Rais Kikwete alisema Sensa hutoa taarifa muhimu zinazotumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo ya watu wake.
“Tulitenga siku 14 kwa ajili ya zoezi hili la
Sensa, wengine hizi ndizo walifanya siku za mikutano na maandamano.
Mwaka una siku nyingi, lakini sijui kwa nini walitaka wafanye mikutano
na maandamano hayo katika siku hizi 14 tu?” alisema Rais Kikwete.
Aliwashukuru viongozi wa vyama vya siasa, dini na
vyama vya kiraia pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari ambao
waliwahamasisha watu wao kushiriki katika sensa hiyo akiwataka kuendelea
kuhamasisha matumizi ya taarifa za matokeo ya Sensa hiyo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sensa
hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Serikali kutokana na kutambua
umuhimu wa Sensa, imekuwa ikiongeza bajeti kwa ajili ya shughuli hizo.
Alisema katika Sensa ya mwaka huu, imetoa asilimia 90 ya gharama zote, kulinganisha na asilimia 75 katika Sensa ya mwaka 2002.
Alisema pia katika kutekeleza jukumu hilo kulikuwa
na changamoto mbalimbali ikiwamo ya watendaji wanne kupoteza maisha.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi walipoteza maisha katika mazingira yapi.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema Sensa
ya mwaka 2012, itachangia kuboresha maisha kwa kutumia takwimu sahihi za
wakati ili kuwezesha kutunga sera na kupanga maendeleo.
Alisema matokeo ya Sensa ya 2012 yametoka mapema
kuliko miaka mingine kutokana na maendeleo ya kiteknolojia na utayari wa
Serikali katika kuhakikisha kuwa yanapatikana haraka.Kamishna wa Sensa,
Hajat Amina Mrisho Saidi alisema utoaji wa matokeo ya Sensa kwa mwaka
huu ni jambo la kujivunia, akisema hata nchi zilizoendelea matokeo hayo
huwa yanachukua muda.
“Tanzania tumeweza kutoa matokeo haya ya awali
ndani ya muda wa takriban miezi mitatu tu, kutokana na dhamira ya kweli
ya Serikali kufanya Sensa na uzalendo wa wataalamu na wananchi,”
alisema.
Alisema ofisi yake itahakikisha kuwa machapisho ya
taarifa zote za Sensa, yanatolewa kwa Kiswahili na kusambazwa kwa
wananchi ifikapo Juni, mwaka huu.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Mipango ya Watu, Mary Khan aliipongeza Tanzania kwa kuendesha Sensa na
kutoa matokeo ndani ya muda mfupi.
Alisema matokeo ya Sensa hiyo yatawasaidia watunga
sera na viongozi ikiwa ni pamoja kufanikisha mipango ya maendeleo na
malengo ya kitaifa na kimataifa.
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment