Joseph Mwambije
Songea
Wakulima mkoani Ruvuma wamelalamikia uhaba wa upatikanaji wa taarifa na habari sahihi na zenye manufaa za kilimo kwa wakazi wa maeneo ya vijijini kuwa umechangia wao kutofanya vizuri katika shughuli zao na kuendelea kuwa masikini.
Wakulima hao walitoa malalamiko hayo juzi
kwenye mafunzo ya kuwajengea wakulima uelewa wa sera, mikataba, dira
pamoja na mikakati inayoandaliwa na serikali, ambayo yanatolewa na Mtandao wa
Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa ufadhili wa shirika la Ujerumani la
Meserior.
Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa
kwenye vijiji mbalimbali
kwa kuwashirikisha wakulima na viongozi wa serikali ngazi ya kijiji na
kata ambapo Wakulima hao walisema kutokana na tatizo hilo wamefanya
jitihada
binafsi za kutafuta ili kupata habari hizo, lakini hawakufanikiwa baada
ya
kukosa ushirikiano toka kwa wataalam na viongozi wa serikali.
“Tumekuwa tukienda ofisini kwa viongozi wetu kuwaomba
machapisho mbalimbali kama katiba na sera lakini
nao wamekuwa wamekuwa wakituambia kuwa hawana hata tunapowaambia wafuatilie watuletee hakuna
tunachokipata, tumebaki kusikia habari kwa watu tu ambao mara nyingi huwa siyo
sahihi,” alisema Rashid Haule mkulima wa
kata ya Subira Songea mjini.
Aliongeza kuwa “kwa mfano hivi sasa tunapigania tupate
nakala za katiba lakini tunaambiwa hazipatikani ili hali tunaambiwa timu ya
kukusanya maoni itakapokuja twende kutoa maoni yetu, jiulize tutatoa maoni gani
wakati katiba ya zamani hatuijui?”
Aidha wakulima hao walilaumu serikali kwa kuwalazimisha
wakulima vijijini kutekeleza mikakati ambayo hawaijui na hakuna jitihada
zinazowekwa za kuhakikisha habari sahihi zinawafikia walengwa.
Hata hivyo wakulima hao walizishukuru asasi na mashirika
yasiyo ya kiserikali kama MVIWATA, ambayo
yamekuwa yakiwasambazia machapisho mbalimbali yenye lengo la kumuelimisha
mwananchi wa kijijini.
Kwa upande wao viongozi wa serikali ngazi za mitaa, vijiji
na kata wamekiri ofisi zao kutokuwa na machapisho yenye habari muhimu kwa
wakulima na kusema wao pia wamekuwa wakisikia tu habari za kuwepo kwa
machapisho kadhaa lakini nakala zake hazijawafikia .
“Kuna vijarida vimetoka lakini kama
sisi wenyeviti wa mitaa hatuna na vingine ndio tumeviona hapa kupitia kwenu MVIWATA
zaidi tunapewa vitabu vyenye kanuni za kuwaongoza raia na vijarida vidogo
vidogo vya kuhimiza watu watumie neti,”. Alisema Bw. Paulo Mumba Mwenyekiti wa mtaa katika kata ya subira.
Naye Afisa ugani
wa kata ya Mpandangindo Bw. Eleuterius Ngowi alikiri kuwa licha ya kuwa katika
sekta ya kilimo lakini hana habari sahihi kuhusiana na Mpango wa Maendeleo ya
Kilimo wa Wilaya (DADPS) kwa kuwa hajawezeshwa vya kutosha.
Akizungumza
kwenye mafunzo hayo, mratibu wa MVIWATA wa Mkoa wa Ruvuma Ladslaus Bigambo, alisema mafunzo hayo
yanatolewa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa MVIWATA wa kuwajengea uwezo na hamasa
ya kujisomea machapisho au vitabu mbalimbali vinavyomgusa moja kwa moja mkulima
ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowazunguka kama njia
mojawapo ya kutetea maslahi yao.
Alisema imebidi
kuwahamasisha wakulima kuona umuhimu wa kujisomea kwani kuna vitu vingi
vinavyowahusu ambavyo hawavijui na viongozi wanatumia udhaifu huo
kutokuwatekelezea haki zao kwa kuwa wanafahamu hakuna mkulima atayewauliza wala
kuwawajibisha.
“Dira ya Maendeleo
ya Taifa inahamasisha mtu kujiwekea akiba na kuwekeza katika maeneo yenye tija
kwa lengo la kujenga utajiri wa mtu binafsi, kwa kutumia dira hii viongozi wetu
Serikalini wanafanya watakavyo masuala ya ufisadi na hakuna hatua yoyote wanayochukuliwa
na Serikali kwa sababu hienda wanatimiza Dira ya Taifa ya Maendeleo” alisema
Bw. Ladslausi.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuendelea kutolewa katika kata kumi mkoani hapa zilizoko kwenye wilaya za Songea Mjini, Songea vijijini, Tunduru na Mbinga, na katika kila wilaya zimechaguliwa kata mbili zenye idadi ya wakulima 100 na wakiwakilishi wa serikali .
Mwisho
No comments:
Post a Comment