza kazi walimu waliogoma alikana kufanya hivyo na kusema yeye alitembelea kujionea hali halisi ya mgomo ambapo  alimwambia Mwandishi wa habari hizi awasiliane na Meya wa Manispaa ya Songea, Charles Mhagama.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Songea alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema hali ni mbaya kuhusiana na mgomo huo ambsapo anasema walipotembelea yeye na Mkuu wa Wilaya walishuhudia kukiwa na walimu wachache huku katika Shule nyingine kukiwa hakuna walimu kabisa.

'Wengine walikuja kuripoti na kurudi nyumbani huku wengine wamegoma kabisa hata kuja Shuleni   ni kweli tumeagiza Watendaji wa Kata waorodheshe idadi ya walimu wealiogoma ili tujionee hali halisi na  Serikali ijue hatua za kuchukua'alisema.

Alipoulizwa malalamiko ya walimu waliogoma kutishwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa kuwatisha walimu kuwafukuza kazi alisema hakuwatisha bali aliwaambia kuwa watafukuzwa kazi na kusisitiza kwamba walimu watakaogoma watachukuilwa hatua na Serikali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

Aliwatoa wito kwa walimu kuachana na mgomo na kuendelea na kazi na kuwataka kuachana na maneno ya watu wanaowashawishi kugoma kwa kuwa wakifanya hivyo hatua dhidi yao zitachukuliwa.

Madai ya msingi ya Walimu ni nyongeza ya mshahara na posho ya kufundisha katika mazingira magumu

MWISHO