.Wavunja gari,jeneza wampekua marehemu wapora sh. 20 milioni
.waipora maiti
Full Story
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia
gari lililokuwa linasafirisha maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani
Mara kisha kupora takriban Sh19.8 milioni walizokuwa nazo waombolezaji.
Katika tukio hilo la kusikitisha lililotokea juzi
mkoani Singida, majambazi hao walivunja vioo vyote vya gari pamoja na
jeneza lililokuwa na mwili wa Munchari Lyoba aliyekuwa mwanafunzi wa
mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) cha Morogoro na
kumpekua marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya
chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida, mkuu wa
msafara uliokuwa ukisafirisha maiti, Makaranga alisema kuwa tukio hilo
lilitokea juzi saa 7:30 usiku katika gari aina ya Land Cruiser mali ya
SUA.
Akisimulia tukio hilo, Makaranga alisema kuwa
lilitokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Mwanza nje kidogo ya Mji wa
Singida kwenye kona maarufu kwa jina la Mohammed Trans kuelekea mkoani
Mara.
Alisema kuwa gari hilo pamoja na jeneza,
lililobeba viongozi wa wanafunzi sita na viongozi wengine wanne
lilipofika eneo la tukio, walikuta mawe makubwa yamepangwa barabarani na
kuwalazimisha kusimama ndipo wakavamiwa na kundi kubwa la vijana, ambao
walibeba bunduki mbili aina ya gobore, marungu, mashoka na mawe.
“Walipofika walipiga kioo cha gari letu kwa mbele
na kumparaza kwa panga usoni dereva wetu. Baada ya hapo walivunja vioo
vyote na kutuamuru kutoa kila kitu tulichokuwa nacho,” alisema
Makaranga.
Makaranga alisema kuwa katika tukio hilo, aliporwa
Sh2 milioni alizokabidhiwa azihifadhi kwa ajili ya kugharimia msafara
huo, Sh8.8 milioni zilizochangwa na wanafunzi kama rambirambi kwa
mwenzao na jumla ya Sh9 milioni ambazo wasindikizaji walikuwa nazo
mifukoni mwao.
“Pia tuliporwa simu zetu zote za mikononi, viatu, laptop na mabegi yote ya nguo zetu,” alisema.
Makaranga aliyeeleza kuwa anafanya kazi za
kiutawala SUA, aliwataja walioumizwa na majambazi hao kuwa ni pamoja na
yeye, dereva wao na kiongozi wa wanafunzi, Idd Idd ambao walitibiwa
katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na kuruhusiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa amewasiliana na
uongozi wa SUA ili watume gari lingine na kukarabati jeneza
lililoharibiwa na majambazi hao.
Mlozi aliongeza kuwa kwa ushirikiano wa Jeshi la
Polisi na Kamati ya Ulinzi na Usalama, watahakikisha watu waliofanya
unyama huo, wanakamatwa haraka iwezekanavyo ili waweze kufikishwa mbele
ya vyombo vya sheria.
“Nimesikitishwa sana na tukio hili, inaelekea sasa
binadamu tunaanza kutoka kwenye utu na kuhamia kwenye vitendo ambavyo
binadamu wa Mwenyezi Mungu hawezi kuthubutu kuvifanya. Watu wanafikia
hata kufungua jeneza na kuanza kulisachi,” alisema Mlozi akionyesha
masikitiko
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment