Sunday, July 15, 2012

MHANDO WA TANESCO ASIMAMISHWA KAZI

 

Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi William Mhando
MKURUGENZI Mkuu Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi William Mhando amesimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo kuanzia jana.
Kwa  mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi  na kusainiwa na Mwenyekiti wake, Jenerali Mstaafu Robert Mboma, Mhando amesimamishwa kazi pamoja na watendaji wakuu wengine wa Tanesco ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Viongozi wengine wa Tanesco waliosimamishwa  kazi ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi Harun Mattambo.
Hata hivyo, Mhando alisema kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC 1) jana kuwa hana taarifa zozote kuhusiana na kusimamishwa kwake.

Ingawa  taarifa hiyo ya Mboma haikueleza nani anakaimu nafasi iliyoachwa wazi na Mhando, lakini habari tulizopata kutoka vyanzo vyetu ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco zinasema Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji atakuwa Felschami Mramba ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Masoko na Usambazaji wa Tanesco.

Hatua hiyo imetangazwa jana jijini Dar es Salaam kufuatia  kikao cha dharura cha Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kilichofanyika  Julai 13 mwaka huu, ambacho kilijadili tuhuma mbalimbali dhidi ya menejimenti ya Tanesco.
Taarifa hiyo fupi imeeleza  kuwa tuhuma dhidi ya Mhandisi Mhando ni nzito hivyo ni vyema zifanyiwe uchunguzi huru na wa kina.
“Hivyo, Bodi  iliazimia pamoja na mambo mengine kama ifuatavyo: Uchunguzi wa tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mboma alibainisha bodi yake kufanya kikao kingine cha dharura jana Julai 14, na kuamua kuwasimamisha kazi watendaji hao mara moja ili kupisha uchunguzi huo.
 “Pamoja na uamuzi huo, Bodi imechukua hatua stahiki za kuhakikisha kwamba shughuli za utendaji na uendeshaji wa Tanesco zinaendelea kama kawaida,” imesema taarifa hiyo.
Awali saa 11 jioni jana waandishi wa habari walijazana katika Ofisi ya Wizara ya Nishati na Madini iliyopo Mtaa wa Ohio, ambapo hawakufanikiwa  kuwaona wakurugenzi hao waliokuwa kwenye kikao huku wakitakiwa kuondoka eneo hilo na kusubiri kwa mbali.
Waandishi hao walilazimika kusubiri kwa takriban saa nzima ndipo alipotokea Ofisa Habari wa Wizara ya Nishati na Madini aliyetambuliwa kwa jina la Fadhili Kileo na kugawa nakala ya taarifa ya kikao hicho huku wakurugenzi hao wakipanda magari yao na kuondoka bila ya kuzungumza  na waandishi hao hali iliyowakera waandishi.
 “Jamani naomba mtusamehe sana, hii siyo kawaida yetu, imekuwa ni dharura tu ndiyo maana mnaona wakurugenzi wanaondoka,” alisema Kileo akiwasihi waandishi wa habari waliokuwa wakilalamika.
Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi naye alikataa kuzungumza na waandishi wa habari akisema kuwa hahusiki.
“Hapana mimi sihusiki, nendeni kwa hao viongozi waliokuwa kwenye kikao,” alisema  Maswi.
Mhando aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tanesco kuanzia tarehe 1 Juni, 2010.
Baada ya uteuzi huo, Mhando alisema atahakikisha wateja wote wa Tanesco wanakuwa na mita za Luku.
Kabla ya uteuzi huo, Mhando alikuwa ni Meneja Mkuu Usambazaji Umeme na Masoko katika shirika hilo.
Mhando alichukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk Idris Rashid ambaye alimaliza muda wake wa uongozi.
Wasifu wa Mhando
Mhando aliajiriwa na Tanesco mwezi Oktoba mwaka 1987 kama Mhandisi wa Umeme na baadaye alipandishwa na kuwa Mhandisi katika njia za umeme. Mwaka 1990 hadi 1992 aliteuliwa kuwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida.
Mwaka 1992 hadi 1994 alikuwa Meneja wa Mkoa wa Tanesco, Mkoa wa Mbeya. Alipandishwa cheo mwaka 1995 na kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini Magharibi hadi mwaka 1999.
Ana elimu ya Shahada ya Uzamili (Masters) katika masuala ya umeme aliyoipata mjini Havana nchini Cuba mwaka 1987, pamoja na mafunzo mengine aliyoyapata katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa muda mrefu Tanesco imekuwa katika matatizo mbalimbali ya kiutendaji na utoaji huduma yaliyosababisha taifa kuingia katika mgawo wa umeme na kudhoofisha maendeleo na ukuaji wa uchumi.

Matatizo hayo ni pamoja na uchakavu wa mitambo ya Tanesco, hujuma za miundombinu na kuingiwa kwa mikataba mibovu.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wa kutoa ufafanuzi juu ya taarifa iliyotolewa na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC), kuwa kuna ubadhirifu ndani ya Tanesco  Mei 7, mwaka huu, Mhando alisema ikigundulika kuna ubadhirifu wowote uliofanyika katika shirika hilo kutokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) basi atakuwa tayari kujiuzulu.

Taarifa ya POAC ilisema shirika hilo lilifanya ununuzi wa kati ya Sh300 bilioni hadi Sh600 bilioni lakini Mhando alisema kuwa si kweli.

"Kama nimekosea niko tayari kujiuzulu na mwajiri akiamua kunihamisha sina tatizo na ninawaambia mimi sina miaka miwili kazini na shirika linapata hati safi hilo mwelewe na mliseme," alisema Mhando.

No comments:

Post a Comment