Tuesday, July 17, 2012

MHANDO WA TANESCO AICHANGANYA SERIKALI NA WABUNGE

 
Mkurugenzi Mkuu wa shirika Tanesco,William Mhando
FHATUA ya Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, William Mhando imeibua mvutano kati ya wabunge na Serikali.
Mwishoni mwa wiki, bodi hiyo iliwasimamisha kazi Mhando, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Huduma za Tanesco, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Ununuzi,  Harun Mattambo.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walio katika Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na wengine wa Kamati ya Nishati na Madini, wamesema uamuzi huo umejaa maswali kuliko majibu.

Moja ya maswali hayo ni mchakato wa kumsimamisha wakihoji kikao kilichochukua uamuzi huo kuitishwa na wizara badala ya bodi, kupatikana Mkaguzi Kampuni ya Ernst&Young kukagua hesabu za Tanesco bila kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma na tuhuma za ukabila dhidi ya bosi huyo wa Tanesco.

Lakini, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alipoulizwa jana kuhusu tuhuma hizo  za wizara kuingilia mamlaka ya bodi, alijibu: “Kesho (leo) tunakutana na kamati, kwa hiyo siwezi kuzungumza chochote nitazungumza ndani ya kamati.”

Hata hivyo, habari kutoka kamati hizo za Bunge zinasema mkutano kati ya watendaji wa wizara, bodi na wajumbe wa kamati hizo unatarajiwa kuwa na mvutano mkali.

Tayari baadhi ya wajumbe wa POAC wamehoji tuhuma za ukabila ambazo anatuhumiwa kuwa nazo Mhando, huku wakimnyooshea kidole Maswi na waziri wake.

“Hivi Mhando ukabila wake ni nini...? Hivi, tunapaswa kujadili uwezo wa mtu au kabila lake?” alihoji mmoja wa wajumbe wa POAC.

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alipoulizwa kuhusu kikao chao cha kesho alisema tayari wameshamwandikia barua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na wanatarajia kukutana na bodi kupata ufafanuzi.

Kusimamishwa Mhando
Hatua hiyo ya kumsimamisha Mhando ilitangazwa mwishoni mwa wiki na bodi hiyo baada ya kikao cha dharura ambacho kilijadili tuhuma mbalimbali dhidi ya menejimenti ya Tanesco.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wake, Jenerali Mstaafu Robert Mboma na kuchukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Mhando ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

“Hivyo, Bodi iliazimia pamoja na mambo mengine, kama ifuatavyo: Uchunguzi wa tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini,” ilieleza sehemu ya taarifa aliyoitoa Mboma kwa vyombo vya habari.

Mhando aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Juni Mosi, 2010 akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Dk Idris Rashidi ambaye alimaliza muda wake wa uongozi.

Mara baada ya uteuzi huo, Mhando alisema kwamba moja ya mambo ambayo atahakikisha anayatekeleza ni kuhakikisha kuwa wateja wote wa shirika hilo wanakuwa na mita za Luku.

Kabla ya uteuzi huo, Mhando alikuwa ni Meneja Mkuu Usambazaji Umeme na Masoko katika shirika hilo.

No comments:

Post a Comment