Sunday, August 26, 2012

KUTENGULIWA MATOKEO IGUNGA,MAKADA WA CCM WAMNYOSHEA KIDOLE MKAPA

 
Sunday, 26 August 2012 09:34


KITENDO cha Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kutengua matokeo ya ubunge Jimbo la Igunga yaliyompa ushindi Dk Dalaly Peter Kafumu (CCM), kimeibua mvutano mwingine ndani ya CCM, ambapo sasa  baadhi ya makada wake wameanza kumnyooshea kidole Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadhi ya mawaziri kuwa ndiyo chanzo cha kushindwa huko. 
Baadhi ya makada maarufu na wenye uzoefu wa muda mrefu ndani ya chama hicho tawala, kwa nyakati tofauti kwenye mahojiano na Mwananchi Jumapili wamekiri kwamba, imefika mahali ambapo CCM inapaswa ijitazame na kuwa makini juu ya watu inaopaswa kuwatumia katika  kampeni zake. 
Katika tathmini yao, makada hao wamemtaja Rais Mstaafu Mkapa na mawaziri kadhaa, wakisema kuwa CCM haikuwa makini katika kuwateua wasimame kwenye majukwaa kupiga kampeni za kisiasa.  Walitaja moja ya sababu kuwa ni Mkapa na baadhi ya mawaziri hao mashuhuri kuwa siyo wanasiasa wa jukwaani bali ni watendaji.
Licha ya CCM kujaribu kumtumia rais huyo mstaafu na mawaziri hao kutokana na heshima iliyojengeka kwao mbele ya Watanzania walio wengi, tathmini ya makada hao inaeleza kuwa hoja zao katika kampeni ama ziliwapa mwanya wapinzani, hasa Chadema kuiumbua CCM kwenye propaganda za majukwaani, hata kisheria.  
Walikuwa wakizungumzia chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni katika Jimbo la Arumeru na ule wa Igunga Oktoba mwaka jana, ambao licha ya CCM kushinda, wiki hii mahakama kuu ilitengua ushindi huo.  Kuanguka Igunga  Dk Kafumu aliibuka mshindi kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Oktoba 2, mwaka jana kuziba nafasi ya Rostam Aziz aliyejiuzulu kwa madai ya kuchoshwa na kile alichoita siasa za majitaka  ndani ya CCM, lakini mahakama imetengua ushindi wake. 
Uchaguzi huo ulikuwa wa ushindani mkubwa kati ya Dk Kafumu na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye ambaye aliamua kupinga ushindi wa Dk Kafumu mahakamani akidai hakuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo.  Kashindye alifungua kesi hiyo Machi 26, mwaka huu.  Wakati wa kampeni za uchaguzi huo vigogo mbalimbali wa CCM akiwamo Mkapa walipiga kambi Igunga na kushiriki mikutano mbalimbali ya kampeni, ambapo pamoja na mambo mengine walitoa kauli tata zilizosababisha CCM kushindwa katika kesi hiyo. 
Mbali na Mkapa viongozi wengine waliotoa kauli hizo na sasa wananyooshewa vidole ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama na Mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage.   Kauli tata ya Mkapa  Wakili wa mlalamikaji, Profesa Abdallah Safari, Agosti 20 mwaka huu aliwasilisha mahakamani hapo zaidi ya malalamiko 13 dhidi ya Dk Kafumu na wenzake. 
Mbali na kueleza yaliyozungumzwa na Dk Magufuli, Profesa Safari alidai hoja nyingine ni Baraza la Waislamu (Bakwata) Wilaya ya Igunga kuwakataza waumini wasiipigie kura Chadema na kwamba naye Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alitoa ahadi ya kugawa mahindi kwa wananchi wa Igunga siku moja kabla ya uchaguzi ili waichague CCM.  Makada waonya

Mbunge wa Kahama, James Lembeli alisema kuwa utaratibu wa sasa wa chama hicho kuwatumia viongozi wastaafu umepitwa na wakati kwa sababu Watanzania wa sasa hawahitaji kusikia maneno mengi, bali sera.  Alisema kuwa CCM inatakiwa itazame ilipojikwaa na kuacha kutafuta mchawi kwa kuwa matatizo yaliyokifikisha chama hicho kilipo sasa yanajulikana. 
“Kampeni za CCM hivi sasa hazina maandalizi, kila anayeweza kuzungumza anachukuliwa na kujumuishwa kwenye kampeni, jambo ambalo siyo sahihi,” alisema Lembeli na kuongeza:  “Inatumia watu bila kuangalia kama wanakubalika, katika chaguzi zinazokuja, chama kiwatumie  makada wanaopendwa na wananchi na wenye uwezo wa kuuza sera za chama.” 
Alitaja sababu nyingine ya CCM kuanguka hasa Igunga kuwa ni pamoja na mgawanyiko uliokuwapo ndani ya chama hicho baada ya baadhi ya makada kuzuiwa kushiriki katika kampeni hizo wakati wana mvuto kwa wapiga kura.  Akitolea mfano watu hao alisema kuwa ni pamoja na Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta, ambapo alibainisha kuwa waliotoswa katika kampeni hizo wasingeweza kuishiwa maneno ya kuzungumza na kuanza kutoa ahadi zinazovunja sheria ya uchaguzi.
Dk Kigwangallah Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dk Hamisi Kigwangallah alisema kitendo cha CCM kutumia vigogo akiwamo Rais mstaafu Mkapa katika uchaguzi wa Igunga, ndiyo chanzo cha kushindwa kwa kesi hiyo kwa kuwa walizungumza mambo yasiyo na msingi wowote.  Dk Kigwangallah ambaye Agosti 22 alichukua fomu za kuwania kiti cha Uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa alisema kuwa uchaguzi mwingine ukifanyika katika jimbo hilo, viongozi na wabunge kutoka mikoa ya Tabora, Mwanza na Shinyanga ndiyo waachwe kufanya kampeni.
“Ni kweli CCM tuliweka watu wengi, ambao walipunguza kura za chama, lakini pia walizungumza mambo yasiyostahili,” alisema Dk Kigwangallah na kuongeza:  “Uchaguzi ujao Igunga wasituletee watu kutoka CCM taifa, wanakuja na helikopta na kutumia gharama kubwa halafu mambo yanaharabika. Nadhani tubadilishe hali hii.”
Hata hivyo, alisema kuwa CCM inakubalika kwa kiasi kikubwa mkoani Tabora, hasa katika Jimbo la Igunga na kwamba kama Dk Kafumu akigombea tena, ataibuka mshindi kwani anakubalika na alishafanya mambo ya maendeleo. 
Ibrahim Kaduma Kada mkongwe wa chama hicho, Ibrahim Kaduma alipoulizwa iwapo moja ya sababu za CCM kushindwa ni kuwatumia vigogo ambao siyo mahiri katika siasa za jukwaani, hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo akitaka aachwe.  “Naomba uniache kwanza, masuala haya yanatosha …, naomba uniache tafadhali kwa hisani yako tu,” alisema Kaduma.  Ole Moloimet  Naye Lepilal Ole Moloimet, kada wa CCM aliyewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM na Serikali, alikilaumu chama chake kwa tabia ya kumtumia Rais Mstaafu Mkapa na baadhi ya mawaziri kwenye kampeni za uchaguzi. 
Alisema kitendo cha kuwatumia watu hao licha ya kusababisha wadhalilike kinaonyesha udhaifu wa watu wanaoiongoza CCM hivi sasa.  "Suala la kuwatumia marais wastaafu, kuwatumia mawaziri ni udhaifu wa viongozi wa CCM wanaoiongoza hivi sasa," alisema Moloimet.  Akizungumzia  uchaguzi wa Arumeru alisema: “Mkapa alidhalilishwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu. …Wananchi walihoji kama alishindwa mgogoro huo wakati wa utawala wake, akizungumzia suala hilo sasa atakuwa anawaongopea."
Alisema kimsingi marais wastaafu hawapaswi kutumiwa kwenye siasa, badala yake iwe ni matukio muhimu yanayohusu Watanzania wote au juu ya uhusiano wa kimataifa kama vile mgogoro wa mpaka na Malawi.  "Imefika mahali hawa viongozi wastaafu hata  wakiombwa wakanadi sera majukwaani wao wenyewe wanapaswa wajipime. Si kila kitu wakubali," alisema Moloimet.   
Tuvute subira- Mgeja  Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja alisema: “Nadhani tuvute subira kwa sababu tukianza kunyoosheana vidole nani hakufaa nani alifaa itakuwa siyo jambo zuri, kama ni hivyo mbona tulivyoshinda Igunga hawakuwalaumu walioshiriki katika kampeni.”  
Lusinde: Hakuna tatizo
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema kuwatumia wazee katika chaguzi za chama hicho hakuna tatizo, akiamini kuwa Jimbo la Igunga ni mali ya CCM na kwamba uamuzi wa kukata rufaa au kutokata anamwachia Dk Kafumu.  “Natamani kama uchaguzi ungefanyika tena ili twende tukalichukue jimbo,” alisema Lusinde.
Sababu za kutenguliwa matokeo  Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mary Nsimbo Shangali alisema Mahakama ilipokea malalamiko 15 ambayo yaliridhiwa na pande zote mbili lakini baadaye yakaongezwa madai mengine mawili hivyo kufikia 17.  Alisema hoja zilizothibitishwa na Mahakama ambazo  zilizotumika kutengua matokeo hayo ni saba kati ya 17. 
Baadhi ya hoja hizo ni pamoja madai kwamba Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alitumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbutu, ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Igunga.  Jaji Shangali aliikubali hoja nyingine ya washtaki kuwa ni ugawaji wa mahindi ya kuwawezesha wakazi wa Igunga kukabiliana na njaa wakati wa uchaguzi huo kwamba ulitumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kuwashawishi wananchi wawapigie kura.
Mbali na Dk Kafumu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uchaguzi walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga aliyetangaza matokeo hayo.    
Kauli ya Nape  Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kwamba haoni kuwa kauli za Rais Mkapa, Magufuli, Mukama ndizo zilizokiangusha chama hicho alisema: “Ndiyo maana tunataka kukata rufaa kwa sababu hatukubaliani na hiyo hoja.”
Vita ya kuwania uongozi
Katika hatua nyingine, upepo wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM umezidi kushika kasi baada ya Mbunge wa Jimbo la Kahama, James Lembeli kuchukua fomu ya kugombea Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga huku akitamba kuwa ameingia kwa lengo la kumaliza makundi ya kisiasa yaliyokithiri ndani ya chama hicho. 
Lembeli amechukua fomu sambamba na mpinzani wake mkubwa kisiasa Khamis Mgeja, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa CCM mkoani humo.  Mbali na vigogo hao, mbunge wa zamani wa Shinyanga mjini Leonard Derefa naye alichukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
Wengine ni Teresia Kashinje, Bonaventure Mguziki, Regina Masanja na Alex Seseja.   Hata hivyo, katika kinyang’anyiro hicho wagombea wanaoonyesha kuvutia  hisia za wanaCCM wa Shinyanga ni Lembeli na Mgeja, ambao wamekuwa mahasimu wa siku nyingi katika siasa za mkoa huo, huku wote wakitoka wilayani Kahama.
Katika majigambo yao Lembeli amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akitamba kuwa atahakikisha anamng’oa Mgeja katika nafasi hiyo huku Mgeja naye akidai hasimu wake huyo ni ‘sisimizi’ ambaye hamnyimi usingizi.
Makada wengine wa chama hicho waliochukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali ni pamoja na  Mkurugenzi wa Uchaguzi CCM Makao Makuu, Matson Chizii ambaye amejitosa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Dar es Salaam.  Wengine waliochukua fomu za kuwania nafasi hiyo mkoani Dar es Salaam ni  John Guninita anayetetea nafasi hiyo na Mjumbe wa Nec, Ramadhan Madabida.

Naye Katibu wa Nec, Uchumi na Fedha na Mbunge wa Iramba  Magharibi, Mwigulu Nchemba amejitosa kuwania nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) kupitia kundi la viti 10 wakati Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda akijitosa kuwania nafasi ya NEC kupitia Wilaya ya Lindi Vijijini.  Aliyekuwa mbunge wa Misungwi, Dalali Shibiriti naye amechukua fomu ya kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) kupitia wilaya hiyo. 
Uchaguzi huo pia umemwibua aliyekuwa Mbunge wa Busega, Dk Raphael Chegeni ambapo baadhi ya vijana wa wilaya hiyo walimchukulia fomu kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Wilaya ya Busega.  Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi naye amejitosa kuwania nafasi ya uenyekiti wa mkoa wa chama hicho mkoani Mbeya.

No comments:

Post a Comment