Wednesday, July 11, 2012

WAKULIMA WALALAMIKIA KUPEWA MASHINE A KUKAMUA MAFUTA YA ALIZETI ZILIZOCHAKACHULIWA

Na Joseph Mwambije
Tunduru

Wakulima wa kijiji cha Namasakata, kata ya Namasakata wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, wameilalamikia idara ya kilimo wilayani humo kwa kuwapatia mashine za kukamua mafuta ya Alizeti ambazo zimechakachuliwa baadhi ya vifaa vyake na kuomba mamlaka za juu kufanya uchunguzi ili kubaini waliohusika.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa wakulima hao hawajapewa taarifa sahihi kuhusu viliko vifaa hivyo na kwa nini havifungwi kwenye mashine hizo, hali inayochelewesha maendeleo yao.

Wakizungumza jana kwenye jukwaa lililoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoa wa Ruvuma, wakulima hao walisema walipewa Mashine hizo baada ya kuibua miradi kupitia Mpango wa Maendeleo ya Kilimo wilayani (DADP) na kupitishwa na halmashauri ya wilaya mwaka 2010.

Vijiji vilivyopewa mashine hizo zenye upungufu wa vifaa na ambazo hadi sasa mwaka umetimia bila kufungwa vimetajwa kuwa ni pamoja na Namasakata, Mchoteka, Nakapanya, Matemanga pamoja na Tunduru mjini.

Wakulima hao walisema mchakato wa kuibua miradi hiyo ulianza mwaka 2010 na ilipofika Juni 2011 walikabidhiwa mashine hizo na walipokataa kuzichukua kwa sababu zina upungufu wa vifaa, walishinikizwa kuzichukua kwa ahadi ya kuwa mafundi toka Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) wangefika kijijini hapo na kufunga vifaa vinavyopungua.

“Ilipofika mwaka 2011 tuliambiwa mashine zimeshaletwa lakini kabla ya kukabidhiwa mashine hizo  tulitakiwa kuchangia asilimia 20 kwa kujenga banda la kuweka mashine hiyo lililogharimu Tsh 1.5 milioni na baadaye tukakabidhiwa mashine baada ya kuchangia  pia fedha za mafuta ya kuzisafirisha toka wilayani hadi hapa kijijini,” alisema mmoja wa wakulima wa kijiji cha Namasakata Bi. Maimuna Mkwanda.

Wakulima hao walisema licha ya kuahidiwa kuwa mafundi wa SIDO wangepeleka vifaa baada ya siku chache, lakini hakuna utekelezaji mpaka sasa. “Tunashangaa sana hadi leo hii Julai 2012 mashine hii haijafungwa kutokana na kutokukamilika kwa vifaa kwenye injiini na kinu na kila tukiwauliza wataalam wilayani wanasema mafundi toka SIDO ndio wenye mkataba wa kufunga mashine hizo pindi watakapokuwa tayari watakuja nao” alisema Bibi Mkwanda.

Wanasema kutokana na mashine hizo kutofanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu zilipoletwa, wamepata hasara kubwa kwani tangu walipotangaziwa kuwa andiko la kupata mashine limekubalika waliongeza uzalishaji katika zao la alizeti kwa matarajio ya kufanya biashara ya mafuta, matokeo yake wameishia kujuta kwa hasara wanayoendelea kuipata.
Kwa upande wake Afisa Pembejeo wa wilaya ya Tunduru Bw. Hassan Simba alipohojiwa kuhusiana na malalamiko hayo, alisema wakulima hao hawakumalizia asilimia 20 waliyotakiwa kutoa kama mchango wao, hali inayochangia kuchelewa kufungwa kwa mashine hizo.

“Kuna zaidi ya shilingi milioni mbili  zinazohitajika ambazo kwa sasa wilaya inazitafuta ili kufidia mchango huo wa wananchi kwa lengo la kufanikisha zoezi la kufunga mashine hizo na kila kijiji chenye mashine kinapaswa kuandaa mifuko sita ya saruji itakayotumika kufanikisha zoezi hilo,” alisema Bw Simba.

Mwisho

No comments:

Post a Comment