|
Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha akiwasilisha
bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa
mwaka wa fedha 2012/13, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
WABUNGE
vijana walioko katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
watapaswa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria
kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2012/13. Waziri wa Ulinzi na JKT,
Shamsi Vuai Nahodha alisema hayo alipokuwa akiwasilisha hotuba ya
makadirio ya wizara yake bungeni jana. Alisema wabunge vijana watakuwa
sehemu ya kundi la kwanza la vijana 5,000 katika mafunzo yatakayoanza
Machi, mwakani.
Alisema wizara hiyo imelifanyia kazi ombi la
kuandaa mafunzo ya JKT kwa wabunge vijana kama ilivyoombwa mwaka jana na
kwamba wabunge hao wameandaliwa mafunzo hayo ya wiki tatu. “Nafurahi
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imelifanyia kazi ombi
hilo na kuandaa utaratibu wa mafunzo maalumu ya wiki tatu kwa
waheshimiwa wabunge vijana,” alisema Nahodha na kuongeza:
“Kwa
hiyo wabunge vijana wataungana na kundi la kwanza la vijana 5,000
niliowaeleza hapo juu… naomba waheshimiwa wabunge mjiorodheshe kwa
maandalizi ya mafunzo haya.” Waziri Nahodha alisema ni imani yake
kuwa, pamoja na wabunge kunufaika na mafunzo hayo, watahamasisha
urejeshwaji wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria na kutoa taswira
nzuri ya mafunzo hayo kwa jamii.
Alisema JKT tayari imefanya
maandalizi ya kutosha na kwamba kambi tano zenye uwezo wa kuchukua
vijana 20,000 kwa wakati mmoja zimeshaandaliwa kwa ajili hiyo. Alizitaja kambi hizo kuwa ni Bulombora na Kanembwa za mkoani Kigoma, Mlale ya Ruvuma, Msange mkoani Tabora na Oljoro hukoArusha.
Hata
hivyo, alisema gharama ya kuendesha mafunzo hayo ni kubwa hivyo JKT
haitaweza kuchukua vijana wote na ndiyo maana imeamua kuanza na hao
5,000. “Vijana hao ni miongoni mwa vijana 41,348 ambao watahitimu mafunzo ya kidato cha sita katika mwaka 2013,” alisema Nahodha.
Kuhusu
utaratibu wa kujiunga na kambi hizo, Nahodha alisema uandikishaji wa
vijana shuleni utafanyika kati ya Desemba mwaka huu na Januari 2013 na
kwamba kambi zitawapokea kati ya Machi 7 na 16, mwakani.Alisema mafunzo
hayo ya miezi sita yataanza Machi 17 mwakani na kuendelea hadi Agosti
16.
Wanajeshi Syria
Katika hatua nyingine, Nahodha alisema
wanajeshi wa Tanzania kati ya 100 na 200 wanatarajiwa kwenda Syria kuwa
waangalizi wa amani ikiwa ni kuitikia ombi la Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa kwa Serikali.
Alisema ombi hilo linatokana na utendaji mzuri wa jeshi hilo na kwamba tayari Serikali imelikubali. Nahodha alisema tayari Makao Makuu ya Jeshi yameanza maandalizi ya kuwapeleka waangalizi hao. Alisema
Tanzania ina wajibu wa kushirikiana na nchi nyingine kulinda amani
duniani na imekuwa ikishiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda
amani.
Katika hatua nyingine; Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema),
Christowaja Mtinda alilalamikia kitendo cha Wahindi kuuza bidhaa za
maduka ya jeshi kwa gharama za juu, wakati bidhaa hizo hazilipiwi kodi. Alisema
ni lazima Serikali ieleze Wahindi hao wanauzaje bidhaa za kwenye maduka
ya jeshi kwa gharama kubwa wakati maduka hayo yanatakiwa yauze bidhaa
hizo kwa bei ya chini.
“Ukienda sasa hivi wanauza sukari Sh1,800
wakati nje ya maduka hayo sukari kilo ni Sh2,000, hili haliwezekani.
Wanauza friji, tv kwa bei ya juu na TRA, maofisa wa jeshi wa ngazi za
juu wote wanajua,” alisema.
Mtinda alitaka suala hilo litafutiwe
ufumbuzi ili bidhaa ziuzwe kwa bei inayotakiwa. Pia alilalamikia nyumba
za maofisa wa jeshi akisema haziridhishi na kwamba zinahitaji
kukarabatiwa upya.
“Nyumba za maofisa wa jeshi zinatia aibu,
hazijakarabatiwa kitu ambacho kinasababisha wafanye ukarabati kwa fedha
zao wenyewe,” alisema.
Wapinzani wang’aka
Kwa upande wake,
Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu wizara hiyo, Mchungaji Israel Natse
aliitaka Serikali kutoa maelezo ya matumizi ya Sh4.048 bilioni ambazo
zilitumika kuondoa matrekta bandarini. “Hakika fedha hizi ni nyingi
sana kwa kazi ya kuondoa tu matrekta bandarini, Kambi ya Upinzani
inataka kupata majibu ni matrekta mangapi yaliondolewa na gharama ya
kuondoa trekta moja ilikuwa kiasi gani?” alisema Natse alipokuwa akitoa
maoni ya kambi hiyo.
Natse ambaye pia ni Mbunge wa Karatu
(Chadema) alisema malipo hayo yanatia shaka na kwamba Serikali lazima
ieleze fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi gani. Kuhusu
migogoro ya ardhi, mbunge huyo alisema kumekuwapo na migogoro kwa muda
mrefu baina ya wanajeshi na wananchi kwenye maeneo mbalimbali ya nchini
na kwamba ni kama hakuna dalili kwamba kuna nia ya dhati ya kumalizwa
kwa matatizo hayo.
“Migogoro hii imesababisha kuwapo kwa mvutano
baina ya wananchi na jeshi letu kwa upande mmoja na viongozi wa wananchi
kwa upande wa pili,” alisema Natse. Alitoa mfano wa maeneo hayo kuwa
ni Ilemela, Tarime, Kunduchi na mengine mbalimbali ambayo yamekuwa
yakilalamikiwa na wabunge kwa muda mrefu.
“Mara zote Serikali
imekuwa ikitoa majibu kuwa itawalipa fidia wananchi ili waweze kuondoka
na kuyapisha maeneo hayo kwa ajili ya jeshi, kwa mwaka huu wa fedha
2012/13 zimeombwa kiasi cha Sh1 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia ya
ardhi maeneo ya Mapinga, Shinyanga na Arusha.” Alisema kutokana na
fedha hizo ni dhahiri kwamba hakuna nia ya dhati ya kumaliza migogoro
baina ya jeshi na wananchi kwani kiasi hicho kilichotengwa ni kidogo na
ni kwa ajili ya kulipa fidia na sehemu chache tu.
“Tunaitaka
Serikali iwe na nia ya dhati ya kuwalipa wananchi fidia ili kumaliza
migogoro hii ambayo inawafanya wananchi walichukie jeshi lao,” alisema. |
|
No comments:
Post a Comment