Na Joseph Mwambije
Ruvuma
MGOMO wa walimu Mkoani Ruvuma umeeendelea katika siku yake ya tatu huku hali ikiwa mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini ambako walimu hawaendi kabisa Shuleni na Ofisi zimefungwa licha ya Viongozi wa Mkoa huo kuzungumza kwa uneyenyekevu na baadhi ya Wakuu wa Shule wakiwaomba kushawishi walimu wasitishe mgomo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya Shule walimu wamebaki nyumbani na Ofisi za Shule zimefungwa huku wanafunzi wakirandaranda wasijue cha kufanya.
Katika Shule ya Msingi Ruhila katika Manispaa ya Songea ni Mkuu wa Shule hiyo na Mkewe ambao ni walimu pekee walioendelea na kazi.
Shule ya Msingi Mwembachai walimu wanane hawakuja kabisa Shuleni na wamebaki nyumbani wakiendelea na shughuli zao binafsi kuendelea na mgomo wao wa kuishinikiza Serikali kushughulikia madai yao.
Jana Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Said Mwambungu akiwa ameongozana na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa huo aliwaomba Wakuu wa Shule za Msingi na za Sekondari kuwahawiwishi Walimu kusitisha mgomo wao wakati akizungumza nao kwenye Ukumbi wa Chuo kikuu huria.
Akizungumza kwenye Mkutano huo kwa unyenyekevu mkubwa Mkuu wa Wilaya ya Songea Bw. Joseph Mkilikiti aliwaomba Wakuu hao wa Shule kutafakari kwamba watoto wanakosa haki yao ya kufundishwa hivyo watumie busara na kuwashawishi walimu kurejea kazini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Walimu(CWT) Bw. Castory Ngonyani amesema wamesikitishwa na tabia ya Viongozi wa Serikali kuwatisha walimu walio kwenye mgomo na kutaka waache tabia hiyo kwa kuwa mgomo huo uko kisheria.
Amewataka walimu kutoogopa vitisho na kuendelea na mgomo huo endelevu na kubainisha kuwa kitendo cha Waajiri kuwalazimisha walimu walio kwenye mgomo kurudi kazin kabla ya kutatuliwa madai yao ni ukiukwaji wa Sheria.
‘Walimu hawapaswi kutishwa na Serikali kwa kuwa haina mamlaka ya kuwafukuza kazi bali mamlaka hayo yako kwenye Tume ya utumishi wa walimu(TSD) hivyo walimu wapuuze vitisho hivyo na kuendelea na mgomo’alisema Bw. Ngonyani.
Naye Katibu wa CWT wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Luya Ngonyani amesema Mkuu wa Mkoa Bw. Mwambungu hana mamlaka ya kuzuia mgomo ho kwa kuwa ni wa kitaifa na upo kihalali na kisheria kwa muijibu wa Sheria Namba 6 ya ajira na mahusiano ya kazi ya mwaka 2004 kifungu cha 80 kifungu kidogo cha 1.
Alisema kuwa katika Mkoa wa Ruvuma asilimia 97.1.2 waliunga mkono mgomo huo kwa kura na asilimia ndogo iliyobakia hawakuuga mkono ambao alidai kuwa ndio wanaokwenda kazini.
Alisema madai yao ya msingi ni nyongeza ya mshahara kwa asilmia ,posho ya kufundishia na posho ya mazingira magumu ya kazi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment