Thursday, August 30, 2012

Polisi watatu wafariki kufuatia ghasia Mombasa

 Na Mashirika ya habari,
Kenya
Fujo zaendelea Mombasa kwa siku ya pili mfululizo.

Hali ya wasiwasi ingali imetanda mjini Mombasa kwa siku ya tatu baada ya ghasia za siku mbili kufuatia kifo cha mhubiri wa kiisilamu Sheikh Aboud Rogo siku ya Jumatatu.
Inaarifiwa vijana wanalenga kufanya mashambulizi ya kuvizia wakirusha matairi na vifaa vingine barabarani na kisha kutoroka, licha ya kuwa polisi wanashika doria.
Polisi wawili wamethibitishwa kufariki kutokana na majeraha yao baada ya shambulio la guruneti dhidi ya gari lao mjini Mombasa hapo jana.
Hadi kufikia sasa polisi watatu wamefariki tangu kuanza kwa ghasia zilizotokea baada ya kifo cha mhubri wa kiisilamu mwenye siasa kali Sheikh Aboud Rogo siku ya Jumatatu.
Kwa siku mbili, vijana wa kiisilamu wamekuwa wakipambana na polisi katika barabara za Mombasa wakifanya uharibifu kuchoma magari na kupora maduka pamoja na kuvamia makanisa mjini humo. Watu wengine kumi na tatu walijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo.
Mhubiri Aboud Rogo Mohammed, alikuwa mshukiwa wa ugaidi na pia alishukiwa kufadhili kundi la wanamgambo la Al Shabaab nchini Somalia.
Wakati huohuo, watu 12 wamekamatwa na polisi kufuatia makabiliano kati ya polisi na vijana wanaofanya vurugu kufuatia kuuwawa kwa kiongozi wa kidini Sheikh Aboud Rogo siku ya jumatatu.
Katika siku ya pili ya vurugu hizo, wengi ya vijana hao wamekamatwa nje ya Msikiti Musa iliyo eneo la Majengo visiwani Mombasa.
Wakati wa makabiliano hayo polisi walitumia gesi ya kuolisitoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa na ghadhabu.
Hata hivyo katika eneo moja polisi walilazimika kutumia risasi za mpira kuwatawanya vijana waliokuwa wakiwasha matairi barabarini na kufanya uporaji.
Bwana mmoja alichomwa kisu katika karakana yake na kulazimika kupewa huduma ya kwanza na wafuasi wa dhehebu la Jeshi la wokovu.
Na wakati Mombasa ikiwaka moto, wapiganaji wa Al shabaab wametuma ujumbe katika mtandao wao wakiwasihi waislamu wa Kenya "wachukuwe kila hatua zinazostahili kulinda dini yao"
" Waislamu lazima wachukue sheria mikononi mwao, na wasimame kidete dhidi ya makafiri na kuchukua kila hatua kuilinda dini yao, heshima yao ,mali yao na maisha yao kutoka kwa maadui wa waislamu" , Al shabaab wamenukuliwa wakisema hayo katika taarifa yao.
Kiongozi huyo wa kidini Sheikh Aboud Rogo ,aliyepigwa risasi na kuuwa siku ya jumatatu alikuwa ametajwa na Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa kama mtua anayewasajili baadhi ya vijana wa Kenya wkenda kujiunga na wapiganaji wa Al Shabaab.
Sheikh Aboud Rogo pia anadaiwa kuwa alikuwa mfadhili wa kundi hilo la Al shabaab.

No comments:

Post a Comment