Wednesday, December 5, 2012

FAMILIA YA SHARO YAIBUA MAZITO


Kwa ufupi
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo chake ni kichwa kupondeka.
“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.
Full Story

Share


FAMILIA ya msanii Hussein Ramadhani Mkiety (Sharo Milionea) aliyekufa katika ajali wilayani Muheza wiki
iliyopita imedai kuwa haiamini kwamba kifo cha mtoto huyo kilitokana na ajali, hivyo kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli.

Mjomba wa marehemu , Mohamed Msenga alisema jana kwamba familia imekuwa na shaka juu ya mazingira ya kifo hicho baada ya kurejeshewa nguo za msanii huyo zilizokuwa zimeibwa baada ya ajali lakini hazikuwa na damu.

Msenga alisema muda mfupi baada ya mama mzazi wa Marehemu Zaina Mwaimu Mkiety (54), kuitwa polisi na kukabidhiwa  vitu mbalimbali zikiwamo nguo ambazo marehemu alikuwa amevaa siku ya ajali hawakuona hata alama ya damu jambo ambalo liliwashangaza.
Alisema shaka hiyo ilianzia katika eneo ambalo ajali hiyo ilitokea akisema walipofika na kuonyeshwa mahala alipokuwa ameangukia, hawakuona damu jambo ambalo liliwatia shaka.
Alisema begi la nguo za msanii huyo lilikuwa na udongo mwingi likionyesha kwamba walioiba walikuwa wamelifukia kabla ya kusalimisha lakini hakuna damu zilizoonekana.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo chake ni kichwa kupondeka.
“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.

Kuhusu madai ya nguo kutokuwa na damu, alisema marehemu alipata mpasuko wa ndani kwa ndani na siyo wa  nje, ndiyo maana alipofikishwa chumba cha maiti damu zilionekana zikiwa zimeganda masikioni.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia  alisema: “Hiyo ni taarifa ambayo jeshi la polisi litaifanyia kazi kwa kuingia kwa kina katika kuchunguza ili kuridhisha pande zote.”


Mama yake alia kukosa mjukuu
Katika hatua nyingine, mama mzazi wa msanii huyo amesema kutoachiwa mjukuu na tarehe za mwisho wa mwezi ni alama ambazo zitasababisha awe akimkumbuka mwanaye huyo milele.
Akizungumza nyumbani kwake, katika Kitongoji cha Jibandeni Kijiji cha Lusanga wilayani hapa alisema kila ulipokuwa ukifikia mwisho wa mwezi ulikuwa ni muda wake wa neema kwani Sharo Milionea alimtumia fedha za matumizi yake binafsi pamoja na familia nzima nyumbani hapo.

“Pamoja na kwamba kila mara alikuwa akinitumia fedha za kutatua shida zangu mbalimbali nilizokuwa nikimweleza lakini kila mwisho wa mwezi alikuwa akihakikisha anatuma fungu la matumizi yangu na ndugu zake hapa nyumbani,” alisema mama huyo.
Alisema mwisho wa mwezi itakuwa ni alama ya kudumu ya kumbukumbu ya mwanawe kwa sababu ni wakati ambao alikuwa akimtumia fedha za matumizi yake pamoja na
familia nzima.

Kuhusu mjukuu alisema: “Sharo ni mwanangu wa pekee wa kiume, amekufa bila kuniachia mjukuu.. hii inaniuma sana lakini namshukuru Mungu kwani amechukua kiumbe chake na ndiye ajuaye siri iliyofichika mbele yangu,” alisema.

Alisema hadi alipofariki hakuwahi kumdokeza juu ya kuwa na mtoto wala kumpa mimba msichana yeyote... “Unajua Sharo Milionea alizaliwa pacha na mwenzake Hassan lakini mwenzake alifariki dunia siku tano baada ya kuzaliwa kwa hiyo katika kizazi changu mwanangu pekee wa kiume alikuwa Sharo Milionea ambaye nilitumaini kwamba angeniletea wajukuu,” alisema Zaina.

Alisema Sharo Milionea amekufa kabla hajatekeleza ndoto yake ya kumjengea nyumba ya kisasa pamoja na kuweka miradi ya kuboresha maisha yake azma ambayo aliiweka mwezi mmoja kabla ya kupata ajali iliyotoa uhai wake.

Atoa ya moyoni kwa walioshiriki msiba
Zaina alitoa shukrani za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Salma kwa kutuma ujumbe maalumu pamoja na rambirambi kutokana na msiba wa mwanaye huyo. Pia alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, wasanii, waandishi wa habari na kampuni mbalimbali
zilizoshiriki pamoja na kutuma salamu za rambirambi.
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment