Na Mashirika ya Habari
Libya
Balozi wa Marekani nchini Libya
ameuawa baada ya kushambuliwa na watu waliokuwa wamejihami na kuvamia ubalozi
wa Marekani Mashariki mwa mji wa Benghazi.
Balozi J Christopher Stevens, ni
miongoni mwa maafisa wengine wa ubalozi waliouawa kufuatia maandamano kuhusu
filamu iliyotolewa nchini humo ikimkejeli Mtume Muhammad.
Idara ya mambo ya ndani nchini
Marekani, imethibitisha tu kifo cha afisaa mmoja wa ubalozi huo ingawa bado
haijataja jina lake.
Maandamano ya kupinga filamu hiyo
pia yalifanyika mjini Cairo dhidi ya ubalozi wa Marekani.
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya
nje wa Marekani Bi. Hilary Clinton, amelaani mashambulizi hayo.
Serikali ya Libya imetaja shambulio
hilo kama kitendo cha uoga.
Ubalozi huo uliteketezwa na watu
waliojihami kwa bunduki kulalamikia filamu moja iliyotengenezewa nchini
Marekani ambayo wanasema inamdhihaki Mtume Mohammed.
Wanamgambo hao wanaoripotiwa kuwa na
ufungamano na kundi la waislamu wenye msimamo mkali walitumia maguruneti ya
kurushwa kwa roketi kuvamia ubalozi huo kabla ya kuiteketeza. Maafisa wa Libya
wameiambia BBC kwamba hali imetulia kwa sasa.
Machafuko hayo ya Libya yalijiri saa
kadhaa baada ya maelfu ya waandamanaji kukusanyika nje ya ubalozi wa Marekani
mjini Cairo kuelezea hasira zao kuhusu filamu hiyo kumhusu Mtume Mohammed.
Kwa wakati mmoja waandamanaji hao
waliingia ndani ya ubalozi huo na kuichana bendera ya Marekani na kurejesha
yao.
No comments:
Post a Comment