Monday, December 31, 2012

MAANDAMANO YA WANANCHI MTWARA KUPINGA GESI KUSAFIRISHWA DAR YANAFUNUA SERA MBOVU ZINAZOONGOZA NCHI



 Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mtwara Mjini wakiwa kwenye maandamano makubwa waliyoyafanya mapema leo kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar!
 Wakazi hao wakiwa na mabango yao yenye jumbe mbalimbali kama 
 uonavyo pichani
 
Na Joseph Mwambije,Songea
HIVI  majuzi wananchi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana kupinga gesi kusafirishwa kupitia bomba kutoka  Mkoa huo kwenda Dares salaam wakitaka vinu vya kuzalisha gesi vijengwe Mtwara ambako wanadai kuna maeneo mengi badala ya Daressalaam.

Habari za maandamano hayo  zilipamba Vyombo vingi vya habari huku zikipewa  uzito mkubwa kwenye  magazeti mbalimbali na kutikisa  Mkoa wa Mtwara na Nchi kwa ujumla na kuzua mjadala mkubwa unaoendelea Nchini.
Maandama no hayo yalikuwa na Lengo moja kubwa kumfikishia Ujumbe Mkuu wa Nchi kwamba  Wanamtwara wanataka kunufaika na rasilimali zao baada ya kunusa harufu ya kutonufaika na rasilimali hizo zinazowazunguka.
Waandamanaji hao ambao walikuwa na Mabango yenye ujumbe mkali  tayari yameshafikisha ujumbe ambao unapaswa kufanyiwa kazi na Kiongozi Mkuu wa Nchi kwa maslahi ya Wananchi wa Mtwara na Nchi kwa ujumla.
Katika Maandamano hayo ambayo yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huu zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.

Walitembea umbali wa kilomita sita, walitoa maazimio tisa mojawapo likihoji sababu za mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na inakochimbwa gesi hiyo.

Katika tamko hilo lenye kurasa mbili, waandamanaji hao wamesema Serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo, huku tayari Rais Jakaya Kikwete akiwa ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam. Wametaka ujenzi huo usitishwe.

Waandamanaji hao Pia walisema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani hapa mwaka 2009 kwamba ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.

Aidha, wanataka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.

“Tunahitaji viwanda vikubwa vijengwe Mtwara ili kuleta ajira kwa wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani, tuna hofu kutokana na ilivyokuwa kwa wakazi wa Songongo (Lindi) kubaki maskini wakati gesi inazalishwa hapo, yasije yakatukuta sisi, hivyo ni lazima tusimamie rasilimali hii ili iweze kuleta maendeleo,” walisema katika azimio lao.

Walibainisha kuwa  Serikali haijaeleza athari zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa gesi katika eneo hilo na namna itakavyoweza kusaidia kuziondoa, huku wakitaka gharama za uunganishaji wa umeme wa nyumbani zisizidi Sh50,000 ili kila mwananchi aone ananufaika na gesi hiyo.

Waandamanaji hao walisema gharama za mradi huo wa kusafirisha gesi hadi Dar sa Salaam ni kubwa, hivyo wakashauri Serikali ichimbe gesi ya Dar es Salaam katika kisima namba 7 ili kuepuka hasara.
Kutokana na maandamano hayo kuna mengi ya kujifunza ambayo Viongozi wetu wanapaswa kujifunza  na kubadili mfumo wa kuendesha Nchi ili unufaishe  sehemu husika pia badala ya kunufaisha Daressalaam pekee.
Hapa kuna tatizo la kimfumo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi ili mambo yaende sawa vinginevyo  Wananchi watakuwa wakiandamana kila siku lakini Viongozi wanaweka pamba masikioni wasisikie kile kinacholalalamikiwa na wananchi.
Nasema ni tatizo la kimfumo kwa kuwa maeneo mengi yenye madini yamekuwa hayazinufaishi sehemu husika na tena wananchi wake wamekuwa maskini wa kutupwa huku madini zikienda kujenga sehemuu nyingine.
Kwa mfano katika maeneo mengi yenye madini au miradi mikubwa kodi inalipiwa jijini Daressalaam huku eneo husika lenye madini au mradi husika  linaambulia patupu na kubaki kuunufaisha mji huo muhimu wa kibiashara maana  hiyo ndiyo sifa yake kwa kuwa Mji Mkuu ni Dodoma.
Angalau basi eneo husika ambako madini inapatikana  ingekuwa inapata asilimia fulani kwa maslahi ya wananchi wake na kwa maendeleo ya eneo hilo ili kuondoa migogoro,maandamano na vurugu zinazoweza kuzuilika.
Narudia kusema hili ni tatizo la kimfumo kwa mfano kuna sera moja ya Mamlaka ya mapato Tanzania(TRA)  ya Mlipa kodi anayefikia kulipa kiwango cha kodi kinachofikia milioni 500 kwa mwaka huyu analipia Makao makuu ya Mamlaka hiyo jijini Daressalaam.
Mkoa  unabaki na walipa kodi wadogowadogo  lakini wengine wa kiwango hicho cha milioni 500 wanaratibiwa na Makao makuu na kwa mantiki hiyo basi Wafanyabiashara wakubwa wa kutoka Daressalaam wanaokuja kufanya biashara Mikoani TRA Mikoani haiwezi kushughulika nao sana kwa kuwa wanaratibiwa na Makao Makuu.
Hivyo basi hapa panakuwa na ukwepaji mkubwa wa kodi kwa kuwa wa Mkoani hawezi kushughulika na Mfanyabiashara huyo kwani hawezi kumsaidia katika kufikia lengo la kukusanya kodi kwa mwaka.
Mfanyabiashara huyo inakuwa rahisi kudanganya kwa kuwa anaratibiwa na Makao makuu ambao hawajui biashara zake  mikoni zinakwendaje.
Nayaeleza haya baada ya kuzungumza na Maafisa kadhaa wa TRA ambao walizungumza nami kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini.
Katika hili nadhani dhana ya Majimbo inayopigiwa upatu na Chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA) ina mantiki kubwa na inapaswa ifanyiwe kazi kwani hata Mataifa makubwa yaliyoendelea kama Marekani yanaitumia vinginevyo tutakuwa tupiga kelee kila siku kulalamikia rasilimali kutonufaisha sehemu husika.
Nitoe mfano  katika Mkoa wa Ruvuma ambako kuna mgodi mkubwa wa Makaa ya mawe ambayo yameanza kuchimbwa na pia madini ya Urani ambayo yako mbioni kuanza kuchimbwa ambayo kama  kodi ingekuwa inakusanya na TRA  Mkoa wa Ruvuma basi Mkoa huo ungepaa katika ukusanyaji wa mapato.
Basi angalau asilimia Fulani ingeingia katika makusanyo ya kodi ya Mkoa ili kuupaisha Mkoa kimapato badala ya kila kitu kuwa Daressalaam na kufanya hata Wabunge wetu washinde huko baada ya kuupata Ubunge kwa kuwa pesa zetu zinakimbizwa huko.
Nimelizungumza hili kwa kuwa linashabihiana na na lile la Mtwara ambako Wananchi waliandamana kupinga gesi kusafirishwa kwenda Daressalaam.Tunapaswa kubadili mifumo inayoendesha Nchi na Sera zake vinginevyo tutabaki kulia kila siku huku machozi yetu yakienda na maji kama samaki.
Mwisho.
Mwandishi wa  Makala hii ni Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kijamii na Kimataifa.
Anapatikana kwa-0755 761195
                              0655761195
mwambije.blogspot.com 

 

 Waandamanaji wakiwa wamekusanyika kwenye moja ya uwanja mjni Mtwara mapema leo wakipinga gesi kusafirishwa kwenda jijini Dar! 

Monday, December 24, 2012

SONGEA MUNICIPAL COUNCIL SACCO'S,MKUTANO MKUU WA CHAMA WA 20..


Mkutano Mkuu wa 20 wa Mwaka wa Chama cha Ushirika wa Akiba na mikopo cha watumishi wa Manispaa ya Songea uliofanyika tarehe 22/12/2012 katika Ukumbi wa Songea Club.Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa Ruvuma Thabit Mwambungu.
Maandamano yalianzia katika ofisi za Manispaa na kuelekea katika Ukumbi wa Songea Club. 
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu na Viongozi wenzake wakijiandaa kupokea maandamano.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu na Mwenyekiti wa SACCO'S Mpange Skai wakiimba wimbo wa Taifa.
Ukafuatia wimbo maalumu wa Sacco's.
Mwenyekiti wa SACCO'S Mpange Skai akisoma risala ya Ufunguzi.
Meya wa Manispaa ya Songea Mhe Charles Mhagama akimkaribisha mgeni rasmi.
Zawadi za wanachama waliofanya vizuri zilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu.
Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu akifungua Mkutano.
Wanachama wakisikiliza kwa makini.
Meneja wa Sacco's Francis Talewa.
Makamu Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Athumani Luambano.
Mwenyekiti Mpange Skai ikitafakali jambo.
Mwenyekiti wa mikopo ndugu Gideon Masumbuko.
Waliogembea nafasi mbalimbali za Uongozi wa Chama.
Waliongombea  nafasi za kamati ya usimamizi.
Wasimamizi wakihesabu kura.
Walioshida nafasi za  Ujumbe wa Bodi Michaela Mhagama na Peter Mapunda.
Christina Ndimbo.
John Nchimbi.
Mwenyeki Mpangi Skai aliweza kutetea tena nafasi yake.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Joseph Mkilikiti akiwasisitiza wanachama kulipa mikopo kwa wakati.
Dr Daniel Mtamakaya.
Ukafika wakati wa kupiga picha ya pamoja.
CHAMA CHA AKIBA NA MIKOPO CHA WATUMISHI WA MANISPAA YA SONGEA KINA KISIA KUKUSANYA JUMLA YA TSH 600,000,000/= TOKA KATIKA VYANZO VYAKE VYA NDANI.






JWTZ: TUNAMSAKA ASKARI ALIYEPIGA PICHA NA LEMA

 
Mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ),kambi ya Monduli,Arusha akiwa na wabunge wa Chadema,Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na wabunge hao katika Mji mdogo Mererani,Simanjiro mkoani Manyara. 
 


WAKATI Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likihaha kumtafuta aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa amevaa sare za jeshi hilo, mtu huyo ameibuka na kusema yuko tayari kufukuzwa kazi kuliko kuacha kuishabikia Chadema.

Kauli hiyo ya JWTZ imekuja baada ya jana, gazeti hili kuchapisha picha ya mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa JWTZ akiwa amepiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, huku akiwa amenyoosha vidole viwili alama inayotumiwa na Chadema.
Baada ya taarifa hiyo, JWTZ lilitoa taarifa likieleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba linamtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama kweli ni askari wake.
‘‘Kimsingi Jeshi linafanya uchunguzi wa kumtambua mtu huyo kama kweli ni askari,’’ ilisema sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo ambayo iliyatilia shaka mavazi aliyokuwa amevaa mtu huyo kama ndiyo yanayotumiwa na jeshi hilo sasa.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema ingekuwa rahisi kumtambua mtu huyo kwa kuangalia paji la uso lakini alilifunika ili asitambulike.
‘‘Pamoja na hayo, jeshi linamtafuta ili kumchukulia hatua za kinidhamu kutokana Kanuni za Majeshi ya Ulinzi likisema Sheria namba Nne ya Mabadiliko ya Nane katika Katiba ya Nchi ya mwaka 1992, Ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa,’’ ilisema taarifa hiyo.
Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo ni mwanajeshi, moja ya hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.
Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema kuanzia sasa, Jeshi limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika mikutano yote ya siasa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Kuhusu kitendo cha askari huyo kupiga picha na Lema, Kanali Mgawe alisema moja ya masharti muhimu ya askari anapiojiunga na jeshi ni kutambua na kutii sheria inayomzuia kujihusisha na masuala ya siasa na kwamba kitendo cha mtu huyo kimemshangaza na kumfanya amtilie shaka kama kweli ni askari aliyekamilika.
Msimamo wa mtuhumiwa
Kwa upande wake, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa Kikosi cha Chuo cha Mafunzo Monduli (TMA), mkoani Arusha, alisema ni bora afukuzwe kazi kuliko kunyimwa kujiunga na Chadema.
Akizungumza jana kwa sharti la kutotajwa jina akiwa Mirerani, Simanjiro mtu huyo alisema Chadema ni chama makini chenye uwezo wa kuongoza nchi kwani kinatetea wanyonge na kujali masilahi ya jamii.
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI

MKE WANGU AMEUAWA NA MFANYAKAZI MWENZAKE-MUME WA AFISA WA TAKUKURU ALIYEUAWA KWA RISASI

 
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah


 MUME wa aliyekuwa Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), marehemu Bhoke Ryoba ambaye aliuawa juzi kwa kupigwa risasi amesema kifo cha mkewe kimegubikwa na utata mwingi.
 
Akizungumza na jana, mumewe huyo, Charles Gibore, pamoja na mambo mengine alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kubaini ukweli.



“Mke wangu aliuawa na mfanyakazi mwenzake na tukio hilo limegubikwa na utata ambao Takukuru na Polisi ndiyo pekee wanaoweza kutupa ukweli,” alisema Gibore nje ya chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.

Gibore alieleza kuwa mkewe huyo aliuawa usiku wa kuamkia Jumapili katika tafrija ya kuagana na kupongezana na baadhi ya wafanyakazi wenzake wa Takukuru waliokuwa wamepandishwa vyeo, tafrija ambayo Bhoke alipewa zabuni ya kupika chakula.

Alisema pia mkewe aliombwa pia awapatie wenye sherehe hiyo, vijana wawili wa kuwachomea nyama... “Vijana hao walikwenda asubuhi ukumbini ili kuandaa eneo la kuchomea nyama, huku Bhoke akiwa bado nyumbani akiandaa chakula,” alisema Gibore na kuongeza:

“Wale vijana walinieleza kwamba baadaye saa 8:30 mchana, Bhoke na wenzake walifika ukumbini na kuwakuta vijana wawili wanaofanya nao kazi wakinywa pombe, huku wakichezea silaha aina ya bastola kujaribu shabaha.”
“Vijana hao walifyatua risasi juu na ndipo muuaji alipompiga kichwani marehemu katika jicho na mauti yalimfika muda mfupi,” alisema.

Alisema baada ya hapo muuaji huyo alitoweka kisha kujisalimisha mwenyewe katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Temeke, Chang’ombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo alithibitisha mtuhumiwa huyo kujisalimisha na kisha kushikiliwa kituoni hapo na kueleza kuwa amekuwapo hapo Jumamosi iliyopita.

Kamanda Kiondo alisema pamoja na mtuhumiwa huyo kujitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Takukuru, polisi wanaendelea kuchunguza ili kubaini ukweli wa taarifa hizo.
“Tunaendelea kumshikilia hapa na uchunguzi utakapokamilika tutamfikisha mahakamani kwa taratibu nyingine za kisheria,” alisema Kiondo.

Marehemu Bhoke Ryoba alizaliwa Juni 18, 1978 katika Kijiji cha Kiterere, Wilaya ya Tarime mkoani Mara na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao.
Ameacha watoto watatu; Doloresy (10), Dolrisy (4) na Dolrick Gibore ambaye ana mwaka mmoja

CHANZO-GAZETI LA  MWANANCHI

MTANDAO HUU UNAWATAKIA WADAU WOTE HERI YA KRISMASS

This blog has a great pleasure to wish you,Merry Christmas and Happy new year Filled with fun and Celebration

 MTANDAO HUU UNAWATAKIA HERI YA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2013 WENYE FURAHA NA MAFANIKIO TELE.

Wednesday, December 19, 2012

MAZOEZI KABALA YA KUPATA KIFUNGUA KINYWA HUBORESHA AFYA


Mazoezi na Furaha
Daktari mmoja aitwaye Mackod, alipitia makala nyingi za afya ili kuweza  kutambua visababishi vya vifo ambayo havitokani na umri au nasaba ya kiasili (genetic), na akagundua mambo tisa ambayo yanasabisha vifo ambavyo vingeweza kuzuilika.

Mambo hayo tisa ni; uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, ukosefu wa mazoezi, lishe duni, wadudu kama bakteria na virusi, ajali, tabia za ngono za kupita kiasi bila kinga,  vita na madawa ya kulevya.
Katika makala hii ningependa kuzungumzia juu ya ufanyaji wa wazoezi na hasa wakati bora wa kufanya mazoezi.

Mazoezi ni muhimu sana kwa ajili ya kupunguza mafuta ya ziada mwilini, tafiti zinaonesha kuwa asiyefanya mazoezi, madhara anayopata ni sawa na mtu anayevuta tumbaku.
Utafiti uliofanywa na Dr. Jason na Nor Farah (2004) wa Chuo kikuu cha Glasgow, umeonesha kuwa unapofanya mazoezi kabla ya kifungua kinywa, wakati tumbo likiwa tupu, ni bora zaidi kuliko unapoweza kufanya mazoezi baada ya mlo wowote. Kufanya mazoezi ni jambo la maana kwa afya kuliko kutokufanya mazoezi ya mwili, lakini unaweza kupata  faida zaidi kama unaweza kufanya kabla hujala chochote.
Mazoezi kwa ujumla wake yana umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu, hasa kama yakiambatana na lishe bora.

Mazoezi huweza kuzuia magonjwa sugu kama kisukari, magonjwa ya moyo, kansa na shinikizo la damu, pia kwa kufanya mazoezi unaweza kuongeza kipato kwa kuwa unaweza kufanya kazi muda mrefu kuliko asiye fanya mazoezi.

Familia ambazo hufanya mazoezi huwa na afya bora na kipato kikubwa kwa kuwa fedha kidogo wanazopata hutumika kwenye maendeleo ambapo familia wasiofanya mazoezi, hujikuta wakitumia kipato hicho kidogo kwa ajili ya magonjwa ambayo yangeepukika kwa kufanya mazoezi.
Pia kwa kufanya mazoezi kila mara na hasa kabla ya mlo kuna faida nyingi ambazo haziwezi kuonekana kwa haraka, kama vile kuimarisha hali ya kiakili, ambayo matokeo yake ni kuwa na furaha.

Hii inatokana na kuzalishwa kwa wingi kwa kemikali aina ya endorphins wakati wa kufanya mazoezi.

Kemikali hii ya  endorphins  ni muhimu kwenye mapambano ya sonono (depression) na hivyo kumfanya mfanya mazoezi kuwa na furaha zaidi.

Tafiti zinaonesha kuwa mwili huzalisha kemikali hii ya endorphins baada ya mtu kufanya mazoezi ya kawaida kwa dakika 12.

Kama wanafamilia wanaweza kufanya mazoezi kwa muda hata wa saa moja, au nusu saa, wanaweza kuwa na furaha na kuzuia kusambaratika kwa ndoa zao.
Mazoezi na Furaha
Pia kuna kemikali nyingine muhimu ambayo tafiti zinaonesha kuwa huzalishwa baada ya kufanya mazoezi.

Kemikali hii itwayo “serotonin” huongezeka kwenye mfumo wa neva baada ya kufanya mazoezi, ambayo hufanya mfanya mazoezi ajisikie vizuri kiafya na kupunguza sonono (depression). Tafiti pia zinaonesha kuwa kemikali hii, ni muhimu sana katika mwili, kwani hufanya mfanya mazoezi alale usingizi mnono.
Ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara husaidia pia mfanya mazoezi ajithamini, na kuondoa uchovu na unyonge. Unapojithamini, pia inaleta tokeo ya kujiona bora na kuwa mwenye ustawi. Mazoezi pia hufanya tendo la ndoa kuwa bora na hivyo kuleta mahusiano bora ya kinyumba na mpwendwa wako.
Nimejaribu kuanisha umuhimu na faida za maozezi  na hasa wakati  yanapokuwa na tija ili kuleta hamasa ya kufanya mazoezi kwa kila msomaji wa makala hii. Unaweza kufanya mazoezi wewe na familia yako au na wenzako, au pekee yako, chukua muda kidogo katika masaa 24 na ufanye mazoezi, maana utajisikia vizuri na kuwa mwenye afya, lakini kumbuka utapata faida zaidi ukifanya mazoezi wakati tumbo likiwa tupu, yaani kabla ya mlo, baada ya kula chakula tembea taratibu ili kukifanya kitulie vema tumboni.
Usisahau, kabla ya kifungua kinywa asubuhi jitahidi ufanye mazoezi angalau kwa muda wa robo saa.
CHANZO-MTANDAO WA DULLONET