WAPAMBE NUSURA WAZICHAPE KAVUKAVU, UCHAGUZI KUFANYIKA DODOMA LEO
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima
WAPAMBE NUSURA WAZICHAPE KAVUKAVU, UCHAGUZI KUFANYIKA DODOMA LEO
Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKATI uchaguzi wa
viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukifanyika
leo, suala la rushwa, makundi na wajumbe kutaka kuzipiga yalitawala
jana.
Uchaguzi huo wa wazazi ndiyo wa funga dimba la mfululizo wa chaguzi za chama hicho tawala kuanzia ngazi za shina tangu Aprili.
Tuhuma
hizo za rushwa zimejitokeza licha ya juzi wagombea mbalimbali
kukaririwa wakiyakana makundi ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na ajenda
maalumu ya kusaka urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kupitia chama
hicho.
Kampeni na rushwa
Mmoja wa wajumbe kutoka mkoani Iringa
aliuambia Mtandao huu kuwa tayari baadhi ya wajumbe wanaoonekana
kuwa na msimamo mkali wamekuwa wakipewa Sh100,000 kila mmoja wakati
wajumbe wengine wamekuwa wakihongwa kati ya Sh40,000 na 70,000.
“Nikimwona
Rais Jakaya Kikwete nitamwambia. Hali hii siyo nzuri na haiwezi
kuvumiliwa. Kama alivyosema juzijuzi hapa nilimsikia, lazima achukue
hatua, la sivyo chama chetu kitakufa,” alisema mjumbe huyo ambaye
aliomba asitajwe jina.
Katika hatua nyingine, makundi ya baadhi ya
wajumbe waliokuwa wameketi katika moja ya baa maarufu mjini Dodoma, juzi
usiku walitimka mbio baada ya kuona gari likiegeshwa pembezoni mwa baa
hiyo.
Wajumbe hao waliokuwa kwenye harakati za kupanga mikakati ya
kuzunguka katika nyumba za kulala wageni kwa ajili ya ‘kuonana’ na
wajumbe, walitimka wakidhani kuwa gari hilo lilikuwa na maofisa wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wagombea
wanaowania uenyekiti, John Barongo na Abdallah Bulembo juzi, kwa nyakati
tofauti walikanusha kuwa na maslahi na makundi yanayodaiwa kushiriki
katika vitendo vya kutoa rushwa katika uchaguzi huo unaofanyika leo.
Mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Martha Mlata alikataa kuzungumzia
uchaguzi huo.
Uchaguzi huo, unahitimisha uchaguzi wa jumuiya tatu za
chama hicho, baada ya ule wa UWT na UVCCM ambazo zilizua malalamiko
kutokana na kutawaliwa na madai ya rushwa.
Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete akifunga mkutano wa UWT na baadaye alipofungua ule wa
UVCCM, alikemea vitendo hivyo na kueleza athari za rushwa katika
chaguzi za chama.
Mchuano wa wabunge
Kama ilivyokuwa katika
uchaguzi wa UWT, mchuano mwingine mkali unaonekana katika kinyang’anyiro
cha ujumbe wa Nec, huku kukiwa na idadi kubwa ya wabunge wanaowania
nafasi hiyo.
Majina 16 yamepitishwa kuwania viti vitatu vya Nec kwa
upande wa Tanzania Bara, wakati kwa upande wa Tanzania Visiwani majina
yaliyopitishwa ni saba kugombea nafasi mbili.
Miongoni mwa wanaowania
nafasi tatu Bara ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam
Malima, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Manyanya na Mbunge wa
Ilala, Mussa Azzan Zungu.
Pia wamo wabunge ambao majimbo yao yapo
kwenye mabano Said Bwanamdogo (Chalinze), Vita Kawawa (Namtumbo),
Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini) na Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu,
Esther Nyawazwa.
Wengine katika kundi hilo ni Norad Kigola, Priscilla
Mbwaga, Dk Salim Chikago, Jeremia Wambura, Bernard Murunya, Thobias
Mwilapwa, Paulo Kirigini na Clementina Mollel.
Kutoka Zanzibar,
wanaowania nafasi mbili za Nec ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Perera Ame Silima, Abdulla Khamis Feruz, Ali Suleiman Othman,
Fatuma Abeid Haji, Panya Ali Abdalla, Twaha Ally Muhajir na Hassan Rajab
Khatib.
Pia mkutano wa leo unatarajiwa kumchagua Makamu Mwenyekiti,
nafasi inayowaniwa na Hassan Rajab Khatib, Ali Issa Ali na Dogo Iddi
Mabrouk.
Utawachagua pia wajumbe wa Baraza Kuu la Wazazi na wawakilishi wa jumuiya hiyo katika mabaraza ya UVCCM na UWT.
Vijembe vya kampeni
Kampeni
zimekuwa zikipamba moto kadri muda wa uchaguzi unavyokaribia na mbinu
mbalimbali zimekuwa zikitumika ili kujihakikishia ushindi.
Magari
mengi yamepambwa picha nyingi za wagombea, wapambe wanapita sehemu
mbalimbali kuomba kura na kuta za uzio wa ofisi za CCM zimechafuka kwa
picha za wagombea.
Ushindani mkubwa unaonekana kuwa baina ya Barongo
na Bulembo ambao jana walikuwa kivutio kikubwa walipokutana katika ofisi
za CCM Makao Makuu, Dodoma ambako walikumbatiana kisha kuanza
kurushiana vijembe.
Bulembo alisema: “Nilipomkuta anachukua fomu,
nilimwuliza mwalimu wangu huyu (Barongo) kwamba nilidhani kwamba sasa
unaniachia nikutue mzigo, kumbe bado tena nawewe unagombea?”
Barongo
alimjibu akisema: “Hilo haliwezekani kabisa, ujue ninyi bado watoto
hamjakomaa bado mnahitaji kuongozwa, kwa hiyo wewe tulia kwanza muda
mwafaka ukifika nitakukabidhi.”
Jana asubuhi, Bulembo alifika katika
Viwanja vya Bunge kuomba kura kwa baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa
mkutano mkuu wa jumuiya hiyo.
Muda mfupi kabla ya wabunge kuingia
ukumbini, Bulembo alikuwa nje ya lango kuu la kuingilia kwenye ukumbi wa
Bunge na kila mbunge aliyejitokeza alimsalimia kisha kuomba kura kwa
wale ambao ni wajumbe hao.
Mlata jana kwa muda mrefu hakuonekana
katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM na taarifa zinasema huenda alikuwa
akihudhuria kikao cha Baraza Kuu la Jumuiya hiyo kilichofanyika jana
katika Chuo cha Mipango.
Licha ya kutokuwapo kwake, kulikuwa na
vijana wachache waliokuwa wamevalia mabango makubwa yenye picha yake,
vifuani na kwenye migongo yao wakimpigia kampeni.
Wafuasi nusura wazichape
Wakati
Bulembo na Barongo wakirushiana vijembe kwa furaha, watu wanaoaminika
kuwa ni wafuasi wao nusura wachapane makonde walipokuwa wakiimba nyimbo
za hamasa CCM Makao Makuu.
Wafuasi hao jana walikuwa wakizunguka
wakiwa na mabango yenye kuwanadi wagombea hao katika ofisi hizo kati ya
saa sita na saa nane mchana huku wakiimba nyimbo za hamasa.
Hali hiyo
ilisababisha kutosikilizana katika eneo hilo, hivyo kuwalazimu maofisa
wa CCM kuviamuru kuondoka na kuelekea katika mbele ya jengo la vikao vya
NEC maarufu kama White House. Viliitikia wito na kwenda huko ambako
viliendelea kuimba nyimbo za hamasa.
Wakati vikiwa katika eneo hilo,
wafuasi hao walianza kurushiana maneno makali kwa huku kila upande
ukidai kufanyiwa rafu na upande mwingine, hali iliyozua tafrani
iliyodumu kwa zaidi ya dakika 20.
Hata hivyo baadhi ya makada wa
pande hizo mbili, walitumia busara na kuwatuliza na kila kikundi
kuelekea upande tofauti na kuhitimisha shamrashara hizo.
Chanzo-gazeti la Mwananchi