.Ni mapendekezo ya Rasimu ya katiba mpya
Kutokana na
rasimu ya Katiba Mpya kupendekeza kufutwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu,
rasimu hiyo inapendekeza waziri yeyote mwandamizi ateuliwe kukaimu
nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa rais na makamu
wake hawapo nchini kutokana na sababu zozote zile.
Mapendekezo hayo ni tofauti na Katiba ya sasa
ambayo inatamka kwamba ikiwa Rais na Makamu wake hawapo, basi nafasi
hiyo ya juu katika nchi itashikwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Waziri Mkuu aliwekwa katika orodha ya wanaoweza
kukaimu nafasi hiyo katika marekebisho ya Katiba yaliyofanywa mwaka 2000
kupitia waraka maalumu wa Serikali (white paper) na baadaye kupitishwa
na Bunge.
Kabla ya marekebisho hayo ya 13, Ibara ya 37(3)(a)
na (b) ilikuwa ikieleza kuwa iwapo Rais na Makamu wake hawapo nafasi
hiyo ilitakiwa kushikiliwa na Spika wa Bunge na kama hayupo basi Jaji
Mkuu wa Tanzania ndiye alitakiwa kukaimu nafasi hiyo.
Lakini mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya katika
Ibara ya 73(1)(b)na (c) inaeleza kuwa endapo Rais na Makamu wake
hawatakuwapo basi nafasi hiyo itashikiliwa na waziri mwandamizi na kama
hatakuwapo basi Baraza la Mawaziri ndilo litakalokuwa na dhamana ya
kuchagua mtu wa kukaimu nafasi hiyo.
Hata hivyo, mtu yeyote atakayekaimu nafasi ya
madaraka ya Rais, kwa namna yoyote ile, hatakuwa na madaraka ya kuteua
au kumwondoa madarakani kiongozi yeyote yule aliyeteuliwa na Rais kwa
mujibu wa Katiba au jambo jingine lolote kama litakavyoainishwa na Rais
katika hati ya kukasimu madaraka yake.
“Rais atakasimu madaraka yake kwa hati maalumu
aliyotia saini yake,” inaelekeza rasimu hiyo iliyozinduliwa Jumatatu
wiki hii na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba.
Kadhalika rasimu hiyo inaeleza kuwa endapo Baraza
la Mawaziri litaona kuwa Rais hawezi kumudu kazi zake kwa sababu ya
maradhi ya mwili au akili, linaweza kuandaa azimio la kumwomba Jaji Mkuu
athibitishe kwamba Rais, kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili,
hawezi kumudu kazi zake.
“Baada ya kupokea azimio hilo, atateua bodi ya
utabibu ambayo itachunguza suala hilo na kumshauri Jaji Mkuu ipasavyo,”
inaelekeza rasimu hiyo.
Jaji Mkuu baada ya kutafakari ushauri na ushahidi
wa kitabibu, atampelekea Spika hati ya kuthibitisha kwamba kutokana na
maradhi ya mwili au akili, Rais ameshindwa kumudu kazi zake, na iwapo
Jaji Mkuu hatabatilisha hati hiyo ndani ya siku saba kutokana na Rais
kupata nafuu na kurejea kazini, basi itahesabiwa kwamba kiti cha Rais
kipo wazi.
Kutokana na hali hiyo, bodi ya utabibu
itakayoteuliwa kwa mujibu wa Katiba itajumuisha watu wasiopungua watatu
kutoka miongoni mwa madaktari bingwa wanaotambuliwa na sheria inayohusu
madaktari ya Tanzania.
“Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na
Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi, kutomudu kazi
zake kutokana na maradhi ya mwili au akili au kushindwa kutekeleza kazi
na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na kushika madaraka
ya Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano,” inaeleza
sehemu nyingine ya rasimu hiyo.
CHANZO-MWANANCHI
CHANZO-MWANANCHI
No comments:
Post a Comment