Mkapa akoleza mjadala wa gesi
HABARI KAMILI
WITO wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kutaka suluhu ya mgogoro wa gesi unaoendelea baina ya Serikali na wakazi wa mikoa ya kusini, umepokewa kwa hisia tofauti. Baadhi ya wasomi wamempongeza huku wakazi kadhaa wa Mtwara wakimpinga.
WITO wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kutaka suluhu ya mgogoro wa gesi unaoendelea baina ya Serikali na wakazi wa mikoa ya kusini, umepokewa kwa hisia tofauti. Baadhi ya wasomi wamempongeza huku wakazi kadhaa wa Mtwara wakimpinga.
Juzi, baada ya mgogoro huo kuendelea kwa takriban mwezi mmoja sasa, Mkapa alizitaka pande hizo mbili kutafuta mwafaka akieleza kuwa linalowezekana leo, lisingoje kesho.
“Mtafaruku huu haufai kuachwa na kutishia usalama, mipango ya maendeleo siyo siri, mikakati na mbinu za utekelezaji wake siyo siri. Maelezo yake mazuri yanaweza kutolewa yakadhihirisha namna na kasi ambayo rasilimali zinawanufaisha wananchi wa eneo zilimo na taifa zima,” alisema Mkapa katika taarifa yake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema jana kuwa kauli ya Mkapa ni nzuri, huku akisisitiza kuwa katika suala hilo, lazima utaifa uwekwe mbele.
“Hata wakati wa ujenzi wa Barabara ya Mtwara, wapo waliosema kuwa mikoa ya kusini inatengwa, kauli hizi zilikuwapo tangu zamani, kikubwa ni suala hili kuchukuliwa kitaifa zaidi,” alisema Dk Bana.
Wazee watafuta suluhu Dar
Wazee wa Mtwara Mikindani wako Dar es Salaam kusaka suluhu ya mgogoro huo, baada ya kusema kwamba wamebaini kuwa kutakuwa na uvunjifu wa amani kama suala hilo litaachwa liendelee.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wazee hao walisema suala hilo linaleta hofu kubwa kwa taifa hivyo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Katibu wa wazee hao, Selemani Mademu alisema wananchi wa Mtwara wako tayari kufa kuliko kuona wakidharauliwa katika suala hilo.
Mademu alisema: “Wananchi wa Mtwara wanaamini kuwa kituo cha kuchakata gesi asilia kama kitajengwa Mtwara kitatoa fursa kubwa ya kushawishi wawekezaji ambao watajenga viwanda vitakavyotumia malighafi ya gesi asilia na hivyo kuchochea maendeleo ya Mtwara kwa jumla,” alisema na kuongeza kuwa kama Serikali inaamini kwamba wazo lake la kuisafirisha hadi Dar es Salaam ni jema na lenye manufaa kwa wananchi wa Mtwara, ingejikita katika kutoa elimu badala ya kukaa kimya na kuendelea na kile inachoamini.
“Wanamtwara hatupendi kuendelea kuelezwa kwamba tutanufaika na gesi iliyogunduliwa kwa kuahidiwa viwanda kama ambavyo imekuwa desturi ya Serikali yetu. Tunahitaji vitendo vitawale badala ya ahadi ambazo hazitekelezeki. Kwa mfano barabara, umeme, kuimarishwa kwa bandari, mikopo kwa ajili ya ujasiriamali, viwanda vidogo vya kubangua korosho n.k.” alisema.
Wengine wapinga
Mwenyekiti wa Umoja wa Maendeleo Mikoa ya Kusini (UMMK), Said Mannoro (72) alimshutumu Mkapa akidai kuwa ndiye chanzo cha gesi ya Songosongo kupelekwa Dar es Salaam.
Mzee Mannoro ambaye alifika katika ofisi za gazeti hili, Tabata Relini, Dar es Salaam jana alisema Mkapa anatakiwa kueleza faida walizopata wananchi wa Lindi baada ya gesi ya Songosongo inayozalishwa mkoani humo, kupelekwa Dar es Salaam.
Mbali na mzee huyo, baadhi ya viongozi wa dini na vyama vya siasa nao wamempinga Mkapa wakisema kuwa ushauri wake umeegemea upande mmoja na kwamba alipaswa kumshauri Rais Jakaya Kikwete.
Askofu Mteule wa Kanisa la KKKT Dayosisi Mpya ya Kusini Mashariki, Mchungaji Lucas Mbedule alisema Mkapa, amechelewa kutoa ushauri wake na kwamba kwa hali ya sasa alipaswa kumshauri Rais Kikwete akubaliane na matakwa ya wananchi.
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment