Thursday, January 24, 2013

KIGAMBONI YAWA MJI UNAOJITEGEMEA

.yanyofolewa Temeke

(Picha na www.ippmedia.com)
 HABARI KAMILI
 
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi, Prof Anna Tibaijuka akiuzungumza na waandishi wa habari juu ya serikali kuunda Wakala wa Uendelezaji wa mji wa Kigamboni jijini Dar es Salaam jana. 
 
Wengine ni Mkurugenzi wa Upimaji Ramani, Sellasie Mayunga (kushoto), Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Albina Bura na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uendelezaji wa mji wa Kigamboni, Vicent Shahidi.
Serikali imetangaza kuuondoa Mji wa Kigamboni kuwa chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na kuanzisha mamlaka ya upangaji wa mji huo ijulikanayo, kama Wakala wa Kusimamia Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni (KDA).

KDA ambayo ilianzishwa na serikali kisheria Januari 18, mwaka huu, itasimamia uendelezaji wa mji huo unaotarajiwa kuwa wa kisasa.
      
Mji huo pia unatarajiwa kuwa kitovu cha kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jiji la Dar es Salaam ili liweze kushindana na miji mingine duniani katika kuvutia uwekezaji, biashara na utalii na kukuza ajira, hasa kwa vijana.                                                                                                         Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuwa KDA itaongozwa na mkurugenzi mtendaji. Alisema mkurugenzi huyo atateuliwa pamoja na wakurugenzi sita watakaokuwa na wakuu wa idara.

Hata hivyo, alisema kwa sasa KDA inaongozwa na kaimu mkurugenzi mtendaji. Mbali na hilo, alisema KDA pia itasimamiwa na Bodi ya Ushauri pamoja na Baraza la Ushauri.

Alisema Baraza hilo litakuwa na wajumbe wanaowawakilisha wadau wote, hususan wabunge na madiwani wa eneo litakaloendelezwa na KDA.

Waziri Tibaijuka alisema KDA itakuwa na kazi ya kutafuta fedha za kutosha kwa ajili ya mradi, kupanga mji na kusimamia ujenzi wa mji kwa viwango vya kimataifa. Hata hivyo, alisema wananchi watashirikishwa kushauri.

Alisema fidia kwa wananchi ambao makazi yao yatatwaliwa kwa ajili ya kupisha uendelezaji wa mji itatolewa, lakini hawatahamishwa, badala yake watapewa makazi mapya katika mji huo mpya wa Kigamboni.

Hata hivyo, alisema ambaye atalipwa fidia hataruhusiwa kwenda kuishi katika makazi yaliyo nje ya mji mpya wa Kigamboni.

Alifafanua kuwa, atakayeruhusiwa ni yule atakayeonyesha hatimiliki ya kiwanja anachokwenda kujenga nje ya mji huo kwa ajili ya kuishi huko.

Waziri Tibaijuka alisema eneo litakalosimamiwa na KDA lina ukubwa wa hekta 50,934.
Alisema katika uendelezaji huo, kata zote za Kigamboni zimeunganishwa na kwamba, mji huo utaendelezwa na kuwa wa kisasa.

Waziri Tibaijuka alisema yeye ni miongoni mwa wataalamu duniani walioshiriki katika ujenzi wa mji wa Dubai.

Hivyo, akasema hataki kuona tena Watanzania wakifika Dubai waanze kuushangaa mji huo.
Alisema eneo la mji wa Kigamboni linahusisha Kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada, Somangila, Kisarawe II, Kimbiji na Pemba Mnazi.

Waziri Tibaijuka alisema katika kusimamia uendelezaji huo, KDA itaongozwa na mpango kabambe.

Alisema mpango huo ni pamoja na kuwa na mji uliopangwa kwa kiwango cha kimataifa utakaokuwa mfano wa kuigwa na miji mingine nchini.

Pia kupunguza ujenzi holela, kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na shughuli za kiuchumi na kijamii, kama vile viwanda, hoteli, utalii, biashara, elimu, ofisi, afya na vituo vya michezo.

Vilevile, kupunguza msongamano wa magari na huduma za kiuchumi na kijamii katikati ya jiji la Dar es Salaam, kuongezeka kwa thamani ya ardhi katika maeneo ya mji kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara, maji na umeme itakayowezesha kukuza biashara, ujenzi wa majengo na viwanda.

Pia kuhamasisha uwekezaji ili kuongeza ajira, hasa kwa vijana na wananchi wengi wataweza kumiliki nyumba katika maeneo yaliyopangwa na kutumia nyumba zao kupata mikopo kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali.

Alisema mji mpya wa Kigamboni utakuwa na watu takriban 400,000 kulinganisha na watu 80,000 waliopo sasa.

Waziri Tibaijuka alisema katika kutekeleza mpango huo, uwakilishi wa wananchi utakuwapo kama ambavyo umekuwapo katika mchakato wa ufanikishaji wake.

Hii ni hatua mpya na kubwa inachukuliwa na serikali katika kukabiliana na mradi wa Kigamboni ambao wananchi kadhaa wakiongozwa na Mbunge wao, Dk. Faustine Ndugulile, wanadai kuwa wananchi hawajashirikishwa katika mradi huo.

Tayari wananchi hao wameunda kamati ya kusimamia madai yao wakihofia kwamba huenda unalenga kuwapora maeneo yao na kuwapa wawekezaji wakubwa.

MBUNGE AZUNGUMZA
Ndugulie akizungumza na NIPASHE jana jioni, alisema anasikitishwa na hatua zinazozidi kuchukuliwa na serikali kwa eneo la Kigamboni bila kuwashirikisha wananchi.

“Kweli tunaanza mwaka mpya vibaya. Yaani hawa wameshindwa kuwashirikisha wananchi kwenye zile kata za awali nne sasa wameongeza zingine na eneo kubwa zaidi bila hata kuzungumza nao… huu  ni uvunjaji wa sheria, kwa nini lakini?” alihoji.

Mbunge huyo alisema ingawa dhana ya mradi huo ni nzuri, lakini kutokuwashirikisha wananchi ni uvunjaji wa sheria.
“Serikali inaendelea na ubabe na kuvunja sheria sijui ni kwa nini,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment