Tuesday, September 18, 2012

Ugumba wawatesa Watanzania wengi


 

Wauguzi nchini Kenya wakiwa wamewabeba watoto walipatikana kwa njia ya mwananmke kupandikizwa mbegu za kiume, ripoti za nchini kenya zinaonyesha watanzania 60 wamekwenda nchini humo kupata huduma hiyo. Picha na Arthur okwemba
WASAKA WATOTO KENYA KWA SH5.4 MIL, HADI SASA WANAWAKE 60 WAMEHUDUMIWA DAKTARI WA MUHUMBILI AKIRI TATIZO NI KUBWA
Na Mwandishi Wetu,
TATIZO la uzazi linaonekana kushika kasi nchini baada ya idadi kubwa ya wanandoa kukimbilia Kenya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto kwa gharama ya zaidi ya Sh5 milioni.Kati ya wageni 10 wanaokwenda katika vituo vya upandikizaji vya Aga Khan na Nairobi IVF Centre nchini humo, wanne wanatoka Tanzania.Licha ya kuwapo kwa huduma hiyo nchini, imeelezwa kwamba Watanzania wengi wanakimbilia huko kutokana na unafuu wa gharama na ubora wa huduma.
Huduma hiyo ni ya mwanamke kupandikizwa mbegu ya kiume ili kuweza kushika mimba na baadaye kupata mtoto.
Mmiliki wa Kituo cha Upandikizaji cha Nairobi (Nairobi IVF Centre), Dk Joshua Noreh alisema kwa mwaka kliniki yake hupokea zaidi ya wagonjwa 270 kutoka mataifa mbalimbali  likiwamo Bara la Ulaya.
Alisema wagonjwa kutoka Tanzania walianza kumiminika katika kliniki hiyo kuanzia mwaka 2006 na ukiondoa gharama za matibabu ambazo ni Sh5.4 milioni zipo gharama za ushauri na uchunguzi wa tatizo.
“Gharama ya ushauri peke yake ni Sh42,000 za Tanzania. Baada ya ushauri, mgonjwa hutozwa Sh420,000 kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo. Gharama za matibabu hutegemea ukubwa wa tatizo. Tiba yenyewe ni upandikizaji wa mbegu, hadi hatua za kuirutubisha,” alisema.
Dk Noreh alisema ukijumlisha gharama za usafiri, malazi, mlo na tiba kwa wagonjwa wanaotoka Tanzania, wengi wao hutumia kati ya Sh8milioni hadi Sh10 milioni, kwa ajili ya kupata mimba.
Imeelezwa kuwa raia wa Uganda hukimbilia Kenya kukwepa gharama kubwa kwani nchini humo hugharimu kiasi cha Sh500,000 ya Uganda (sawa na Sh9.5 milioni) wakati huduma hiyo hupatikana Kenya kwa Sh300,000 (sawa na Sh5.4 milioni) kwa mzunguko.
“Tuna vituo zaidi ya vitano vya IVF hapa Kenya, ndiyo maana Kenya imekuwa kimbilio la wanandoa au wapenzi kupata matibabu ya aina mbalimbali za ugumba. Lakini  kikubwa ni huduma bora na gharama nafuu ndiyo sababu ya ongezeko hili la wageni kutoka nje.”
Alisema baadhi ya nchi hazina huduma ya IVF hivyo wanandoa huenda Kenya na wengine wanayo huduma hiyo katika nchi zao ila wanachagua Kenya kwa sababu ya urahisi wa tiba hiyo na kuwapo kwa mbegu za wanaume wa Kiafrika zilizohifadhiwa.
Nchi nyingine ambazo wanandoa wake wanaongoza   kwenda Kenya kwa ajili ya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto ni Uganda, Sudan ya Kusini, Marekani na Ethiopia.
Mtaalamu kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Nairobi, Dk Prafull Patel alisema idadi ya wanaohitaji huduma hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutoka mataifa ya Afrika, Uingereza na Marekani.
Alisema zaidi ya robo tatu ya wanaopata huduma hiyo ni watu kutoka nje ya Kenya, lakini hasa ni kutokana na unafuu wa gharama za huduma hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine.
Nchini Uganda, IVF inagharimu Sh9,000,000 za Tanzania wakati Uingereza inagharimu zaidi ya Sh10,800,000 za Tanzania na kwa wenza zinafikia Sh21,600,000 kwa kila mzunguko huku Marekani ikigharimu Sh10,620,000 na Sh19,800,000 kwa mzunguko.
Hii inamaanisha kwamba gharama nchini Kenya ni nusu ya gharama inayolipiwa Marekani, Ulaya na nchi nyingine za Afrika. Hiyo inaelezwa kuwa chanzo cha ongezeko la idadi ya wageni kwenda Kenya kusaka tiba ya ugumba.

Upandikizaji unavyokuwa
Upandikizaji huo hufanyika kwa kuchukua mbegu za mwanamume na kuzipandikiza katika mirija ya uzazi ya mwanamke.
Mwanamke mwenye matatizo huweza kwenda peke yake kupandikizwa kwa kununua mbegu zilizohifadhiwa katika kliniki au wanandoa kwenda pamoja na mwanamume kutoa mbegu ambazo zitapandikizwa kwa mwanamke.
“Tiba huchukua mwezi mmoja, huanzia siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza hedhi na siku ya yai kurutubishwa lakini mwanamume hutumia siku moja tu pale mbegu zake zinapohitajika.”
Dk Noreh alisema sababu ya kuanza tiba siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza mzunguko wake wa mwezi ni kulenga tarehe za uchavushaji, kwani kipindi hicho mbegu za mwanamume hupandikizwa na kusababisha mimba kutungwa.
“Mbegu zilizorutubishwa huachwa kwa siku mbili mpaka tano ndani ya chombo maalumu ili kukuza kiinitete (embryo) kabla ya kuhamishwa katika nyumba ya uzazi ya mwanamke kwa ajili ya kutungisha mimba ya kawaida.”
Alisema tatizo la ugumba linaongezeka duniani na njia hiyo inatumika kuwasaidia wanawake wasiokuwa na mayai ambao mirija yao ya kuyasafirishia imeziba na wanaume ambao manii yao ni dhaifu na hushindwa kuogelea hadi kufikia yai la mwanamke...
“Tatizo la ugumba kwa sasa ni wastani wa asilimia 10, hiyo ina maana kwamba kati ya wanandoa 10 mmojawapo hana uwezo wa kushika mimba. Kiwango hiki kwa sasa kinakua kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo wanawake wa sasa kuchelewa kuolewa wakitoa kipaumbele kumalizia masomo,” alisema Dk Noreh.

Wataalamu wa Tanzania
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili, Dk Henry Mwakyoma alisema ongezeko la Watanzania kufuata huduma hiyo Kenya, limesababishwa na kukua kwa tatizo la uzazi nchini.
Dk Mwakyoma alisema huduma hiyo hutolewa kama tatizo la uzazi analo mwanamke. Alisema kama mwanamume ndiye mwenye tatizo, huduma hiyo haiwezi kutolewa.
“Kama mwanamke ana tatizo la uzazi, kwa mfano mirija imeziba, kizazi kimelegea, anaweza kufanyiwa upandikizaji na kupata mtoto, lakini kama mbegu za mwanamume ni dhaifu, hakuna kitu kinafanyika,” alisema.
Dk Mwakyoma ambaye aliwahi kufanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 80 ya wanaume nchini wana tatizo la ugumba wa kudumu au wa muda, alisema mfumo wa maisha wa sasa ndicho chanzo cha ongezeko la tatizo la uzazi.
Daktari kutoka kituo kimoja cha upandikizaji nchini ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema huduma hiyo inapatikana katika kituo hicho kwa bei nafuu kuliko huko Kenya.
“Gharama za hapa zinategemea ukubwa wa tatizo la mhusika, mchakato wake na afya yake. Wapo wengine hawahitaji kupandikizwa, wengine wanahitaji tu dawa, pia wapo wengine wanaweza kufanyiwa upandikizaji kwa zaidi ya mara moja,” alisema.
Alisema tangu kufunguliwa kwa kituo hicho Februari mwaka huu, idadi ya wanandoa wanaokwenda kupata huduma hiyo imekuwa ikiongezeka. Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi takwimu rasmi kwa mwezi au tangu kufunguliwa kwake.
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment