Sunday, January 27, 2013

MWAKYEMBE ATAMBA KUIFANYA BANDARI YA DAR KUWA YA KISASA

 
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe. 

HABARI KAMILI

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ametamba kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa ya mfano duniani kwa utoaji wa huduma bora za upakiaji na upakuaji kwa wananchi wa ndani na nje ya nchi.
Hayo aliyasema jana alipokuwa akizungumza na madereva wa malori na wadau wengine wa bandari baada ya madereva hao kumtaka awasikilize kero zao wakati alipokuwa bandarini hapo na msafara wa mawaziri kutoka nchini Uganda.
Dk Mwakyembe alilazimika kurudi bandarini hapo jana baada ya juzi kuombwa na madereva hao kuonana naye ili wamweleze kero zao na yeye aliahidi kurudi kesho yake ambayo ilikuwa jana.
Katika mazungumzo hayo Waziri Mwakyembe aliwataka madereva hao kuwa wawazi kueleza kero zote zinazowakabili bandarini hapo kwa kuwa yeye hasa ndiye mwenye dhamana ya kurekebisha na kuboresha huduma bandarini.
Wadau hao walimweleza waziri kuwa kero ni nyingi zikiwamo za upatikanaji wa vibali vya upakiaji na foleni ya magari, ratiba na muda wa kupakia, mwingiliano wa kazi za meli na malori ya mizigo na madai ya rushwa kwa wafanyakazi hasa wa kitengo cha upakiaji wa makontena bandarini hapo.
Waziri aliwataka watendaji bandarini hapo kuondoa urasimu kwani hakuna haja ya malori ya kusafirisha mizigo nje ya nchi kuwa na foleni ndefu bandarini hapo kwa kuwa suala hili linapunguza ushindani wetu katika soko.
“Hakuna haja ya malori ya mizigo yaendayo nje ya nchi kuchelewa kutoka, na ndiyo sababu inayofanya Mombasa wanatuzidi kwa ufanisi” alisema Mwakyembe.
Katika kuimarisha utoaji wa huduma waziri aliwataka TICTS kufanya kazi kwa saa 24 kila siku na kwa siku saba ili kuondoa msongamano wa malori tofauti na sasa ambapo mizigo hupakiwa siku za Jumatatu mpaka Jumatano kuanzia saa 5.00 asubuhi kwa awamu tatu kwa siku kama alivyothibitishiwa na Meneja wa TICTS Bandari ya Dar es Salaam, Daniel Tawale. Akitafuta suluhu ya kero zote za bandarini hapo toka kwa wadau tofauti, waziri alisema kuwa kamati ya muda iundwe ili kwa muda wa siku saba ifanye utafiti na imshauri nini cha kufanya ili kuinusuru bandari hiyo.
“Nataka niunde kamati ndogo sasa hivi ili ichunguze na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike na inipe majibu ndani ya siku saba ofisini kwangu ili niweze kufanya uamuzi sahihi kwa kuwa ni lazima tubadilike ili tuweze kuhudumia wateja wengi wanaotuzunguka” alisema waziri wakati akiunda kamati hiyo.
Waziri aliunda kamati ndogo yenye wajumbe 10 toka sekta tofauti za wadau wa bandari ambayo itaongozwa na Daniel Silla toka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili kuchunguza na kubainisha kero zilizopo bandarini hapo na suluhisho zake.
Wajumbe wengine walioteuliwa ni sekta zao kwenye mabano ni Castrol Felician (TRA), Meshack Gideon (Dereva wa Ndani), Chacha Lukwi (Mshauri wa Madereva), Agness Mathias (KK Security), John Masasi (TICTS), William Kapera (TPA Usalama), Martin Paul (Evergreen Shipping Agent), Jones Jonathan (Wakala Usafirishaji) na Aloyce Gabriel (Wakala Uingizaji).
“Tarehe 03 mwezi Februari nataka ripoti ofisini kwangu ikiwa na uchunguzi mlioufanya ili kuiboresha bandari hii kwa kuwa nataka tuwe bandari ya mfano katika dunia hii” alisema Dk Mwakyembe.

CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment