Sunday, July 8, 2012

VETA SONGEA YAJIZATITI KUTOA ELIMU YENYE UBORA

  • scan0002.jpg
  • scan0003.jpg
  • scan0005.jpg
  • scan0006.jpg




MAELEZO YA PICHA

Na.2
Wa pili kushoto ni ni Mkuu wa Chuo cha VETA Songea Bw. Gideon Ole Lairumbe na wa tatu(kushoto) ni Mkuu wa Wilaya Namtumbo Bw. Saveli Maketa kwenye moja ya mahafli ya Chuo hicho.Wengine ni viongozi wa Veta.

Na 3
Mkuu wa Chuo hicho Bw. Lairumbe

Picha Na 5
Wanachuo wakipita kwenye viunga vya Chuo hicho.
Na.6
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Bw.Maketa wa (kwanza kushoto) akikagua majengo ya Chuo hicho kwenye moja ya mahafali ya Chuo hicho.

Picha zote na Joseph Mwambije,Songea

ILI  KUKABILIANA NA USHINDANI WA SOKO AFRIKA MASHARIKI VETA SONGEA YAJIZATITI KUTOA  MAFUNZO YENYE UBORA


Na Joseph Mwambije, Songea.

Katika kpindi hiki cha kuelekea ushindani wa  wa Soko la Afrika mshariki kielimu na ajira Vyuo vya Ufundi stadi vina dhamana kubwa katika kuhakikisha vijana  wa Kitanzania wanapata elimu ya ufundi uliobobea ili waweze kujitegemea.

Lakini pia Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa ufundi  stadi  kwa vijana unatumika ipasavyo tofauti na ilivyo sasa ambapo fenicha nyingi maofisini zinatumika za kutoka nje ya Nchi hasa  za China ambazo ubora wake ni mdogo ukilinganisha zinazotengenezwa na Mafundi wa hapa Nchini.

Ni jambo lisilopingika kwamba Fenicha zinazotumika kwenye Ofisi za Serikali ni zile za kutoka Nchini China ambazo zinadumu kwa mwaka mmoja na zingine hata mwaka hazimalizi hivyo inakuwa mzigo kwa Serikali kununua fenicha mpya kila mwaka na kuwanyima ajira vijana wa Kitanzania waliojiajiri kwa ufundi ambao wanatengeneza bidhaa zenye ubora kuliko zile za Wachina.


Miongoni mwa Vyuo vilivyojizatiti kutoa elimu bora ni Chuo   cha ufundi Stadi(VETA) Songea  ambacho  kipo kilometa tatu toka katikati ya mji wa Songea eneo la Msamala  barabara ya Songea Njombe.

   Imedhihirika hapa Mjini Songea Mafundi waliosomea kwenye Chuo hiki wakitengeneza bidhaa bora za uhakika lakini wameshindwa kuendelezwa na kutumika kupitia bidhaa zao.


 Chuo hicho kilianzishwa mwaka 1984 wakati huo kikiwa chini ya idara ya mafunzo na majaribio ya Ufundi (NVTD) chini ya wizara ya kazi na maendeleo ya vijana  ambapo  kilianzishwa kikiwa na fani tatu za ufundi ambazo ni ufundi wa magari,ufundi uashi na ufundi wa bomba.
   
Kwa mujibu wa mkuu wa chuo hicho Bw. Gideon Ole Lairumbe anasema madhumuni ya mafunzo wanayotoa ni kutoa wahitimu wenye ubora wa hali ya juu wa ufundi ambao utawawezesha kuajiriwa au kujiajiri wenyewe katika fani  mbalimbali ikiwemo kozi ndefu (CBET)Ushonaji nguo,ambao mwanafunzi katika kozi hii hujifunza jinsi ya kushona nguo mbalimbali kama vile suruali,mashati,magauni,suti,mapazia,nguo za arusi na nyinginezo.
 
 Upande wa kozi ya umeme anasema wanajifunza jinsi ya kutandaza nyaya za umeme kwenye majumba ,kurekebisha vyombo vinavyotumia umeme kama pasi,birika na majiko,pia  kozi ya useremala ambayo wanafunzi wanajifunza kutengeneza kazi za samani za ndani na nje na upauaji wa nyumba ambapo anasema kuwa sehemu kubwa ya wanafunzi ambao wanamaliza fani hiyo hujiajiri wenyewe ambapo ajira hupatikana katika taasisi mbalimbali.
     Anazitaja kozi nyingine kuwa ni  ya uungaji vyuma ambayo mwanafunzi hujifunza jinsi ya kuunga vyuma vizito na vyepesi kwa kutumia gesi,umeme na kutengeneza vitu kama majiko ,milango ya chuma ,grill za milango au madirisha na mabodi ya gari.
   
Kozi nyingine ni ufundi uashi ambayo hujifunza jinsi ya kujenga kwa kutumia matofali imara ,pia wanajifunza jinsi ya kusoma ramani za majengo ,kutengeneza tofali ,kupima majengo,sakafu za aina mbalimbali na ukadiriaji wa gharama za ujenzi.

‘Pamoja na kozi ndefu pia Chuo kinaendesha kozi za muda mfupi ambazo ni za udereva wa pikipiki na wa magari madogo na makubwa,Saloon,utengenezaji wa kompyuta,Uhazili na ufundi wa umeme jua ambapo zinaendeshwa kwa wiki mbili hadi miezi mitatu’alisema

Alifafanua kuwa kozi hi huenda sambamba na uanzishaji wa kozi ya udereva wa pikipiki na magari madogo katika wilaya za Mkoa wa Ruvuma na vijijini na kwamba tayari wameanzisha kozi hizo Tunduru na Mbinga na pia Wilayani Njombe  ambako mafunzo yalifanyika.

Upande wa vijiji ambako wameendesha mafunzo kwa kushirikiana na Serikali ya Kata ni ni katika kijiji cha Bonde la Hagati, na Mikaranga wilayani Mbinga,Peramiho,Kambarage,Magagula na Kizuka  katika Wilaya ya Songea vijijini na kwamba wana mpasngo wa kuendesha mafunzo katika  vijiji vya Namtumbo na Mkoa mpya wa Njombe


     
Bw.  Lairumbe anafafanua zaidi kuwa kozi nyingine ambazo zinatolewa chuoni hapo kuwa ni kozi ya ufundi magari ,umeme wa magari na uhazili (Computer and Secretarial Service) pamoja na masomo ya ziada.

Mkuu huyo wa Chuo anasema Chuo hicho kimepitia mabadiliko makubwa baada ya kujenga majengo mapya na kuachana na  ya zamani na kwamba hivi sasa kina hadhi kubwa kikiwa kimepania kuinua na kubadilisha maisha ya Wananchi wa Songea na Tanzania kwa ujumla.

Anasema kuwa mafunzo yanayotolewa Chuoni hapo yanalenga kumfanya  mtu aweze kuajiriwa au kujiajiri mwenye pasipo kuhangaika na kutoa huduma  kwa jamii huku akijipatia kipato na kuondokana na umaskini na kwamba mafunzo hayo yanachukua miaka miwili katika hatua ya kwanza na mwaka mmoja katika hatua ya pili.


 ‘Chuo hiki kina uwezo wa kupokea wanafunzi 470 kwa mwaka na sasa kwa kushirikiana na Chuo cha walimu wa Veta Morogoro tunaendesha mafunzo ya ualimu wa ufundi ngazi ya cheti’alisema Mkuu huyo wa Chuo .

Anabainisha kuwa katika mwaka wa masomo wa 2011 walimu 30 walihitimu masomo hayo kwa ngazi ya cheti cha ualimu wa ufundi stadi na kupata sifa za kufundisha kwenye vyuo vya ufundi.     

Akielezea mafanikio ambayo wameyapata tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mkoani hapa  Mkuu huyo wa Chuo anasema chuo kimeweza kutoa huduma za kijamii ikiwa ni sehemu ya mafunzo,lakini pia wanafunzi kujitangaza jinsi wanavyoweza kutoa huduma ya viwango gani kwa mfano utengenezaji wa samani za chuo cha ualimu Matogoro,madawati ya halmashauri za wilaya ya Songea,Manispaa ya Songa na Namtumbo,ujenzi wa ofisi ya usalama wa Taifa Mkoa pamoja na uzio wake ambapo anasema kuwa hizo ni baadhi ya huduma zao zikiwemo za mafunzo ya ujasiriamali kwa wastaafu wa JWTZ na wadau mbalimbali ,Kompyuta na udereva.

Katika hatua nyingine Chuo hicho kimechangia kupunguza ajali za barabarani kama kundesha mafunzo ya udereva wa magari na pikipiki kwa  kuendesha kozi fupi kuanzia mwaka jana  baada ya  Serikali kutangaza kubadli leseni za madereva na kuzifanya ziwe za kisasa zaidi na lengo likiwa kuwafikia madereva 3000 ambapo kwa mwaka jana hadi sasa zaidi ya madereva 500 walipatiwa mafunzo hayo wa Mkoa wa Ruvuma .

Kutokana na hilo kwa nyakati tofauti Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Said Mwambungu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Michael Kamuhanda wamempongeza Mkuu wa Chuo hicho kwa kupunguza wimbi la ajali kwa kuendesha mafunzo hayo ambapo viongozi hao kwa nyakati tofauti walieleza kuwa kutokana na mafunzo hayo ajali zimepungua na kuwaasa wamiliki wa magari kutoa kipaumbele kwa kuwaajiri madereva waliosomea VETA.


Vilevile anasema pamoja na kuendesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi Chuo hicho kinatoa huduma za kijamii kwa lengo la kjenga mahusiano mazuri na wananchi wanaokizunguka Chuo hicho na kwamba huduma hizo ni sehemu ya mafunzo kwa vijana.

     
Hata hivyo anasema penye mafanikio hapakosi changamoto ambapo mkuu huyo wa chuo anazitaja  changamoto ambazo zinawakabili kuwa ni mwamko mdogo miongoni mwa jamii ya Mkoa wa Ruvuma katika mafunzo ya ufundi stadi,mtazamo hasi wa jamii  kwamba vijana wanaokwenda kusoma VETA ni wale walioshindwa kuendelea na elimu ya juu ukosefu wa mabweni kwa wanafunzi wa wilaya za mbali kama vile Mbinga,Tunduru na Namtumbo .

Asema kuwa  sambamba na ukosefu wa pesa kwa ajili ya kuendeleza majengo ya madarasa ili kukidhi mafunzo hadi hatua za tatu na zaidi na ukosefu wa viwanda ambavyo vitatumika katika kuwajengea wanafunzi wao umahiri zaidi na kupata ajira baada ya kuhitimu na Wanafunzi kukosa sehemu ya kufanyia mazoezi ya vitendo.

Anasema kuwa wana malengo ya kujenga mabweni mapya,kuanzisha kozi mpya za Food production na front office operation,ujenzi wa ukumbi wa mikutano,ujenzi wa nyumba za wafanyakazi,utengenezaji wa viwanja vya michezo na kuongeza madarasa.
             
Hata hivyo ametoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa kukitumia chuo hicho cha Mkoa katika huduma mbalimbali zinazopatikana hapa pia kuwapeleka watoto wao chuoni hapo ili waweze kupata mafunzo yatakayo waondolea tatizo la kukaa vijiweni kwa kukosa ajira.
                  MWISHO.


No comments:

Post a Comment