Wednesday, October 31, 2012

Utoro wa wabunge wakwamisha azimio


Ukumbi wa Bunge ukiwa na wabunge wachache jambo lililosababisha kushindwa kupitishwa kwa azimio la bunge la kuridhia marekebisho ya pili ya mkataba wa ushirikiano kati ya Jumuiya ya nchi za Ulaya pamoja na nchi wanachama wa Umoja wa nchi za afrika, Caribbean na Pasifiki, mjini Dodoma, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 


Dodoma
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Kifungu cha 77 (1), akidi kwa kila kikao cha Bunge wakati wa kufanya uamuzi itakuwa ni nusu ya wabunge wote, kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 94 ya Katiba, isipokuwa kwamba, idadi hiyo haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa kubadilisha masharti yoyote ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.
Fuul story


UTORO wa baadhi ya wabunge jana ulikwamisha kupitishwa kwa azimio la Marekebisho ya ya Pili ya Mkataba wa Ushirikiano Kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za Afrika, Caribean na Pacific (ACP).
Hii ni mara ya pili kwa wabunge kukwamisha shughuli za Bunge katika kipindi cha miezi minne kutokana na utoro. Awali, utoro huo ulikwamisha kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Kukwama kwa bajeti hiyo kulikuja wiki moja tu tangu Spika wa Bunge, Anna kukemea tabia ya utoro akisema tabia hiyo ilikuwa imekithiri.
Jana, hali hiyo ilitokea baada ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuhitimisha kujibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia azimio la mkataba huo aliloliwasilisha baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Mara baada ya Waziri Mgimwa kumaliza kujibu hoja ili kutoa nafasi kwa Bunge kupitisha azimio hilo, ndipo Mbunge wa Mkanyangeni (CUF), Mohammed Mnyaa aliposimama na kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya Bunge, Kifungu cha 68 akitaka Bunge lisipitishe azimio hilo kutokana na idadi ndogo ya wabunge waliokuwa ndani ya ukumbi.
Aliomba Bunge lipange muda mwingine wa kupitisha azimio hilo ili marekebisho yaliyopo katika mkataba huo yapitishwe kwa mujibu wa kanuni.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kulipitisha azimio hilo hadi leo asubuhi.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Kifungu cha 77 (1), akidi kwa kila kikao cha Bunge wakati wa kufanya uamuzi itakuwa ni nusu ya wabunge wote, kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 94 ya Katiba, isipokuwa kwamba, idadi hiyo haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa kubadilisha masharti yoyote ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.
Wakati Spika akiahirisha Bunge, baadhi ya wabunge walionekana wakiwa nje ya ukumbi wa Bunge huku wengine wakiwa katika mghahawa uliopo katika viwanja hivyo.
Bunge la Tanzania kikatiba, linapaswa kuwa na wabunge 357.
Akichangia azimio hilo Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliishauri Serikali kuwa makini na mikataba ya kimataifa huku akitaka mkataba huo wa ACP usaidie kurejeshwa kwa Sh360 bilioni zilizofichwa nchini Uswisi na baadhi ya Watanzania.
Mnyika alisema kifungu cha 29 cha mkataba huo kinataja ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuzuia biashara haramu na rushwa.
Alitaka Serikali itumie kifungu hicho kuomba mabilioni ya fedha yaliyofichwa na baadhi ya Watanzania katika benki mbalimbali huko Uswisi.
Suala hili limeibuka bungeni wakati, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe mwishoni mwa wiki iliyopita alikaririwa akimtuhumu , Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kuwa ameiandikia barua Serikali ya Uswisi akieleza kuwa Serikali ya Tanzania haina maslahi na fedha hizo madai ambayo Dk Hoseah aliyakanusha. Zitto alidai kuwa fedha hizo zimefichwa na vigogo 10.

Mbunge wa Kisarawe (CCM), Seleman Jaffo akichangia azimio hilo, aliitahadharisha Serikali kuwa makini wakati wa kuingia mikataba ya kimataifa akisema mingine inaweza kuwa na matatizo kwa taifa.
Alisema Watanzania wasipokuwa makini katika kuingia mikataba ya kimataifa, wanaweza kujikuta wanaridhia mambo yasiyofaa kwa taifa kama vile kukubali ndoa za jinsia moja.
Awali, akiwasilisha azimio hilo, Dk Mgimwa alisema madhumuni ya mkataba huo ni kujenga ushirikiano imara utakaowezesha kujenga uchumi endelevu ili kupunguza umasikini katika nchi wanachama.

Mafao ya kujitoa
Hatimaye, Serikali imesalimu amri na kukubali yaishe baada ya kufuta tangazo lake la Agosti mwaka huu la kusitishwa kwa fao la kujitoa.
Hata hivyo, habari zilizopatikana zinaeleza kuwa hatua hiyo ya Serikali inatokana na kelele za wabunge na wanaharakati ambao kwa zaidi ya miezi miwili, wamekuwa wakihoji juu ya sheria hiyo.
Suala hilo la fao la kujitoa liliibuka katika kikao cha wabunge wakati wakipewa taarifa ya shughuli za Bunge katika Mkutano huu unaendelea kilichokaa jana mchana katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Spika Anne Makinda alilitolea ufafanuzi kwa kueleza kuwa Serikali itawasilisha muswada bungeni kufanya marekebisho ya fao hilo.
Jaffo ambaye alikuwa amewasilisha kwa Spika kusudio la kuwasilisha hoja binafsi kupinga kuondolewa kwa fao hilo, alimwambia mwandishi wetu jana kuwa amepokea barua ya kumpa taarifa kuwa Serikali itawasilisha bungeni muswada wa marekebisho.
Alisema marekebisho hayo yataruhusu mifuko yote ya jamii kuendelea kutoa mafao ya kujitoa kama ilivyokuwa awali.
Mbunge huyo alisema amepokea kwa furaha uamuzi huo wa Serikali ili wafanyakazi waendelee kunufaika na mifuko hiyo ya jamii.
“Nashukuru kilio changu kimesikilizwa na Serikali kwangu mimi huu ni ushindi, kwani wafanyakazi wengi nchini hawana kazi za uhakika,” alisema
Alisema wafanyakazi wengi hususan wa sekta ya madini, hawana uhakika wa ajira hivyo kuondolewa kwa fao la kujitoa kungewapa wakati mgumu.
Mnyika pia alikuwa amewasilisha kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kupinga fao la kujitoa kuondolewa katika bunge hili.
Katika Mkutano wa Nane wa Bunge, Jaffo alipinga sheria hiyo ya kufuta fao la kujitoa alipoomba mwongozo wa Spika na mara baada ya kuwasilisha hoja zake, aliungwa mkono na wabunge wengi isipokuwa Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ambaye alisimama na kutetea sheria hiyo.
CHANZO-MWANANCHI

No comments:

Post a Comment