Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa (kushoto) akisikiliza kwa
makini wakati mawaziri mbalimbali walipokuwa wakieleza ufanisi wa wizara
zao kwenye mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma, jana. Pembeni kwake ni
Katibu mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama.
WASSIRA ATAJWA UKATIBU MKUU, WALIOSHINDA WATAMBIANA, WALIOSHINDWA WATOWEKA
WAKATI matokeo ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya
CCM (Nec), yakiwa yamevuja baadhi ya wapambe wa wagombea walioshinda
wameanza kusherehekea, huku wengine wakitambiana.
Hata hivyo, matokeo hayo yamekuwa machungu kwa baadhi ya vigogo walioanguka wakiwamo mawaziri, wabunge na watu maarufu.
Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuunda sekretarieti mpya baada
ya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar
utakaofanyika leo.
Kwa upande wa Zanzibar, matokeo hayo
yanaonyesha kuwa walioshinda ni pamoja na Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif
Khatib; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri
wa Fedha Zanzibar, Omar Yussuf Mzee, Abdulhakim Chasama na Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.
Wengine
ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Khadija
Hassan Aboud, Bhaguanji Mansuria, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Khamis Mbeto.
Watu maarufu
walioangukia pua katika uchaguzi huo ni Naibu Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk Abdallah Juma Sadallah, mtoto wa Rais Mstaafu,
Abdallah Mwinyi ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Mbunge wa Viti
Maalumu, Kidawa Salehe na Naibu Waziri wa Fedha wa zamani, Abdisalaam
Issa Khatib.
Walioshinda Bara
Majina ya wajumbe wa Nec
walioshinda bara na kura walizopata katika mabano ni Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira aliyeongoza kundi
hilo kwa kupata kura 2,135, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba (2,093), Mwekahazina wa CCM, Mwigulu Nchemba
(1,967), na Katibu wa UVCCM, Martine Shigela (1,824).
Wengine ni
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi (1,805), Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard
Membe (1,455), Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David
Mathayo (1,414), Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome (1,207), Katibu
Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (1,174) pamoja na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Vijana na Michezo, Fenela Mukangara (984).
Wakati
walioshinda Bara na wapambe wao wakitambiana, majina makubwa
yaliyoanguka katika uchaguzi huo ni pamoja ni Mbunge wa Afrika
Mashariki, Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, Richard
Hiza Tambwe na Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri.
Wassira atajwa kumrithi Mkama
Habari
zilizopatikana jana mjini hapa zinaeleza kuwa Wassira, anatajwa kuwa
anaweza kuikwaa nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.
Wengine
wanaotajwa kuwa wanaweza kupata nafasi hiyo ya Katibu Mkuu ni Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye pamoja na Waziri Lukuvi.
Makundi yatambiana
Tambo
na kejeli za wapambe, jana zilitawala katika viwanja vya Ukumbi wa
Kizota unakofanyika Mkutano Mkuu wa CCM, baada ya baadhi ya wajumbe
kuanza kusherehekea kutokana na kupata matokeo.
Nje ya ukumbi huo, tangu asubuhi wapambe wa wagombea hao walionekana wakiwa wamekaa katika makundi huku wakinunuliana vinywaji.
Ingawa
matokeo yalitarajiwa kutangazwa leo, lakini takriban wajumbe wote wa
mkutano huo walionekana kuyapata hali ambayo iliwafanya walioshinda
kupongezwa wakati wakiingia katika ukumbi wa mikutano.
Mtandao huu ulimshuhudia, Waziri Mathayo akipongezwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo nje ya ukumbi wa mkutano asubuhi.
Pamoja na kupongezwa na wajumbe wa mkutano huo hata washindi wa uchaguzi huo nao walipokutana walipongezana.
Mwananchi
lilimshuhudia, Shigela akimpongeza Waziri Wassira na baadaye
walikumbatiana na kupongezana na Nchemba. Baadaye baadhi ya wajumbe
walimbeba Shigela juu juu wakimpa pongezi.
Wakati Shigela
akibebwa, baadhi ya wajumbe walimfuata Wassira na kumpongeza kwa
kumshika mikono na wengine kumkumbatia huku yeye wenyewe akitamba kuwa
ni mwarobani wa Chadema.
Waziri Membe akiwa ndani ya ukumbi wa
mkutano, baadhi ya wajumbe wanaomuunga mkono walimfuata na kumzunguka
huku wengine wakimkumbatia.
Walioanguka watoweka
Wakati
walioshinda wakionekana kufurahi na kupongezwa, hali ilikuwa tofauti kwa
wagombea walioshindwa, kwani baada ya kupata matokeo hayo wengi
walitoweka katika eneo la ukumbi huo.
Kamati ya Uchaguzi yalala ukumbini
Kamati
iliyokuwa ikisimamia uchaguzi huo jana ililala katika ukumbi wa
kuhesabia kura kutokana na kazi hiyo kumalizika usiku wa manane, huku
baadhi ya watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo kunyang’anywa simu zao ili
matokeo yasivuje.
Watu hao waliondoka katika ukumbi wa kuhesabia kura uliopo katika Ukumbi wa Kizota saa 12:00 asubuhi.