Baadhi
ya wakazi wa mkoa wa Mtwara Mjini wakiwa kwenye maandamano makubwa
waliyoyafanya mapema leo kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar!
Wakazi hao wakiwa na mabango yao yenye jumbe mbalimbali kama
uonavyo pichani
Na Joseph Mwambije,Songea
HIVI majuzi wananchi
wa Mkoa wa Mtwara waliandamana kupinga gesi kusafirishwa kupitia bomba kutoka Mkoa huo kwenda Dares salaam wakitaka vinu vya
kuzalisha gesi vijengwe Mtwara ambako wanadai kuna maeneo mengi badala ya
Daressalaam.
Habari za maandamano hayo
zilipamba Vyombo vingi vya habari huku zikipewa uzito mkubwa kwenye magazeti mbalimbali na kutikisa Mkoa wa Mtwara na Nchi kwa ujumla na kuzua
mjadala mkubwa unaoendelea Nchini.
Maandama no hayo yalikuwa na Lengo moja kubwa kumfikishia
Ujumbe Mkuu wa Nchi kwamba Wanamtwara
wanataka kunufaika na rasilimali zao baada ya kunusa harufu ya kutonufaika na
rasilimali hizo zinazowazunguka.
Waandamanaji hao ambao walikuwa na Mabango yenye ujumbe
mkali tayari yameshafikisha ujumbe ambao
unapaswa kufanyiwa kazi na Kiongozi Mkuu wa Nchi kwa maslahi ya Wananchi wa
Mtwara na Nchi kwa ujumla.
Katika Maandamano hayo ambayo
yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huu zikiwamo Tandahimba na Newala,
yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya
kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.
Walitembea umbali wa kilomita sita, walitoa maazimio tisa mojawapo likihoji sababu za mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na inakochimbwa gesi hiyo.
Katika tamko hilo lenye kurasa mbili, waandamanaji hao wamesema Serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo, huku tayari Rais Jakaya Kikwete akiwa ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam. Wametaka ujenzi huo usitishwe.
Waandamanaji hao Pia walisema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani hapa mwaka 2009 kwamba ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.
Aidha, wanataka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.
“Tunahitaji viwanda vikubwa vijengwe Mtwara ili kuleta ajira kwa wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani, tuna hofu kutokana na ilivyokuwa kwa wakazi wa Songongo (Lindi) kubaki maskini wakati gesi inazalishwa hapo, yasije yakatukuta sisi, hivyo ni lazima tusimamie rasilimali hii ili iweze kuleta maendeleo,” walisema katika azimio lao.
Walibainisha kuwa Serikali haijaeleza athari zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa gesi katika eneo hilo na namna itakavyoweza kusaidia kuziondoa, huku wakitaka gharama za uunganishaji wa umeme wa nyumbani zisizidi Sh50,000 ili kila mwananchi aone ananufaika na gesi hiyo.
Waandamanaji hao walisema gharama za mradi huo wa kusafirisha gesi hadi Dar sa Salaam ni kubwa, hivyo wakashauri Serikali ichimbe gesi ya Dar es Salaam katika kisima namba 7 ili kuepuka hasara.
Kutokana na maandamano hayo kuna
mengi ya kujifunza ambayo Viongozi wetu wanapaswa kujifunza na kubadili mfumo wa kuendesha Nchi ili
unufaishe sehemu husika pia badala ya
kunufaisha Daressalaam pekee.
Hapa kuna tatizo la kimfumo ambalo
linapaswa kufanyiwa kazi ili mambo yaende sawa vinginevyo Wananchi watakuwa wakiandamana kila siku
lakini Viongozi wanaweka pamba masikioni wasisikie kile kinacholalalamikiwa na
wananchi.
Nasema ni tatizo la kimfumo kwa kuwa
maeneo mengi yenye madini yamekuwa hayazinufaishi sehemu husika na tena
wananchi wake wamekuwa maskini wa kutupwa huku madini zikienda kujenga sehemuu
nyingine.
Kwa mfano katika maeneo mengi yenye
madini au miradi mikubwa kodi inalipiwa jijini Daressalaam huku eneo husika
lenye madini au mradi husika linaambulia
patupu na kubaki kuunufaisha mji huo muhimu wa kibiashara maana hiyo ndiyo sifa yake kwa kuwa Mji Mkuu ni
Dodoma.
Angalau basi eneo husika ambako
madini inapatikana ingekuwa inapata
asilimia fulani kwa maslahi ya wananchi wake na kwa maendeleo ya eneo hilo ili
kuondoa migogoro,maandamano na vurugu zinazoweza kuzuilika.
Narudia kusema hili ni tatizo la
kimfumo kwa mfano kuna sera moja ya Mamlaka ya mapato Tanzania(TRA) ya Mlipa kodi anayefikia kulipa kiwango cha
kodi kinachofikia milioni 500 kwa mwaka huyu analipia Makao makuu ya Mamlaka
hiyo jijini Daressalaam.
Mkoa
unabaki na walipa kodi wadogowadogo
lakini wengine wa kiwango hicho cha milioni 500 wanaratibiwa na Makao
makuu na kwa mantiki hiyo basi Wafanyabiashara wakubwa wa kutoka Daressalaam
wanaokuja kufanya biashara Mikoani TRA Mikoani haiwezi kushughulika nao sana
kwa kuwa wanaratibiwa na Makao Makuu.
Hivyo basi hapa panakuwa na ukwepaji
mkubwa wa kodi kwa kuwa wa Mkoani hawezi kushughulika na Mfanyabiashara huyo
kwani hawezi kumsaidia katika kufikia lengo la kukusanya kodi kwa mwaka.
Mfanyabiashara huyo inakuwa rahisi
kudanganya kwa kuwa anaratibiwa na Makao makuu ambao hawajui biashara zake mikoni zinakwendaje.
Nayaeleza haya baada ya kuzungumza
na Maafisa kadhaa wa TRA ambao walizungumza nami kwa masharti ya kutoandikwa
majina yao gazetini.
Katika hili nadhani dhana ya Majimbo
inayopigiwa upatu na Chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA) ina mantiki
kubwa na inapaswa ifanyiwe kazi kwani hata Mataifa makubwa yaliyoendelea kama
Marekani yanaitumia vinginevyo tutakuwa tupiga kelee kila siku kulalamikia
rasilimali kutonufaisha sehemu husika.
Nitoe mfano katika Mkoa wa Ruvuma ambako kuna mgodi
mkubwa wa Makaa ya mawe ambayo yameanza kuchimbwa na pia madini ya Urani ambayo
yako mbioni kuanza kuchimbwa ambayo kama
kodi ingekuwa inakusanya na TRA
Mkoa wa Ruvuma basi Mkoa huo ungepaa katika ukusanyaji wa mapato.
Basi angalau asilimia Fulani
ingeingia katika makusanyo ya kodi ya Mkoa ili kuupaisha Mkoa kimapato badala
ya kila kitu kuwa Daressalaam na kufanya hata Wabunge wetu washinde huko baada
ya kuupata Ubunge kwa kuwa pesa zetu zinakimbizwa huko.
Nimelizungumza hili kwa kuwa
linashabihiana na na lile la Mtwara ambako Wananchi waliandamana kupinga gesi
kusafirishwa kwenda Daressalaam.Tunapaswa kubadili mifumo inayoendesha Nchi na
Sera zake vinginevyo tutabaki kulia kila siku huku machozi yetu yakienda na
maji kama samaki.
Mwisho.
Mwandishi wa Makala hii ni Mchambuzi wa masuala ya kisiasa
kijamii na Kimataifa.
Anapatikana kwa-0755 761195
0655761195
mwambije.blogspot.com
Waandamanaji wakiwa wamekusanyika kwenye moja ya uwanja mjni Mtwara mapema leo wakipinga gesi kusafirishwa kwenda jijini Dar!
No comments:
Post a Comment