NA JOSEPH MWAMBIJE
KATIKA
miaka ya hivi karibuni watu wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na
tabia za watu mbalimbali ambao wamekuwa wakitabiri kuhusiana na mwisho
wa dunia na kwamba Sayansi ya Dunia iko ukingoni.
Tabiri
hizi zimekuwa zikiweka watu njia panda ambapo wengine wamekuwa
wakitafakari ikiwa Yesu au Issa bin Mariam atakuja watajibu nini ilhali
hawana maandalizi yoyote lakini wengine wenye mioyo dhaifu wanadiriki
kuacha shughuli zao na kumsubiri Yesu huku wengine wakienda milimani
kusubiri ujio wake.
Mwaka
jana tulishuhudia vituko zaidi vya vikundi vya watu waliowaachisha
watoto wao shule na kwenda milimani kusubiri ujio wa Bwana Yesu na
wengine wakitaka kwenda Ulaya kuhubiri injili bila kuwa na paspoti na
tiketi za Ndege kwa madai kuwa mwisho wa dunia umefika.
Lakini
taarifa za hivi karibuni ambazo zimedai kuwa ifikapo Disemba 21 mwaka
2012 ni mwisho wa dunia zimezua hofu zaidi kwa wakazi wa dunia, hofu
inatanda zaidi kutokana na kauli za Wanasayansi wanaodai kuwa Sayari ya
dunia hii imebakiza miezi michache kufikia ukomo wake.
Kauli
za Wanasayansi hao zinasimamia kwenye vipimo vya tabiri za mnajimu wa
Kifaransa, Michael de Nastredame aliyeishi karne ya 16 (1503 – 1566), tabiri
za mnajimu huyo maarufu kupitia kitabu chake cha Les Prophetics
(Ubashiri) zinadai kuwa mwaka 2012 kutakuwa na vita ya tatu ya dunia
itakayosababisha maangamizi makubwa ya dunia.
Kutokana
na utabiri huo Wanasayansi walio katika mlengo wa kat ya Sayansi na
Unajimu wanayajengea hoja maandishi ya Nostradumus kuwa uwepo wa Nishati
za Nyuklia katika Nchi mbalimbali ndiyo zao la dunia wakati wa Vita Kuu
ya tatu. Kwa wale wanaofuatilia makala zangu kuna wakati niliwahi
kuandika Makala yenye kichwa, Mzozo wa Israel na Irani na hofu ya kuzuka
Vita ya tatu ya dunia.
Baadhi
ya Nchi zinazomiliki Nishati ya Nyuklia ni Marekani, baadhi ya Nchi
zilizokuwa zinaunda Umoja wa Soviet , China , Ufaransa , India ,
Pakistan , Iran na Korea Kaskazini. Athari za
mabomu ya Nyuklia zipo Hiroshima Nchini Japan ambapo athari zake zipo
hadi leo kutokana na bomu hilo la Atomic lililotupwa wakati wa Vita ya
Pili ya dunia mwaka 1939 hadi
mwaka 1945.
Kutokana
na makali ya Bomu hilo ambalo liliua watu 80,000 na wengine wengi
kujeruhiwa Japan ilisalimu amri na vita hiyo ikakomeshwa, katika Mji wa
Hiroshima ambako lilitupwa bomu hilo hadi leo bado watu wanazaliwa
vilema huku kukiwa na simanzi isiyofutika. Nchi za Israel , Afrika
Kusini , Argentina na Brazil zinatajwa kuwa na uwezo wa kumiliki na
kutumia Nyuklia lakini bado hazina mpango wa kumiliki na kurutubisha
silaha hizo za maangamizi.
Wanasayansi
wanaeleza kuwa kizaazaa cha dunia kuangamia ni tufani zito ambalo
litaigonga na kusababisha kupoteza mawasiliano kati yake na jua hivyo
ile sumaku ya asili kushindwa kufanya kazi yake, katika maelezo yao
wanasayansi wanafafanua kuwa kuna Sayansi inayoitwa Nibiru Planet x
ambayo itapoteza mwelekeo Disemba 21 2012na kuigonga dunia na
kusababisha itoweke.
“Hii
ina maana kuwa baada ya Disemba 21, 2012 hakutakuwa na Sayansi
inayoitwa dunia kwani itagongwa na Planet x na kuipoteza, itaiachanisha
na jua kisha itadondoka” ilisema sehemu ya ripoti ya Wanasayansi hao.
Hata hivyo kwa upande wa pili Wanasayansi wa Taasisi ya NASA ya Nchini Marekani wanautaka Ulimwengu kutambua kwamba 2012 si mwisho wa dunia huku wakiwataka wakazi wa
dunia kutokuwa na wasiwasi kuhusiana na habari za mwisho wa dunia. NASA
wanadai kuwa katika matoleo yote yanayoelezea kuwa dunia mwisho wake ni
2012, hakuna hata moja ambalo wamejiridhisha kitaalamu badala yake
wameelezea hali hiyo kwamba inakuja kwa lengo la kutisha watu.
Habari
za mwisho wa dunia hazijaanza leo ambapo iliwahi kuelezwa kuwa mwaka
1844 ni mwisho wa dunia, pia ikaelezwa kuwa mwaka 2000 ni mwisho wa
dunia lakini pia ikavumishwa kuwa mwaka 2003 ndio ingekuwa ukomo wa
dunia. Pia kumekuwa na watu wengi ambao wamekuwa wakiibuka na
kujitangaza kuwa wao ni Yesu.
Lakini
hebu twende kwenye hoja za msingi katika biblia na vitabu vingine vya
dini tuone ukweli uko wapi, madai hayo ya mwisho wa dunia yana ukweli
gani? Je Biblia inawaitaje wanazusha kuhusu mwisho wa dunia na kwamba
matukio yanayotendeka sasa yanaashiria nini?
Hofu
imetanda huku baadhi ya maeneo wakishindwa hata kufanya kazi
wakijiandaa na mwisho wa dunia, kwingineko duniani wameuza walivyonavyo
na kusaidia maskini kisha kubaki watupu wakisubiri ujio wa Yesu kwa hofu
kuu wakiwa na hoja kwamba mali wanazomiliki hazina maana wakati dunia
imefika mwisho, lakini pia ndani ya biblia tutaona kama hayo ni maagizo
ya Yesu.
Watu
waishi kwa hofu wakihofia mwisho wa dunia, pia tutaona kama kuna
tarehe, mwezi na mwaka vilivyotajwa kuwa ni mwisho wa dunia na Ujio wa
Yesu? Naam kwa wale wasiyoyafahamu Maandiko Matakatifu.wanakuwa na hofu
kubwa hadi kufikia kiwango cha kupatwa shinikizo la damu au ugonjwa wa
moyo wakihofia mwisho wa dunia.
Katika hofu zao ndipo na matapeli wanawajia wakidai wakidai wao ni akina Yesu na Manabii waliotumwa na Mungu kuja
kuwapa maonyo na kuwataka kukabidhi mali zao kwa akina Yesu hao na
Manabii hao wa Uongo. Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia akina
Yesu wengi wa uongo na Manabii wa uongo.
Dunia
bado haijasahau yale yaliyotendwa na Nabii wa uongo Bw. Kibwetere na
kule Uganda aliyewaamuru wafuasi wake wamkabidhi mali zake na kusubiri
mwisho wa dunia wakiwa kanisani, mwisho uliowajia kwa Nabii huyo wa
uongo kuwachoma moto wakiwa kanisani na familia zao.
Mikanganyiko
hii itazidi kuwaathiri wengi wasioyafahamu maandiko kadri tunavyosonga
mbele huku akina Yesu wa bandia wakizidi kuibuka na kutoa mafundisho
kinyume na Yesu wa ukweli ambaye kwa mujibu wa Biblia yuko mbinguni
akiwaombea watu wake pengine hili suala la mwisho wa dunia au kiama ni
suala tete ambalo halina budi kujadiliwa kwa kuwa linatugusa katika
maisha yetu ya kila siku.
Nasema
linatugusa kwa kuwa kila binadamu kuna kitu anachoabudu na katika hilo
wapo wapagani ambao hawana dini, wapo wanaoabudu dini za jadi na wapo
wanaoabudu dini mbalimbali lakini katika yote Biblia inasema kitu
chochote ambacho mwanadamu anakiweka mbele kuliko Mungu basi huyo ndiye
Mungu wake hivyo basi kwa mantiki hiyo hakuna ambaye hana Mungu.
Ili kupata ukweli wa tarehe, mwezi, mwaka na siku sahihi ya kuja Bwana
Yesu na mwisho wa dunia hebu tuiulize Biblia inayoaminiwa na wakristo
wengi na wasio wakristo duniani. Biblia inasema katika kitabu cha
Mathayo 24:3 – 6, Hata alipokuwa meketi katika mlima wa Mizeituni
Wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha wakisema tuambie mambo hayo
yatakuwa lini, nayo ni nini dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia?
Yesu akajibu akawaambia, angalieni mtu asiwadanganye kwa sababu wengi
watakuja kwa jina langu wakisema mimi ni Kristo, nao watawadanganya
wengi, nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya Vita, angalieni
msitishwe, maana hayo hayana budi kutokea, lakini ule mwisho bado.
Hapa
tunaona kwamba habari za mwisho wa dunia hazijaanzia kwetu, kumbe
zilianza toka kwa wanafunzi wa Yesu ambao walitaka kujua ukweli wa Mambo
hayo, wanahoji mambo hayo yatakuwa lini na dalili za kuja kwa Yesu na
mwisho wa dunia? Lakini Yesu anajibu kwamba
waangalie mtu asiwadanganye kwa sababu wengi watakuja wakidai wao ni
akina Kristo na kwamba watawadanganya wengi na pia anawaambia
watayasikia matetesi ya Vita wasitishwe kwani ule mwisho bado.
Pia
Yesu anatahadharisha kuwa tusitishwe kwa kuwa tutasikia Matetesi ya
vita lakini mwisho wa dunia bado. Hapa Yesu anagusia dalili za kuja
kwake na mwisho wa dunia kuwa ni pamoja na matetesi ya Vita na
kuthibitisha kuwa kuna mwisho wa dunia lakini hauji kiuzushi kama watu
wanavyozusha hivyo bado anawaasa watu kutokuwa na hofu na ujio wake.
Ukiendelea
katika mstari wa 7 katika kutaja dalili za ujio wake na mwisho wa dunia
anasema Taifa litaondoka kupigana na Taifa, Ufalme kupigana na Ufalme,
kutakuwa na njaa na kutakuwa na matetemeko ya Nchi na mahali mahali.
Dalili hizi zinazoelezwa na Biblia zimetokea sana na kukaririwa katika
bongo za watu wengi ambapo hadi hivi leo dunia imeshuhudia vita nyingi
sana na ni nchi chache sana duniani ambazo hazijawahi kupigana Vita.
Matetemeko
ya ardhi ndio usiseme na hivi karibuni lilitokea tetemeko la ardhi
Nchini Haiti na kuua watu wengi, upande wa njaa Nchi nyingi duniani
zinakumbwa na njaa na watu wanakufa kwa njaa. Katika mstari wa 11 Yesu
anasema Manabii wengi wa uongo watatokea ns kuwadanganya wengi. Kuhusu
Manabii wa uongo nimekwisha kueleza na nikagusia kuhusu akina Kibwetere.
Pia
katika sura hiyo ya Mathayo 24 anasema kwa sababu ya kuongezeka Maasi
upendo wa wengi utapoa ambapo katika hili tumeshuhudia ndugu wakiuana
kwa sababu ya mali huku wengine wakiwatoa watoto wao kafara kwa kuuwaua
kikatili kwa sababu ya mali .
Ukifuatilia
vyombo vya habari ndugu msomaji kuna mambo mengi ya kutisha
yanayofanywa na wanadamu ambayo hata Shetani mwenyewe yanamshangaza.
Nimewahi kusoma simulizi ya jamaa mmoja aliyeuwa watoto wake wawili,
mama yake na kisha kuzini na maiti ya Msichana mrembo aliyemuua ili
apate utajiri. Ni simulizi ya kutisha ambayo Jamaa huyo alizini na maiti
inayotoa harufu huku sauti ya Jini ikimwambia atakuwa milionea kwa
kutimiza masharti ya kishirikina.
Anasema
wakati huo mtu akiwaambia tazama, kristo yupo hapa, au yuko kule
msisadiki kwa maana watatokea Makristo wa wa uongo na Manabii wa uongo
nao watatoa ishara kubwa na maajabu wapate kuwapoteza yumkini hata walio
wateule. Labda nihoji, hadi naandika Makala hii kuna Yesu wangapi wa
uongo waliokwishaibuka? Bila shaka ni wengi.
Biblia
inaendelea kusema “Tazama nimekwisha kuwaonya mbele, basi wakiwaambia,
yuko jangwani msitoke, yumo nyumbani msisadiki, kwa maana kama vile
umeme utokavyo Mashariki ukaonekana hata Mangharibi hivyo ndivyo kutakavyokuja kwake Mwana wa Adamu.
Hiyo
ni hoja ya msingi sana kwamba Yesu atapokuja ataonekana na watu wote
kama vile Umeme kwani huko mbele tutashuhudia maajabu makubwa zaidi ya
haya tunayoyaona ambapo shetani ataigiza kuja kwa Yesu na kutoa maagizo
yaliyo kinyume na Mungu huku akihalalisha na kubariki uovu.
Yesu atapokuja ataonekana na watu wote lakini Yesu huyu wa bandia ataonekana baadhi ya maeneo. Mathayo 24:36 inasema “Walakini kwa habari ya siku ile na saa ile hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana (Yesu) ila
baba(Mungu) peke yake. Sasa nihoji hao wanaotabiri kwa kutaja tarehe,
mwezi, siku na mwaka wa kuja yesu uhakika huo wanautoa wapi wakati
Biblia inasema hata Yesu mwenyewe hajui.
Lakini
hoja ya msingi Biblia inasema wanadamu wanapaswa kujiandaa na ujio wa
Yesu kwa kuwa hawajui atakuja lini ambapo Mathayo 24: 42 anasema
“kesheni basi kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana (Yesu)
wenu. Ifahamike kuwa kukesha kunakoelezwa hapa si kukesha kwa kukaa
macho la hasha bali kuwa tayari kwa kutenda mema muda wote. (Biblia
katika sura ya 24 ya Mathayo)
Kauli
hii ya Yesu inashabiina na usemi maarufu sana usemao ishi katika maisha
ya dunia kana kwamba utaishi miaka 100 ijayo na kidini ishi kama
utakufa leo, kauli hiyo inamaanisha kwa maisha ya kidunia fanya mambo ya
maendeleo kwa matarajio ya kuendelea kuwepo duniani muda mrefu na kwa
maisha ya dunia ujiandae kana kwamba utakufa leo.
Kikubwa
tunachopaswa kutambua ni kwamba dalili nyingi za kuja kwa Yesu na
mwisho wa dunia zimetimia na zinaendelea kutimia na kwamba yuko jirani
kuja na si kwamba ule mwisho umefika bali “U karibu kufika, lakini pia
hawapaswi kuishi kwa hofu kwani Yesu ni mtu wa upendo.
Ifahamike
kuwa dunia haitaangamizwa kwa Vita kama wanasayansi wanavyodai na pia
mwisho wa dunia hautakuja kwa dunia kugongana na Sayari nyingine bali
itaangamizwa kwa moto kwa maana watenda mabaya wataangamizwa kwa moto (
Ufunuo 20: 12 – 15) Ikumbukwe pia dunia ya kwanza wakati wa Nuhu
iliangamizwa kwa maji na baada ya dunia kuangamizwa kutakuwa na Mbingu
mpya na Nchi mpya na Mji mtakatifu Yerusalemu piya utaoshuka kutoka
Mbinguni (Ufunuo 21: 1 – 2)
MWISHO.
Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa simu-0755/0655 761195
Barua pepe-josephmwambije@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment