Friday, November 9, 2012

RC NJOMBE AKABIDHI PIKIPIKI 15 KWA MAKATIBU TARAFA 15 WA MKOA HUO

 Hizi ni pikipiki 15 zilizokabidhiwa Makatibu Tarafa 15 wa Mkoa wa Njombe
 Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sarah Dumba akikagua Pikipiki hizo  huku Mkuu wa Mkoa Bw. Aseri Msangi  akimtazama.
RC  NJOMBE AKABIDHI PIKIPIKI 15 KWA MAKATIBU TARAFA 15 WA MKOA HUO

Na  Joseph Mwambije,
Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Bw. Aseri  Msangi amekabidhi Pikipiki  15 aina ya Yamaha kwa Makatibu Tarafa  15 zenye thamani ya shilingi milioni 33 kwa makatibu Tarafa hao ili kuwarahisishia kazi pindi wanapowatembelea wananchi kuhimiza  shughuli za maendeleo.

Pikipiki hizo zilitolewa hivi karibu katika  Ofisi za Halmahauri ya Wilaya ya Njombe Mkoani humo kwa lengo la kuwapatia vyombo vya usafiri Makatibu Tarafa hao ili waweze kuwafikia wananchi kwa urahisi wanapowatembelea kuwahimiza katika shughuli za maendeleo.

Akikabidhi  Pikipiki hizo Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Makatibu Tarafa hao kuvitumia vyombo hivyo vya usafiri kwa malengo yaliyopangwa na kuwa waangalifu  barabarani kwa kufuata sheria za usalama barabarani.

‘Pikipiki hazina bodi,bodi ni miili yenu wenyewe hivyo mnapasaswa kuwa waangalifu muwapo  barabarani’alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

 Kwa  upande wao Makatibu Tarafa,Linus Malamba wa Tarafa ya  Mwambao,Frola Nyati wa,Tarafa ya Wanging’ombe, wameishukuru Serikali kwa kuwapatia Vifaa hivyo vya usafiri na kubainisha kuwa vitawasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Wanasema kuwa pikipiki hizo zitawasaidia kuwafikia wananchi kwa haraka na kuweza kutatua matatizo yao na kuwapunguzia kazi kwa kuwa wataweza kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.

Hata hivyo baadhi ya Makatibu Tarafa wamekuwa wakitilia shaka ubora wa pikipiki hizo ambapo mmoja wa Makatibu Tarafa hao alisikika akimweleza Mkuu huyo wa Mkoa waziwazi kuwa ubora wa Pikipiki hizo ni mdogo.

Afisa Manunuzi wa  wa Mkoa  wa Njombe Bw. Gaitan Lugenge alipoulizwa kuhusu ubora wa Pikipiki hizo alisema  zina ubora wa hali ya juu na kwamba ni imara na zinapitika katika maeneo ya Makatibu Tarafa hao.

 RC Msangi akizungumza kabla ya kukabidhi Pikipiki hizo.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sarah Dumba.
 Mmoja wa Makatibu Tarafa akijaribu Pikipiki yake
.

 Katibu Tarafa wa Tarafa ya wanging'ombe Frola Nyati akizungumza na Waaandishi wa habari kuzungumzia jinsi Pikipiki itakavyomsaidia kurahisisha kazi na kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Afisa Manunuzi wa Mkoa wa Njombe Bw. Gaitan Lugenge akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana  na makabidhiano ya Pikipiki hizo.

No comments:

Post a Comment