Wednesday, July 25, 2012

TUYALINDE NA KUYATUNZA MAZINGIRA ILI KUIFANYA DUNIA KUWA MAHALI SALAMA PA KUISHI



Na Joseph Mwambije
Songea
Katika vitu muhimu hapa duniani ni suala la mazingira  kwa kuwa linagusa maisha yetu ya kila siku na kwa umuhimu wake  basi hata Vitabu vya dini vimeligusia ambapo Biblia takatifu kwa kugusia inasema  baada ya kuwaumba Adamu na Eva Mungu aliwaweka katika Bustani ya Edeni ili wailinde na kuitunza.

Dunia ilipotoka mikononi mwa Muumba wake ilikuwa ikipendeza kweli kweli na kumvutia kila mtu kuikaa lakini uharibifu wa mazingira umetufikisha hapa tulipo ambapo binadamu wamekuwa wakiharibu mazingira bila hata huruma kwa dunia ambayo wao ni wakaaji ambapo kutokana na hilo Taasisi mbalimbali  pamoja na wanaharakati wa mazingira wamekuwa wakipigia kelele uharibifu wa mazingira.

Uharibifu wa mazingira umekuwa ukichangiwa na vitendo na tabia za binadamu katika kukata miti ovyo,kutengeneza mkaa lakini pia kwa Nchi zilizoendelea uharibifu wa mazingira umekuwa ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na viwanda ambapo moshi wake umekuwa ukiwaathiri binadamu kiafya kwa kuwasababishia magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa kansa.

Ukipita vijijini leo misitu ya asili imebaki vipara kutokana na ufyekaji wa miti ovyo usiozingatia falsafa ya kata mti panda mti unaofanywa na  baadhi ya watu wasio wastaarabu ambao wanayaharibu mazingira kana kwamba wao watakwenda kuishi kwenye
Sayari nyingine tofauti na hii  wanyoiharibu.

Lakini pia kwa sasa dunia imeendelea sana na  baadhi ya Nchi zimekuwa zikitengeneza silaha nzito ambazo nazo kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikiharibu mazingira kwa kutoa moshi mapiganoni au katika majaribio.

Lakini tukizungumzia katika mazingira yetu katika  Mkoa wetu wa Ruvuma na Nchi kwa ujumla kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira umekuwa ukifanyika kwa kuchoma mkaa na kukata miti ovyo na athari zake zimeshaanza kujionyesha na hili ni dhahiri kwamba athari za uharibifu wa mazingira zinatishia  viumbe hai wakiwemo wanyama na binadamu.

Kutokana na uharibifu huo wa mazingira  tumekuwa hatupati mvua za kutosha  na hilo lipelekea kukosa mazao ya kutosha na kutishia  kuingiliwa na janga la njaa na tusipochukua hatua za tahadhari huko mbeleni  Nchi yetu inaweza kugeuka jangwa siku si nyingi.

Nimeanza kwa kuinukuu Biblia kwamba Mungu alipowaumba Adamu na Eva aliwapa Bustani ya Edeni wailinde na kuitunza si kuiharibu na kama wangeamua kuharibu mazingira basi sisi wa vizazi hivi vinavyoharibu mazingira visingeikuta kwa mantiki hiyo basi ni wajibu wa kila mmoja kuyatunza mazingira ili kuifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi.

Sidhani kama kuna mtu akipewa nyumba ili ailinde na kuitunza na badala yake yeye akaamua kuiharibu hivyo basi tuna kila sababu ya msingi ya kubadili tabia na kuacha kuharibu mazingira na badala yake tuyalinde na kuyatunza.

Hapa Songea imezoeleka kuwepo na kampeni za upandaji miti pasi na mikakati ya kuiendeleza miti iliyopandwa na utamaduni huu ubadilishwe wa kampeni ya kupanda miti bila kuendeleza huku kampeni za kupanda miti zikigharimu pesa nyingi bila mafasnikio ya kuiendeleza miti iliyopandwa.

Nafikiri kunapofanyika kampeni za upandaji miti kuwepo na tahmini ya miti iliyopandwa awali  je ni miti kiasi gani iliyoharibika na mikakati ikoje kuwadhibiti wanaoharibu miti pamoja na kuwachukulia hatu wafanyakazi wa Taasisi ya misitu wasiwajibika kati utunzaji wa mazingira.

Suala la mazingira ni pana sana,kwa upande mwingine Halmashauri ya  Manispaa  ya Songea inapaswa kuwajibika katika utunzaji wa mazingira ya viunga vya mji wa Songea kwa kuondoa taka zilizolundikana katika Manispa hiyo na kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Hivyo basi katika kampeni ya mazingira hebu kila mwananchi aone kwamba  kutunza mazingira ni suala la  kila mmoja si la viongozi pekee na tuache kutupa taka ovyo ili kuzuia magonjwa ya mlipuko.

Hivyo basi ni wajibu wetu sote kushirikiana kwa kuyalinda na kuyatunza mazingira ili kuifanya dunia kuwa  mahali salama na pazuri kwa kuishi ambapo patamvutia kila mmoja wetu na si kumchukiza.
Mwisho
 
 



No comments:

Post a Comment