Friday, January 25, 2013

SITA AJIPIGIA CHAPUO YA URAIS


.Asema anafaa  kuwa Rais

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta 
,”
HABARI KAMILI


WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema kwamba anazo sifa za kuwa Rais wa Tanzania na anafikiria kugombea 2015, iwapo dhamira yake itaridhika na mazingira na upepo wa kisiasa wa wakati huo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mtandao huu Sitta alitaja mambo kadhaa aliyoeleza kuwa ni ishara ya kukubalika kwake, ikiwamo kuteuliwa na marais wote wanne; Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete katika nyadhifa mbalimbali ikiwamo ya uwaziri.
Kauli ya Sitta imekuja baada ya kuwapo kwa minong’ono ya baadhi ya wananchi kumtaja kuwa miongoni mwa watu wanaoweza kujitokeza kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
“Ni faraja kusikia watu wakinizungumzia kuwa ninazo sifa (za kuwa Rais). Nami ninaamini ninazo sifa. Wakati utakapofika nitajipima. Kama hali hii itaendelea, basi nitaona ni vizuri nigombee,” alisema Sitta ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge.
Hata hivyo, alisema hana mkakati wowote sasa wa kuendesha harakati za kutafuta nafasi hiyo kwa udi na uvumba kama baadhi ya wengine (bila kuwataja), wanavyofanya... “Sina sababu za kuanza kutafuta support (kuungwa mkono) wala uundaji wa kamati za ushawishi kwa watu sasa,” alisema Sitta.
Badala yake alisema atasubiri hadi muda wa kuchukua fomu za kugombea utakapofika ndipo atakapojitathmini na kusema endapo atabaini kuwa Watanzania wengi wanamuunga mkono, atachukua uamuzi wa kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Aitahadharisha CCM
Waziri huyo aliwahadharisha wanachama wa CCM kwamba wasipokuwa makini, wanaweza kuipoteza nafasi hiyo ya urais na kwenda kwa vyama vya upinzani.
Alionya kuwa iwapo watamteua mtu asiye mwadilifu, Watanzania hawatamchagua na badala yake watampa nafasi hiyo mgombea yeyote kutoka vyama vya upinzani.
Alisema Watanzania wengi wana werevu wa kutosha kujua watu ambao ni mafisadi na ambao wamekuwa wakitumia fedha zao chafu kwa ajili ya kutaka wakubalike mbele ya macho ya Watanzania. Alisema suala la uadilifu ni moja ya vigezo muhimu ambayo CCM wanapaswa kuvizingatia ili kupata ushindi wa kiti cha urais mwaka 2015.
“Ndiyo maana nilipokuwa mbele ya Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba niliweka wazi kwamba Tanzania tunahitaji kuwa na jopo la kuhoji viongozi na wananchi wawe na fursa ya kuwachambua,” alisema Sitta.
Alisema kinachohitajika Tanzania ni mfumo ambao utajenga mazingira ya kuwa na viongozi waadilifu katika ngazi zote.
Alisema hali hiyo itaepusha mfumo unaoonekana sasa wa viongozi kwenye ngazi mbalimbali kuishi kiujanjaujanja, kujinufaisha na kutojali athari kwa uchumi wa nchi na Watanzania kwa ujumla.
Alitoa mfano wa uzembe uliofanywa na viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambao umesababisha Bandari ya Dar es Salaam kupoteza uaminifu kwa nchi mbalimbali zinazopakana na Tanzania.
Alisema uzembe huo umeifanya Bandari ya Dar es Salaam kuingiza Sh38 bilioni kwa mwezi tofauti na Mombasa ambayo inaingiza Sh300 bilioni.
CCM ni imara?
Akizungumzia miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM, mbunge huyo wa Urambo Mashariki alisema anaamini kwamba chama hicho kimefanya vizuri licha ya kuchafuliwa na watu wachache kutokana na tabia zao za ufisadi.
CHANZO-GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment