Wednesday, October 31, 2012

RUSHWA NJE NJE UCHAGUZI WA JUMUIYA YA WAZAZI YA CCM

WAPAMBE NUSURA WAZICHAPE KAVUKAVU, UCHAGUZI KUFANYIKA DODOMA LEO

Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima 

WAPAMBE NUSURA WAZICHAPE KAVUKAVU, UCHAGUZI KUFANYIKA DODOMA LEO
Full story



Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKATI uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukifanyika leo, suala la rushwa, makundi na wajumbe kutaka kuzipiga yalitawala jana.
Uchaguzi huo wa wazazi ndiyo wa funga dimba la mfululizo wa chaguzi za chama hicho tawala kuanzia ngazi za shina tangu Aprili.
Tuhuma hizo za rushwa zimejitokeza licha ya juzi wagombea mbalimbali kukaririwa wakiyakana makundi ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na ajenda maalumu ya kusaka urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kupitia chama hicho.
Kampeni na rushwa
Mmoja wa wajumbe kutoka mkoani Iringa aliuambia Mtandao huu kuwa tayari baadhi ya wajumbe wanaoonekana kuwa na msimamo mkali wamekuwa wakipewa Sh100,000 kila mmoja wakati wajumbe wengine wamekuwa wakihongwa kati ya Sh40,000 na 70,000.
“Nikimwona Rais Jakaya Kikwete nitamwambia. Hali hii siyo nzuri na haiwezi kuvumiliwa. Kama alivyosema juzijuzi hapa nilimsikia, lazima achukue hatua, la sivyo chama chetu kitakufa,” alisema mjumbe huyo ambaye aliomba asitajwe jina.
Katika hatua nyingine, makundi ya baadhi ya wajumbe waliokuwa wameketi katika moja ya baa maarufu mjini Dodoma, juzi usiku walitimka mbio baada ya kuona gari likiegeshwa pembezoni mwa baa hiyo.
Wajumbe hao waliokuwa kwenye harakati za kupanga mikakati ya kuzunguka katika nyumba za kulala wageni kwa ajili ya ‘kuonana’ na wajumbe, walitimka wakidhani kuwa gari hilo lilikuwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wagombea wanaowania uenyekiti, John Barongo na Abdallah Bulembo juzi, kwa nyakati tofauti walikanusha kuwa na maslahi na makundi yanayodaiwa kushiriki katika vitendo vya kutoa rushwa katika uchaguzi huo unaofanyika leo. Mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Martha Mlata alikataa kuzungumzia uchaguzi huo.
Uchaguzi huo, unahitimisha uchaguzi wa jumuiya tatu za chama hicho, baada ya ule wa UWT na UVCCM ambazo zilizua malalamiko kutokana na kutawaliwa na madai ya rushwa.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akifunga mkutano wa UWT na baadaye alipofungua ule wa UVCCM,   alikemea vitendo hivyo na kueleza athari za rushwa katika chaguzi za chama.

Mchuano wa wabunge
Kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa UWT, mchuano mwingine mkali unaonekana katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa Nec, huku kukiwa na idadi kubwa ya wabunge wanaowania nafasi hiyo.
Majina 16 yamepitishwa kuwania viti vitatu vya Nec kwa upande wa Tanzania Bara, wakati kwa upande wa Tanzania Visiwani majina yaliyopitishwa ni saba kugombea nafasi mbili.
Miongoni mwa wanaowania nafasi tatu Bara ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Manyanya na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu.
Pia wamo wabunge ambao majimbo yao yapo kwenye mabano Said Bwanamdogo (Chalinze), Vita Kawawa (Namtumbo), Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini) na Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu, Esther Nyawazwa.
Wengine katika kundi hilo ni Norad Kigola, Priscilla Mbwaga, Dk Salim Chikago, Jeremia Wambura, Bernard Murunya, Thobias Mwilapwa, Paulo Kirigini na Clementina Mollel.
Kutoka Zanzibar, wanaowania nafasi mbili za Nec ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Perera Ame Silima, Abdulla Khamis Feruz, Ali Suleiman Othman, Fatuma Abeid Haji, Panya Ali Abdalla, Twaha Ally Muhajir na Hassan Rajab Khatib.
Pia mkutano wa leo unatarajiwa kumchagua Makamu Mwenyekiti, nafasi inayowaniwa na Hassan Rajab Khatib, Ali Issa Ali na Dogo Iddi Mabrouk.
Utawachagua pia wajumbe wa Baraza Kuu la Wazazi na wawakilishi wa jumuiya hiyo katika mabaraza ya UVCCM na UWT.

Vijembe vya kampeni
Kampeni zimekuwa zikipamba moto kadri muda wa uchaguzi unavyokaribia na mbinu mbalimbali zimekuwa zikitumika ili kujihakikishia ushindi.
Magari mengi yamepambwa picha nyingi za wagombea, wapambe wanapita sehemu mbalimbali kuomba kura na kuta za uzio wa ofisi za CCM zimechafuka kwa picha za wagombea.
Ushindani mkubwa unaonekana kuwa baina ya Barongo na Bulembo ambao jana walikuwa kivutio kikubwa walipokutana katika ofisi za CCM Makao Makuu, Dodoma ambako walikumbatiana kisha kuanza kurushiana vijembe.
Bulembo alisema: “Nilipomkuta anachukua fomu, nilimwuliza mwalimu wangu huyu (Barongo) kwamba nilidhani kwamba sasa unaniachia nikutue mzigo, kumbe bado tena nawewe unagombea?”
Barongo alimjibu akisema: “Hilo haliwezekani kabisa, ujue ninyi bado watoto hamjakomaa bado mnahitaji kuongozwa, kwa hiyo wewe tulia kwanza muda mwafaka ukifika nitakukabidhi.”
Jana asubuhi, Bulembo alifika katika Viwanja vya Bunge kuomba kura kwa baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa mkutano mkuu wa jumuiya hiyo.
Muda mfupi kabla ya wabunge kuingia ukumbini, Bulembo alikuwa nje ya lango kuu la kuingilia kwenye ukumbi wa Bunge na kila mbunge aliyejitokeza alimsalimia kisha kuomba kura kwa wale ambao ni wajumbe hao.
Mlata jana kwa muda mrefu hakuonekana katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM na taarifa zinasema huenda alikuwa akihudhuria kikao cha Baraza Kuu la Jumuiya hiyo kilichofanyika jana katika Chuo cha Mipango.
Licha ya kutokuwapo kwake, kulikuwa na vijana wachache waliokuwa wamevalia mabango makubwa yenye picha yake, vifuani na kwenye migongo yao wakimpigia kampeni.
Wafuasi nusura wazichape
Wakati Bulembo na Barongo wakirushiana vijembe kwa furaha, watu wanaoaminika kuwa ni wafuasi wao nusura wachapane makonde walipokuwa wakiimba nyimbo za hamasa CCM Makao Makuu.
Wafuasi hao jana walikuwa wakizunguka wakiwa na mabango yenye kuwanadi wagombea hao katika ofisi hizo kati ya saa sita na saa nane mchana huku wakiimba nyimbo za hamasa.
Hali hiyo ilisababisha kutosikilizana katika eneo hilo, hivyo kuwalazimu maofisa wa CCM kuviamuru kuondoka na kuelekea katika mbele ya jengo la vikao vya NEC maarufu kama White House. Viliitikia wito na kwenda huko ambako viliendelea kuimba nyimbo za hamasa.
Wakati vikiwa katika eneo hilo, wafuasi hao walianza kurushiana maneno makali kwa huku kila upande ukidai kufanyiwa rafu na upande mwingine, hali iliyozua tafrani iliyodumu kwa zaidi ya dakika 20.
Hata hivyo baadhi ya makada wa pande hizo mbili, walitumia busara na kuwatuliza na kila kikundi kuelekea upande tofauti na kuhitimisha shamrashara hizo.
Chanzo-gazeti la  Mwananchi

No comments:

Post a Comment