MZOZO WA ISRAELI NA IRANI NA HOFU YA KUZUKA VITA YA TATU YA DUNIA
NA JOSEPH MWAMBIJE.
NI
KATIKA muda mrefu sasa Mataifa Mawili ya Israeli na Irani yamekuwa
katika Vita kali ya maneno na kutishia amani ya Mashariki ya Kati na ya
Dunia kwa ujumla.
Wakati
Irani ikijigamba kuifuata Israeli katika ramani ya Dunia nayo Israeli
imekuwa ikijibu kwamba itakuwa imeiwahi kuifuta Irani kabla haijatimiza
azma yake hiyo.
Hivi
karibuni Nchi ya Israeli ilifanya zoezi zito la kivita ambalo
halijawahi kufanyika katika historia ya Taifa hilo ambalo limekuwa
katika misukosuko ya kivita na kuleta hofu kwa Wananchi wa Mashariki ya
Kati hasa wa Irani na Syria. Hata hivyo Waziri Mkuu wa Israeli Ehud
Olmert Alisema hilo ni zoezi la kawaida la kutaka kuona jinsi raia wake
walivyo tayari kukabiliana na majanga mbalimbali ya kivita.
Zoezi
hilo la kivita lilijumuisha ving`ora vya muda wa dakika moja na nusu
vilivyowashwa kote Israeli Saa 4:39 asubuhi isipokuwa kwenye eneo la Mji
wa Kusini wa Sderot ambao umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara kwa
Maroketi ya Wapalestina yanayorushwa toka Gaza.
Hata
hivyo mazoezi hayo yalifanyika siku chache baada ya baadhi ya Viongozi
wa Nchi hiyo kukiri kwamba Nchi hiyo imo katika hatari ya kushambuliwa.
Waziri wa Miundombinu wa Israeli, Bnjamin Ben Eliezer Alisema shambulizi
lolote kutoka Irani litasababisha mashambulizi makali ya kulipiza
kutoka Israeli. Alisema Irani inawachokoza kupitia marafiki zao Syria na
Hizbullah kwa kuwapatia silaha.
Waziri wa Ulinzi wa Israeli, Ehud Barak Alisema zoezi hilo ni Matokeo ya vita vya mwaka 2006 kati ya Jeshi la Israeli na
kikundi cha Hizbullah ambayo Israeli ilishindwa kukitokomeza kikundi
hicho. Vita hiyo ilipiganwa baada ya baadhi ya Wanajeshi wa Israeli
kutekwa na kikundi hicho.
Lakini
wakati Israeli ikifanya zoezi hilo Irani nayo ilijibu kwa kuyafanyia
majaribio makombora yake ambayo ilijigamba kwamba yana uwezo wa kupiga
hadi Nchini Israeli na Marekani. Majaribio ya makombora hayo yalileta na wasiwasi duniani na kuleta hofu kwa hizo mbili kuingia vitani.
Mwaka
2007 Rais wa Marekani George Bush alionya kwamba Nchi hizo kama
zitaingia vitani kuna wasiwasi wa kuzuka Vita ya tatu ya dunia ambapo
vyombo vya habari vya Israeli viliripoti mwaka huo kwa kutoa michoro
inayoonyesha ramani ya Gogu na Magofu ambayo inahusisha nchi zote muhimu
katika mgogoro huo. Rais George Bush Alisema mpango wa Irani wa
kumiliki Silaha za Nyuklia utasababisha kuzuka kwa vita ya tatu ya
dunia.
Novemba
Mwaka 2007 vituo vya Televisheni vya Channel 2 na channel 10 vya
Israeli vilionyesha ramani ya dunia na michoro inayoonyesha mvutano wa
pande zote mbili zinazopigana na kuashiria kuibuka kwa Vita ya tatu ya
dunia.
Vituo
hivyo vilionyesha nyuma ya upande wa Israeli kuna Marekani, Uingereza,
Ufaransa na Ujerumani wakati nyuma ya Irani kuna Urusi, China, Syria na
Korea Kaskazini. Katika mwaka huohuo na mwezi Novemba aliwaambia
waandishi wa habari kwamba kitendo cha Irani kumiliki Silaha za Nyuklia
kinaleta hatari ya kuzuka vita ya tatu ya dunia.
“Kama
Irani itamiliki Silaha za Nyuklia itakuwa tishio kubwa kwa amani ya
dunia, alisema Rais Bush na kuongeza kwa hiyo ninawaambia ninyi watu
kwamba kama mnapenda kuzuia Vita ya tatu ya dunia ni vema mngeizuia
Irani isimiliki Silaha za nyuklia.
Siku
chache katika Mwaka huohuo Rais wa Urusi Viladimir Putin alitembelea
Irani na kuishutumu Marekani kwa kugoma kuacha kutumia nguvu dhidi ya
mpango wa nyuklia wa Irani. Urusi ilipinga Irani isiwekewe vikwazo
vikali zaidi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambako ina
kura ya veto ambapo Rais huyo wa Urusi alidai kwamba hakuna ushahidi wa
kutosha kuthibitisha kwamba Irani inatengeneza Silaha za nyuklia
ukiachilia mbali mpango wao kwa ajili ya nishati na matumizi ya amani.
Mzozo
wa Irani na Israeli ukiachwa uendelee kwa hatari ya kuzuka vita ya tatu
ya dunia ambayo itaathiri dunia nzima na wakazi waishio ndani yake. Ni
vyame mzozo huo ukamalizwa haraka kuliko kuachwa uendelee kitu
kinachoweza kuleta madhara makubwa baadaye. Mzozo huu si wa kushangilia
hata kidogo na ni vyema Viongozi wa dini wakaingilia kati kuombea Nchi
hizi zisiingie vitani. Hivi inapotokea Nchi moja inatishia kuifuta Nchi
nyingine katika ramani ya dunia unafikiri mwisho wake ni nini? Bila
shaka hilo ni swali gumu kulijibu au rais kulijibu.
Endapo
Irani na Israeli zitaingia vitani ni wazi Nchi marafiki na Irani
zitaingia Vitani kuisaidia Nchi hiyo na upande mwingine Nchi rafiki na
Israeli zitaingia Vitani kuisaidia Nchi hiyo hapo ndipo wasiwasi mkubwa
unapozuka wakati huu ambapo nishati ya mafuta imekuwa ikipanda bai kila
kukicha, hivyo basi ni wazi basi kama nchi hizi mbili zitaingia Vitani
Uchumi wa dunia utaathiriwa na kuzidi kuyumba.
Wakati
Nchi hizi zikiwa katika mzozo wa kuingia Vitani hebu tujikumbushe vita
ya kwanza ya dunia na ya pili ilivyokuwa na ni jinsi gani ilileta
madhara makubwa kwa walimwengu wakati vikipiganwa na viliwaletea ufahari
Viongozi walioziongoza nchi hizo, kwa mfano Adolf Hitler anatajwa kama
Jasusi la kikoloni lililotawala dunia kwa muda wa Masaa 24 au siku moja
wakati wa vita ya pili ya dunia.
Vita
vya kwanza vya dunia vilianza mwaka 1914 na kumalizika mwaka 1918
vikianzia ulaya na kuenea katika makoloni mbalimbali duniani kote.
Katika Vita hivyo Waingereza, Wafaransa na rafiki zao walipambana na
Wajerumani na rafiki zao Ulaya ilikuwa uwanja Mkuu wa mapambano huku
Makoloni ya Mataifa hayo yakburutwa kushiriki katika Vita hivyo.
Katika
Afrika Mashariki Koloni la Wajerumani ambalo lilitokana na nchi tatu za
Tanganyika, Burundi na Rwanda zililazimishwa kupigana upande wa
Waingereza. Kiini cha Vita hivyo kilikuwa kugombania
Makoloni.Mataifa haya yalikuwa na nia ya kupata utajiri ili kutawala
Uchumi wa Ulimwengu. Mabeberu wa Ujerumani walianza kuzitishia Nchi
nyingine za ulimwengu na kwa hiyo Ujerumani ilipata upinzani kutoka
mataifa mengine na kuamua kuzusha vita.
Katika
Bara la Afrika mapambano makali kushinda yote yalikuwa katika Afrika
Mashariki. Hii ni kwa sababu Koloni la Ujerumani la Afrika Mashariki
lilikuwa muhimu kwa Nchi hiyo. Katika Koloni hilo Wajerumani walikuwa
wameanzisha Kilimo cha Mazao ya biashara na chakula kwa kiwango kikubwa.
Hadi kufikia Mwaka 1913 Walowezi wa Ujerumani walikuwa na mashamba
makubwa ya Mkonge, Mpira na Kahawa na hivyo nguvu ya Ujerumani ililenga
kulilinda Koloni hilo.
Wakati
Ujerumani ikilenga kulilinda Koloni hilo Wapinzani hao walilenga
kuzivunja nguvu zao katika Afrika ya Mashariki. Kwa mantiki hiyo basi
kulikuwa na Mkusanyiko mkubwa wa Majeshi ya pande zote mbili katika
Afrika Mashariki ambapo Wajerumani wakiwa na Jeshi la Askari 16,000
walikabiliana na Waingereza waliokuwa na askari 140,000.
Katika
Mapambano hayo Koloni la Ujerumani la Afrika Mashariki likiongozwa na
Kiongozi wao shupavu Jenerali Von Lettow Vorbeck lilishambuliwa na
Waingereza kutoka Kaskazini wakitumia Makoloni ya Kenya na Uganda huku
Jeshi hilola Ujerumani likiyakabili vilivyo Majeshi ya Uingereza, licha
ya Uchache wao. Kwa upande wa Magharibi, Majeshi ya Wabelgiji
yalishambulia kuanzia Burundi na Rwanda na kuelekea Tabora Tanganyika
(Tanzania).
Upande
wa Kusini Majeshi ya Waingereza kutoka Zambia, Zimbabwe na Malawi
yalishambulia Koloni la Wajerumani. Wakati huohuo Majeshi ya Makaburu wa
Afrika ya Kusini yakiongozwa na Jenerali Smuts yalikuja kuwasaidia
Waingereza katika Mapambano yao dhidi ya Wajerumani.
Liccha
ya koloni la Wajerumani kuzingirwa na Majeshi ya Uingereza na rafiki
zao lakini Majeshi ya Ujerumani hayakushindwa katika Uwanja wa
mapambano. Hata hivyo Majeshi ya Ujerumani Ukanda wa Afrika Mashariki
yalilazimika kujisalimisha kwa Waingereza baada ya Ujerumani kushindwa
Sehemu za Ulaya Mwaka 1918 na ndio ukawa mwisho wa vita ya kwanza ya
dunia vilivyoanza Mwaka 1914.
ATHARI YA VITA YA KWANZA YA DUNIA
Vita
vya kwanza vya dunia viliharibu kabisa Uchumi wa Koloni la ujerumani
kwa sababu kwa upande wa Afrika Mashariki Koloni hilo ndilo lilikuwa
Uwanja wa Vita wakati pia likiwa tegemeo la Ujerumani. Wakati Vita
vikipiganwa mashamba ya Mkonge, Mibuni na Mpira hayakuangaliwa. Kaskazini mwa Tanzania sehemu za Usambara na Kilimanjaro baadhi ya mashamba yalikuwa bado yako katika hali nzuri.
Lakini
mashamba mengi yalikuwa katikati na Kusini mwa Tanganyika yalikuwa
yameharibika na wakati huo wa Vita hakukuwapo na Manamba wa kuhudumia
mashamba hayo kwa sababu wafanyakazi wengi wa mashamba hayo
walilazimishwa kujiunga na Jeshi la Wajerumani. Pia Vita iliathiri
uendeshaji wa Shule na njia za Mawasiliano.
Vita
hiyo ilisababisha zaidi ya Waafrika 20,000 kupoteza maisha katika
ukanda wa Afrika Mashariki pekee. Pia Vita ilisababisha njaa kali na
watu walipoteza maisha huku watu wengine wakifa kwa magonjwa yaliyozuka
wakati wa Vita kwa mfano ilikadiriwa kuwa Ugonjwa wa mafua makali
uliozuka mwaka 1918 uliua asilimia mbili ya watu wote wa Koloni la
Ujerumani la Afrika Mashariki walipoteza maisha yao kwa manufaa ya
Mabepari na migogoro yote iliyotokea wakati wa Vita haikuwa na manufaa
kwa Waafrika.
Vita
hivyo viliharibu kabisa Uchumi wa Tanganyika(Tanzania kwa sasa) ambavyo
ilikuwa Koloni la Ujerumani ambapo Miundombinu yote ya Uzalishaji mali
na biashara iliharibika na hata zile bidhaa chache zilizozalishwa
hazikuweza kusafirishwa kwenda Nchi za Nje wala bidhaa kutoka Nje
hazikuweza kuingizwa Nchini kwa sababu ya Vita Koloni hilo lilikuwa
limezingirwa na Majeshi ya Uingereza.
Mara
baada ya Vita hivyo kumalizika Nchi za Ulaya zilizoshinda zikiongozwa
na Uingereza zilikutana Varsailles huko Ufaransa na kuunda Umoja kwa
mara ya kwanza, uliojulikana kama Jumuiya ya Mataifa. Wajerumani
walinyang`anywaywa Makoloni yao yote ambayo yalikabidhiwa kwa Jumuiya ya
Mataifa ambayo iligawa Koloni la Ujerumani la Afrika Mashariki katika
sehemu mbili huku sehemu kubwa ikikabidhiwa kwa Waingereza Mwaka 1920 na
Waingereza waliiita sehemu hiyo Tanganyika.
Sehemu
ya pili iliyogawanywa ilikuwa Burundi na Rwanda ambazo zilikabidhiwa
kwa Wabelgiji. Wakoloni hawa walipewa dhamana ya kutawala Nchi hizo kwa
niaba ya Jumuia ya Mataifa. Waliagizwa kuangalia mambo ya
Uchumi, Ustawi wa Jamii na Ufundishaji wa maadili kwa Wananchi. Taifa
Tawala lilitakiwa kupeleka taarifa ya maendeleo ya Koloni kwa Jumuiya ya
Mataifa kila mwaka.
VITA YA PILI YA DUNIA
Wajerumani
hawakuridhika na kunyang`anywa Makoloni yao na Jumuiya ya Mataifa na
hivyo basi Ujerumani ikawa na nia ya kuyarejesha Makoloni yake hali
ambayo ilizua wasiwasi Vita ya pili ya dunia ambavyo vilianza Mwaka 1939
hadi mwaka 1945.
Katika
Vita hivyo Wafaransa, Wabelgiji, Waingereza, Wamarekani na Warusi
walikuwa upande mmoja huku upande mwingine kulikuwa na Wajerumani,
Waitalia na Wajapani. Katika Bara la Afrika mapambano makubwa yalikuwa
sehemu za Kaskazini na Kaskazini Mashariki. Tanganyika ililazimishwa
kushiriki Vita hivi kwa kutoa askari, chakula na michango ya aina
mbalimbali.
Watanganyika
wengi walilazimika kushiriki katika Vita kama askari. Baadhi yao
walishiriki katika mapambano dhidi ya Waitaliano huko Ethiopia na
Somalia huku baadhi yao walikwenda hadi Bara Hindi ambako walipambana na Majeshi ya Wajapani huko Burma.
Katika Vita hivyo Ujerumani ikiongozwa na Adolf Hilter
iliweza kuyakabili mapambano vilivyo na kufanikiwa kutawala dunia kwa
muda wa Masaa 24. Lakini hata hivyo kibao kilibadilika ghafla ambapo
Ujerumani ilibanwa sehemu za Ulaya kwenye Nchi za baridi ambapo askari wa Ujerumani walishindwa Vita mwaka 1945 kutokana na baridi kali.
Madhara
ya Vita vya pili vya dunia hayatofautiani sana na madhara yaliyotokea
wakati wa Vita vya kwanza ambapo watu wengi walipoteza maisha na
Miundombinu kuharibiwa huku Uchumi wa Nchi zilizoshiriki Vita ukiyumba
Naam
hayo ndiyo yaliyojiri wakati wa Vita vya kwanza vya dunia na Vita vya
pili vya dunia. Vita vya kwanza vya dunia vilitokana na Mataifa ya Ulaya
kugombea Makoloni wakati Vita vya pili vya dunia vilitokana na
Ujerumani kutaka kurejesha Makoloni yake iliyonyang`anywa na Jumuiya ya
Mataifa.
Lakini
Mzozo katika kile kinachotaka kusababisha Vita ya tatu ya dunia
hakieleweki na ni vyema Umoja wa Mataifa ukatumia busara kutatua mzozo
huo vinginevyo dunia inaweza kuingia Vitani.
Ni
Rai yangu kwa Umoja wa Mataifa kuomba usifanya maamuzi kama
yaliyofanywa na Jumuiya ya Mataifa mwaka 1918 na kuifanya Ujerumani
ijipange kwa Vita nyingin ya pili ya dunia.
MWISHO.
Makala hii imeandikwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali vikiwamo Vitabu vya historia na Mitandao ya Internet.
Mwandishi anapatikana kwa simu 0755/0655 761195.
Barua pepe-josephmwambije@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment