“TANZANIA iliundwa mwaka 11964 kwa kuunganisha visiwa vya Bahari ya Hindi vya Zimbabwe na Pemba vilivyoungana na nchi ya Bara iliyokuwa ikiitwa Tanganyika…”.
Hii ni sehemu ya wasilisho la hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alilolitoa wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa viongozi na wataalamu wa elimu katika Bara la Afrika uliofanyika Afrika Kusini tangu Oktoba 5 hadi 7 mwaka huu.
Makosa hayo yaliyotajwa mwanzo wa makala hii – tena kutoka kwa waziri wa elimu – ni ya kusikitisha. Yanasikitisha zaidi, kwani yanatoa ujumbe kwamba inavyoonekana ni jambo adimu kwa viongozi na watendaji wa kazi za umma kufanya matayarisho ya kazi zao zikiwemo za vitendo au za maneno.
Hapa jambo moja ni dhahiri: Tukianzia na kosa kwamba Tanzania ilizaliwa mwaka 11964 (yaani mwaka elfu kumi na moja na mia tisa sitini na nne), na kwamba Tanzania hiyohiyo ilitokana na kuunganishwa kwa visiwa vya Bahari ya Hindi vya Zimbabwe (ambapo Zimbabwe ni moja ya nchi za kusini mwa Afrika), ni kwamba aliyeandika wasilisho hilo alilifanya kwa kulipua bila kuwa na umakini wowote.
Pia, kosa jingine alilolifanya Waziri Mulugo katika wasilisho lake alilolitoa lote katika lugha ya Kiingereza, ni kwamba Shahada ya Uzamili (Masters) na Shahada ya Uzamivu (PhD) hutolewa na NACTE (National Council for Technical Education), jambo ambalo si kweli.
Kama makosa yote hayo aliyaandika waziri Mulugo mwenyewe, basi atakuwa aliyaandika bila umakini, kwani alilazimika kuirudia tena kazi yake hiyo mara kadhaa na kuhakikisha kwamba ilikuwa sahihi, hususani kwa vile ilikuwa inapelekwa kwenda kwa wataalam na wasomi wenzake wa Afrika. Hii ni pamoja na Watanzania aliokuwa nao katika msafara wake, na mamilioni ya Watanzania ambao wangemsikia akiitoa mada hiyo moja kwa moja au baadaye kuisoma au kuisikia katika vyombo vya habari.
Vilevile, kama wasilisho hilo lilitayarishwa na maofisa wa wizara yake na yeye akalichukua na kuliweka kwenye mkoba wake moja kwa moja bila kulipitia, basi ni dhahiri waziri huyo alifanya kitendo cha hatari sana – kwake na kwa taifa!
Alikuwa na uhakika gani kwamba alichoandikiwa kilikuwa sahihi bila kukisoma? Hivyo, ndivyo kazi zinavyofanyika katika ofisi zetu za Tanzania?
Maswali ni mengi, lakini kitu kimoja ni dhahiri: Makosa hayo aliyasema Waziri Philipo Mulugo! Si mwingine!
Kitu cha kutia uchungu sana ni kwamba makosa au uzembe huo umetoka katika kinywa cha waziri anayeshughulikia elimu! Hilo ni jambo la kusikitisha na kuwakatisha tamaa zaidi Watanzania ambao wengi wao tayari wamekata tamaa kwamba elimu na mfumo mzima wa elimu nchini unaotolewa na taasisi za serikali ni wa kiwango cha chini.
Kibaya zaidi ni kwamba, pamoja na makosa au kasoro zote zilizokuwemo katika wasilisho la waziri huyo tangu alitoe, hakuna hatua yoyote ambayo hadi leo imechukuliwa na wizara yake kuelezea makosa hayo iwapo yalikuwa ni ya bahati mbaya au vipi!
Walioyasikia na kuyasoma magazetini wameachwa waamue wanavyotaka, hakuna ambaye ameingilia na kutoa ufafanuzi wowote.
Tukio hilo ambalo limefanywa na waziri ambaye ni miongoni mwa mawaziri walioteuliwa katika baraza jipya na Rais Kikwete katika kuwapa matumaini mapya Watanzania, kweli ni la kusikitisha mbali na kuendeleza moyo wa manung’uniko kwamba hakuna lolote jipya katika baraza hilo lililokabidhiwa madaraka hivi karibuni.
Hii ndiyo aina ya maisha ambayo Watanzania wameyazoea na kuona kwamba viongozi kufanya makosa au uzembe na kukaa kimya bila kufafanua chochote kwa wananchi ndiyo jadi yetu.
Hakuna uwajibikaji wala kuomba radhi!
CHANZO-BLOGU YA GLOBAL
No comments:
Post a Comment